Salma Said (24) akiwa amempakata mtoto wake nyumbani kwao Chamazi Jijini Dar es Salaam.
.......................................................
Na Dotto Mwaibale, Dar es Salaam
MTOTO aliyekuwa akitumia jina la mama Salma of Said mwenye umri wa miezi minne Mkazi wa
Chamazi Islamic Mtaa wa Msufini maarufu kwa Mzee Adi au Chaurembo jijini Dar es
Salaam mwenye kadi ya matibabu namba M82-80-11 ambaye amezaliwa akiwa na kichwa maji (Hydrocephalus) amesitishiwa
matibabu aliyokuwa akiyapata Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Mlonganzila
kutokana na wazazi wake kudaiwa zaidi ya shilingi Milioni 3, baada ya kufanyiwa
matibabu hospitalini hapo.
Salma Said (24) mama wa mtoto huyo akizungumza na waandishi wa habari Machi 25, 2025 alisema hajui hatima ya mtoto wake huyo baada ya kifaa maalumu cha kumtolea maji alichowekewa kuacha kufanya hali ambayo imemfanya mtoto huyo kuwa na kidonda kichwani sehemu kilipowekwa kifaa hicho.
“Siwezi tena kurudi Hospitali kutokana na deni kubwa
tunalodaiwa mbaya zaidi hiki kifaa walichomuwekea kishwani kwa ajili ya kutoa
maji kimeacha kufanya kazi na muonea huruma mwanangu,” alisema Salma huku
akionesha kukata tamaa.
Salma alisema alijifungua mtoto huyo Novemba 19, 2024 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke akiwa na changamoto ya maradhi hayo yanayomsumbua ambapo alilazimika kuhamishiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Mlongazila na kuanza matibabu rasmi.
Alisema yeye na ndugu zake walijichangachanga na kupata fedha za kununua kifaa cha kutoa maji kichwani ambacho kinawekwa kwa gharama ya Sh. 500,000 kwa mara moja ambapo aliwekewa kwa awamu mbili lakini kutokana na mfufulizo wa matibabu yake deni la matibabu yake limefikia kiasi hicho cha fedha.
Alisema familiya yake haina uwezo wa fedha hata kula yao kwa
siku ni ya mlo mmoja tena kwa kubangaiza na wanamtegemea bibi yao kwa kila kitu
na kueleza kuwa hata nyumba ya kuishi kwani
walipo hivi sasa ni eneo la msikiti,
Alisema baba ya mtoto huyo kutokana na kushindwa kulipa deni
hilo baada ya kupunguzwa kazi mkoani Shinyanga aliondoka nyumbani na hajui
alipo.
Salma alisema walijaribu kuomba mtoto wake apate msamaha wa
matibabu dawati la ustawi wa jamii imeshindikana baada ya kuelezwa alipe deni ndipo moto wake aendelee na matibabu hivyo anaomba msaada kutoka
kwa kila mtanzania ili apate fedha hizo na mtoto wake huyo aweze
kuendelea kupatiwa matibabu.
“ Namuomba Rais Samia kama atasikia ombi langu
anisaidie pamoja na watanzania kwani sina furaha ninapo muona mwanangu akiteseka na jinsi tunavyopitia katika wakati huu mgumu,” alisema Salma huku akitokwa na
machozi.
Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Kata ya Mianzini Majimatitu (A) kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Hawa Omari ambaye ndiye amemuibua mtoto huyo ameelezea changamoto za mtoto huyo na kuwaomba wadau mbalimbali kujitokeza kumsaidia ili zipatikane fedha za kulipa deni ili aweze kuendelea kupatiwa matibabu.
Daktari anayemtibu mtoto huyo aliyetambulika kwa jina moja la Rebeca alipopigiwa simu ili kujua uwepo wa deni hilo na kama upo msamaha wa matibabu kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano alisema kwa kifupi kuwa maelezo zaidi ya kujua jambo hilo wahusika waende kwa uongozi wa hospitali hiyo kwa ufafanuzi.
Ugonjwa wa Hydrocephalus dalili zake ni kichwa kuwa kikubwa kupita kiasi, utosi kuvimba, macho kuonekana kuangalia chini, mtoto hukereka haraka (irritability), dege dege na fuvu la kichwa kutofunga vizuri.
Dalili zingine ni kutapika, kuwa na usingizi kila wakati, utapia mlo ambapo ishara nyingine ni macho kutumbukia ndani, na kuwa na muonekano mwingine ambao sehemu nyeupe ya ndani ya macho huwa juu ya ile sehemu nyeusi na kitaalamu huitwa “sun setting appearance.
Kwa mtu yeyote au taasisi ambao wataguswa kumsaidia mtoto huyo anaweza kuwasiliana na mwandishi wa habari hii kwa namba +255754362990 ili kufika nyumbani kwa mama huyo kama livyoelekezwa hapo juu na Mungu atawabariki kwani kutoa kwa ajili ya wengine ni ibada na wala sio utajiri.


.jpg)








No comments:
Post a Comment