Meneja Maendeleo na Biashara wa Benki ya NBC Tawi la Singida, Olairivan Elineema ambaye alikuwa mgeni rasmi akimkabidhi cheti Mhitimu Grace Abdallah kwenye mahafali ya 16 ya wahitimu wa kidato cha Nne katika Shule ya Sekondari ya Dr. Ali Mohammed Shein kwa niaba ya Meneja wa benki hiyo Tawi la Singida mwishoni mwa wiki.
....................................
Imeandaliwa na Dotto Mwaibale,
Philemon Solomon ( 0754-362 990 )
WAHITIMU wa
Kidato cha Nne Shule ya Sekondari ya Dr. Ali Mohammed Shein iliyopo Kata ya
Misughaa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi
mkoani Singida wameambiwa kuwa kumaliza kidato hicho iwe ndio mwanzo wa kuanza
maandalizi ya kuendelea na masomo ya elimu ya juu hivyo wakati wakisubiri
majibu ya mitihani yao wasije wakajiingiza
kufanya vitendo visivyofaa.
Ombi hilo
limetolewa na Meneja Maendeleo na Biashara wa Benki ya NBC Tawi la Singida,
Olairivan Elineema ambaye alikuwa mgeni
rasmi akizungumza kwenye mahafali ya 16 ya wahitimu hao kwa niaba ya
Meneja wa benki hiyo Tawi la Singida mwishoni mwa wiki.
“Mnaporudi
nyumbani yale yote waliyoyakazania walimu wenu kuyaweka kwenye vichwa vyenu
yenye maadili mema tunawaomba wadogo zetu msiende kuyaacha, huko nje kuna kila akili ya mtu kuna wavuta
bange kuna wahuni msiende kuwa wamoja wapo. Mkienda kuwa wema amuwasaidii tu
wazazi wenu ila hata viongozi wenu na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania
Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye anaiangaikia nchi mnakuwa mna mrahisishia
kazi,” alisema Elineema.
Elineema
alisema mbali ya kusaidia viongozi hao pia watakuja kusaidia hadi vizazi vyao
vinatakapo kuja ambapo alitoa angalizo kuwa watakapo haribu maisha yao watakuwa
wamewaambia wazazi wao kuwa hawataki maisha hivyo watakuwa wamefunga hata
furaha za watoto wao ambao wangekuja kuwabariki siku za mbele wakizeeka.
Elineema
aliwataka wahitimu hao wasifunge safari ya maisha ambayo wazazi wao
wamewaanzishia ambapo aliwasihi pindi watakapotoka shuleni hapo waendelee kuwa
na nidhamu ile ile waliyokuwa nayo shuleni na jambo kubwa na la msingi ni kutoacha kumtaja Mungu
kwa kila kitu watakachokuwa wakihitaji kukifanya.
Aidha,
Elineema aliwaomba wahitimu hao wasiangalie njia iliyo mbaya badala yake
waitazame njia iliyo nzuri siku zote za maisha yao na kuwaeleza kuwa hakuna
mzazi ambaye atamuangaikia mtoto wake kuanzia mchanga hadi elimu ya juu na
mwishoni aje amuache akiharibiwa bila kufaidi matunda yake.
Diwani wa
Kata hiyo, Selemani Musa, aliwaomba wazazi na walezi kujenga tabia ya kutoa
chakula kwa ajili ya lishe kwa wanafunzi
wa shule hiyo wanapokuwa shuleni.
“Tujitahidi
kuwa changia watoto wetu liche wakiwa shuleni ili waweze kusoma kwa mfululizo
na bila ya kukosa chakula,” alisema Musa.
Alisema kuwatunza wanafunzi hao na kuwapa
chakula kutawafanya wanafunzi kufanya vizuri kwenye masomo yao ambapo aliomba
utaratibu huo wa chakula uanzie shule za msingi.
Mkuu wa
Shule hiyo, Jacksom Maruma akizungumza wakati akitoa taarifa ya shule hiyo alisema
imeongeza ufaulu wa wanafunzi ambapo kwa mwaka 2023 ufaulu uliongezeka na kufikia asilimia 96.
Akizungumzia
miundombinu alisema walipata msaada wa fedha za Uviko 19 ambapo walipata
madarasa mawili na chumba kimoja cha darasa kutoka fedha Serikali Kuu ambapo pia waliwezeshwa fedha kwa ajili ya
ujenzi wa chumba kimoja cha maabara na ujenzi wa matundu 10 ya vyoo ambapo
walipata fedha za tozo.
Alisema
walipata mifuko 400 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa Hosteli kupitia kwa aliyekuwa Waziri wa Habari,
Mawasiliano, na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye na kuwa
pia wamepokea kompyuta 10, Intanenti routa moja, printa moja kutoka Mfuko wa
Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) na kuwa kwa msaada huo wanakila sababu ya
kumshukuru Mbunge wa Jimbo la Ikungi Mashariki Miraji Mtaturu na Rais Samia
Suluhu Hassan.
Alitaja
baadhi ya changamoto kuwa ni uchakavu wa madarasa, hawana ukumbi wa mikutano,
samani za maktaba, nyumba za walimu, madarasa chakavu na jengo la utawala.
Akizungumzia
kuhusu michezo Mwalimu Maruma alisema wameanzisha kituo cha kuibua vipaji vya mpira wa miguu
kinachojulikana kwa jina la Misughaa Sport Centre.
Mwalimu
Maruma akizungumzia juu ya chakula kwa ajili ya wanafunzi alishukuru
ushirikiano wanaoutoa wazazi kwani wanachakula cha kutosha na kuwa kwenye stoo
yao wana akiba ya kutosha chakula ambacho watakitumia hadi mwakani.
Mjumbe wa bodi ya shule hiyo Fr. Patric Myuku kutoka Jimbo Katoliki Singida aliupongeza
uongozi wa shule hiyo, bodi ya shule kwa kazi kubwa wanayoifanya bila ya
kuwasahau wahitimu na wazazi.
Fr. Myuku aliwaomba wanafunzi hao wawe wapambanaji na kueleza kuwa maendeleo yanahitaji
wanafunzi wanaojibidisha na kuwa wakiwa legelege kwenye masomo hawawezi
kufanikiwa na kuwa maisha mazuri kwa asilimia kubwa yanatokana na shule ambapo
aliwasisitizia sana washike elimu wasiiache iende zake.
Mwenyekiti
wa Bodi ya shule hiyo, Athumani Kitiku alisema katika shule hiyo kuna
changamoto nyingi ikiwemo maabara moja, hosteli kwa ajili ya wasichana ambayo itakuwa
na uwezo wa kuchukua wanafunzi zaidi ya 100 lakini iliyopo haina uwezo huo
hivyo amewaomba wadau na Serikali wawasaidie.
Kwa upande
wake Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Ngwano John
Ngwano aliishukuru Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa
fedha zaidi ya Sh. Milioni 136 katika shule hiyo kwa ajili ya ujenzi wa
miundombinu ambapo alihimiza itunzwe.
“Nina imani
kuwa Serikali itakapopata nafasi tena tutaweza kupata fedha za kumalizia ujenzi
wa maabara ambayo tunayo moja, maboma mawili,” alisema Ngwano.
Aliwahimiza
wananchi kuendelea kuchangia chakula cha watoto shuleni na kueleza kuwa masomo yanakwenda sanjari na
chakula.
Wanafunzi wa
shule hiyo Shadia Hassan na Ntandu Constantino wakizungumza kwa niaba ya wenzao
waliushukuru uongozi wa shule hiyo kwa kuratibu uchangiaji wa chakula shuleni
hapo na muitikio wa wazazi wao kwani unawasaidia kupata masomo bila ya kuwa na
njaa.
“Tuna mshukuru sana Mkuu wa Shule Jackson Muruma na timu yake pamoja na kamati ya shule kwa mpango wa chakula hapa shuleni umetuusaidia sana na zaidi shukurani zetu tunazitoa kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha shule yetu kupata miundombinu bora kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi chini ya Mkurugenzi, Justice Kijazi,” alisema Shadia Hassan.
Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Ngwano John Ngwano akizungumza kwenye mahafali hayo.
Picha ya pamoja viongozi mbalimbali, wahitimu na mgeni rasmi, Meneja Maendeleo na Biashara wa Benki ya NBC Tawi la Singida, Olairivan Elineema.
Muonekano wa baadhi ya majengo ya shule hiyo.











No comments:
Post a Comment