Na Mwandishi Wetu-Morogoro
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imepongezwa kwa
kutekeleza mkakati wa nishati safi ya kupikia kwa vitendo kwa kuweka mfumo wa
huduma hiyo katika shule ya Sekondari Morogoro na Kituo cha Makazi ya Wazee cha
Fungafunga mkoani Morogoro.
Pongezi hizo zimetolewa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt.
Dotto Biteko kupitia kwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dkt James
Mataragio wakati akifungua kikao cha tatu cha Baraza la Pili la Wafanyakazi wa
EWURA kwa niaba ya Dkt. Biteko.
Pamoja na kufungua kikao cha baraza, Pia Dkt. Matarajio alizindua mradi wa
nishati safi na salama ya kupikia katika Shule ya sekondari Morogoro,
uliotekelezwa na EWURA, leo 11 Novemba 2024.
“Napenda kuwapongeza EWURA, wamekuja na jambo tofauti, ambalo lina matokeo
Chanya na tija kwa jamii, sio kufanya tu kikao cha baraza kama vikao vingine,
bali kugusa maisha ya watu, jambo hili litekelezwe na taasisi zote zilizo chini
ya Wizara yetu,” alisema Dkt. Matarajio.
Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dkt. James Andilile akitoa taarifa ya mradi huo,
alisema ni utaratibu wa EWURA kurudisha kwa jamii kwa namna mbalimbali na
kwamba, mradi huo utasaidia wanafunzi zaidi ya 700 wa Shule ya Sekondari
Morogoro na Wazee zaidi ya 104 katika makazi yao Fungafunga.
“Tunaahidi kuendelea kusimamia utekelezaji wa mradi huu ikiwa ni pamoja na
kutoa elimu ya matumizi sahihi na salama ya gesi ya kupikia kwa wapishi,
walimu, wanafunzi na wasimamizi wa makazi ya wazee” alieleza.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Morogoro, Bonifasi Werema, alitoa shukrani kwa
kupatiwa mradi huo ambao ameeleza utasaidia kuimarisha afya za wanafunzi,
walimu na wapishi, kutunza mazingira na kupunguza gharama ambazo zilikuwa
zikitumika kununua kuni.
Bi Rehema Kombe, Mfawidhi wa Makazi ya Wazee cha Fungafunga, alieleza
kufurahishwa kwake na mradi huo, ambao ameeleza utaokoa mud wa kuandaa chakula
kutoka saa tatu hadi dakika 45 na kupunguza gharama za kuni.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA)
Dkt James Andilile, akitoa taarifa ya mradi wa nishati safi na salama ya
kupikia katika viwanja vya shule ya Sekondari Morogoro ambao umedhaminiwa na
EWURA, leo 11 Novemba 2024.
0 Comments