BAADHI ya Wananchi wa Kijiji cha Kazole Kusini Mji Mpya Kata ya Vikindu Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani wanalalamikia kupigwa, kujeruhiwa na kubambikiwa kesi huku wenzao wakitumikia vifungo gerezani kwa madai ya kung’oa bikoni kwenye shamba la mtu anayedaiwa kuwa ni Mwekezaji.
Afisa Usalama Mkuu wa Kampuni inayodaiwa kusimamia shamba hilo, Joseph Mwenga aliyefika kwenye eneo ambalo waandishi wa habari walikuwa wakipata maelezo ya wananchi kuhusu jambo hilo huku akiwa ameongozana na walinzi wa jamii ya kimasai waliokuwa wamebeba silaha za jadi alisema kwa kifupi kuwa wao wapo kisheria katika shamba hilo.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge hakuweza kupatikana ili kuzungumzia suala hilo baada ya waandishi wa habari kufika ofisini kwake na kuambiwa na katibu wake kuwa alikuwa kwenye mbio za mwenge.
Hata hivyo Katibu Tawala wa Wilaya ya Mkuranga Omary Mwanga akizungumza kwa niaba ya mkuu wa wilaya hiyo alikiri kujua jambo hilo na kueleza kuwa ni la muda wa miaka mitano sasa na kuwa wananchi hao walimfungulia kesi mwekezaji huyo ambaye alishinda.
“Ninachokijua kama munachouliza kinahusu shamba la Hamidu Barani, wananchi walifungua kesi dhidi yake na mahakama kuu ilimpa ushindi na sisi kama serikali tunasimamia hukumu na maamuzi ya mahakama na si vinginevyo,” alisema Mwanga.
Alisema umiliki wa hati ya ardhi unapositishwa kunataratibu nyingi zinazofanywa ikiwa ni pamoja na kutangazwa kwenye gazeti la Serikali.
Alisema hivi sasa mwekezaji huyo anaendelea na zoezi la kufufua mipaka ya shamba lake hilo kwa kuweka bikoni mpya.








No comments:
Post a Comment