WANANCHI MKURANGA WADAI KUPIGWA, KUHARIBIWA MAZAO YAO NA MWEKEZAJI, WAMUOMBA RAIS SAMIA AWASAIDIE - SINGIDANI BLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Saturday, 12 April 2025

WANANCHI MKURANGA WADAI KUPIGWA, KUHARIBIWA MAZAO YAO NA MWEKEZAJI, WAMUOMBA RAIS SAMIA AWASAIDIE

Mwenyekiti wa Jumuhiya ya Maridhiano na Amani Tanzania ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Siasa  wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kata ya Mtoni, Sikujua Mziray, akizungumza na waandishi wa habari Aprili 7, 2025 (hawapo pichani) kuhusu madai ya Wananchi wa Kijiji cha Kazole Kusini Mji Mpya Kata ya Vikindu Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani kupigwa, kujeruhiwa na kubambikiwa kesi na anayesaiwa mwekezaji.

...........................................

Na Dotto Mwaibale, Mkuranga

BAADHI ya Wananchi wa Kijiji cha Kazole Kusini Mji Mpya Kata ya Vikindu Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani wanalalamikia kupigwa, kujeruhiwa na kubambikiwa kesi huku wenzao wakitumikia vifungo gerezani kwa madai ya kung’oa bikoni kwenye shamba la mtu anayedaiwa kuwa ni Mwekezaji.

Wakizungumza na waandishi wa habari Aprili 7, 2025 wananchi hao wamedai kuwa waliruhusiwa kuendeleza shamba hilo kwa shughuli za kilimo baada ya Rais wa Awamu ya tano Hayati John Pombe Magufuli kudaiwa kufuta hati ya umiliki wa shamba hilo kufuatia aliyekuwa mwekezaji  kushindwa kuliendeleza tangu apewe na kijiji hicho mwaka 1988 ili kuanzisha kiwanda badala yake linadaiwa kuwa na  mifugo isiyozidi 100 wakiwemo mbuzi, ng’ombe na kondoo.

Muwekezaji aliyefutiwa hati hiyo ametajwa kuwa ni Antinyazi Gulamali (maarufu kama Hamidu Barani) ambaye alikuwa akimiliki hekta 1750 ambazo hajaziendeleza hadi leo.

Hamidu ametajwa pia kumiliki Kiwanda cha Soap and Allied Industry kilichopo jijini Dar es Salaam na kuwa tangu amiliki eneo hilo wananchi hawakuwahi  kumuona hadi siku aliyohudhuria mkutano ulioitishwa na aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe.William Lukuvi lakini zaidi ya hapo ni kuendelea kuwepo na matukio ya  kukamatwa na walinzi wa shamba hilo huku viongozi wa Mkoa wa Pwani wakidaiwa kutozungumza chochote kuhusu jambo hilo.

Wananchi hao wamedai kuwa kesi kubwa wanayofunguliwa ni kuingia kwenye shamba hilo na kutoa bikoni na siyo ya kuliendeleza baada ya mwekezaji huyo kuondolewa umiliki wake.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari ambao walifika katika eneo hilo kusikiliza malalamiko ya  wananchi hao, mkazi wa Kijiji hicho Omari Kilumbi alisema wanateseka kutokana na wanaodaiwa kuwa ni walinzi wa shamba hilo kuharibu mazao yao waliyopanda (mihogo na mboga mboga) kwa kuyafyeka na kulisha mifugo jambo lililowafanya wakose chakula (futari) wakati wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

“ Shamba hili limetuletea misukosuko mingi mno ikiwemo ya kupigwa na kujeruhiwa na walinzi hawa, kufyekewa mazao yetu na kufunguliwa kesi ya kung’oa bikoni  halali na kuwekwa haramu wakati siyo kweli kwani zinazoondolewa zipo kwenye shamba hilo zaidi ya miaka mitano ,” alisema Kilumbi.

Kilumbi alisema kwa nyakati tofauti wamewahi kutumikia vifungo gerezani na kuwataja baadhi ya walio jeruhiwa na walinzi hao baada ya kupigwa kuwa ni  Mzee Omari Mtibila, Eliud Ibrahim na Esal Omary.

Aliwataja wanaotumikia kifungo gerezani kuwa ni Aminiel Mshana, Ramadhani Gogi, Haruni Makanjila na Beatrice Kivamba aliyekuwa mjamzito ambaye anatumikia kifungo cha nje baada ya kuwa na mtoto mchanga aliyemzaa wakati akiendelea kutumikia kifungo hicho.

Kikongwe Mwanahamisi Binti Hassan (80) anasema anasikitika  kwa vitendo ambavyo wanafanyiwa na walinzi wa kampuni hiyo hasa cha kuharibu mazao yao na kubomoa vibanda vyao walivyo vijenga katika shamba hilo na kueleza kuwa kulipata shamba hilo hawakubeti ambapo ana muomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan awasaidie.

Kwa upande wake Bibi Nuru Mbonde (64) alisema hali siyo shwari katika eneo hilo wanaharibiwa mazao yao waliyolima na kubomolewa nyumba zao na kibaya zaidi walinzi hao walichana bendera ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) iliyosimikwa katika masikani ya chama hicho waliyoianzisha ndani ya shamba hilo.

“Mama Samia Rais wetu wanawake wenzako na uzee wetu huu tunanyanyaswa utafikiri Tanzania siyo nchi yetu tunaomba tusaidie tunapita katika wakati mgumu kwani polisi wanatukamata na kutufungulia kesi na kibaya zaidi wanaokamatwa ni wale wanaotoa taarifa za kunyanyaswa kwetu tukimbilie wapi sisi jameni ? ” alisema bibi huyo huku akiangua kilio.

Mwenyekiti wa Jumuhiya ya Maridhiano na Amani Tanzania ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Siasa  wa CCM Kata ya Mtoni, Sikujua Mziray alisema chokochoko hizo zilianza baada ya Magufuli  kufuta hati hiyo aliposimamishwa na wananchi Mkuranga na kuzungumza nao alipokuwa akitokea kwenye mazishi ya Rais wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjamin Mkapa Lupaso mkoani Mtwara.

Alisema mara baada ya Magufuli kueleza nia ya kufuta hati ya umiliki wa shamba hilo, William Lukuvi alifika katika kijiji hicho na kuwaambia wananchi wajiunge katika vikundi vya watu watano ili waanze kufanya kilimo  kwenye maeneo ya mabondeni wakati wakisubiri kurasimishiwa rasmi.

“Hii ni neema ya Wilaya ya Mkuranga na vitongoji vyake ambavyo ni vinufaika wa eneo hilo,” walimnukuu Lukuvi alivyo sema.

Alisema baada ya hapo haukufanyika utaratibu wowote wa Serikali Mkoa wa Pwani kuhusu maagizo yaliyotolewa na Lukuvi ambapo wananchi waliendelea kulitumia shamba hilo kwa kilimo na mwaka jana mwishoni ndipo walipoanza kupata madhira hayo.

Alisema jambo la kushangaza ni pale wanapoona shamba hilo likipimwa viwanja vidogo vidogo na anayedaiwa kuwa mwekezaji ambavyo vinadaiwa vitauzwa kwa madalali wakati hati ya umiliki ilisitishwa.

“Tumekuwa katika sintofahamu kwa mambo yanayofanyika katika shamba hili kwani hati ya umiliki  ilifutwa inakuwaje tena aanze kupima viwanja kwa lengo la kuviuza na hakuna kiongozi yeyote aliyefika kuzungumza na wananchi kuhusu jambo hilo huyu ni mwekezaji kweli au mlanguzi wa ardhi yetu ? ,” alihoji Mziray.

Mziray alisema mara nyingi kila wanapohoji kuhusu shamba hilo viongozi wa wilaya hiyo wamedaiwa kutoa madai ya kuwepo kesi mahakama kuu wakidai ilifunguliwa na wananchi dhidi ya mwekezaji huyo kesi ambayo hata namba yake na tarehe iliyofunguliwa hawaitaji.

Alisema kesi iliyopo mahakama kuu ni ile iliyofunguliwa na Kampuni  ya NCG Chemical Industries Limited Company dhidi ya wananchi ambayo inasimamiwa na William Mlacha Meneja wa kampuni hiyo huku kwa upande wa wananchi ikisimamiwa na Mwanasheria waliyemtaja kwa jina  la Alex Enock na wala haihusu shamba hilo.

“ Sisi hatujawahi kuwa na kesi yoyote na mwekezaji huyu zaidi ya ile iliyofunguliwa na kampuni ya Chemical Industries Limited Company shauri namba 209/ 2022 dhidi ya Amiri Malombola na wenzake 60 iliyokuwa mbele ya Jaji Mhina ambayo itupiliwa mbali  na Machi 22, 2024 walifungua kesi nyingine namba 55/130  ya ardhi namba 28132 iliyopo mbele ya Jaji Msafiri ambayo imepangwa kusikilizwa Mei 15, 2025 na kama kulikuwepo kesi iliyofunguliwa na mwekezaji huyo labda ilikuwa baina yake dhidi ya Serikali na siyo wananchi wa hapa ,” alisema Mziray.

 Mziray alisema kisiasa jambo hilo haliposawa kwani lisipofanyiwa kazi kwa wakati upo uwezekano mkubwa wa kuwafanya wananchi kuwa na hasira na  kupunguza kura za Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi oktoba mwaka huu ukizingatia kuwa katika kijiji hicho kuna wananchi zaidi ya  600 kitu ambacho akitakuwa siyo kizuri kumnyima kura Rais Samia  aliye wafanyia maendeleo makubwa watanzania kwa sababu tu ya baadhi ya watu kutaka kupoka ardhi hiyo kiujanja.

Afisa Usalama Mkuu wa Kampuni inayodaiwa kusimamia shamba hilo,  Joseph Mwenga aliyefika kwenye eneo ambalo waandishi wa habari walikuwa wakipata maelezo kutoka kwa wananchi kuhusu jambo hilo huku akiwa ameongozana na walinzi wa jamii ya kimasai waliokuwa wamebeba silaha za jadi alisema kwa kifupi kuwa wao wapo kisheria katika shamba hilo.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Abubakar Kunenge hakuweza kupatikana ili kuzungumzia suala hilo baada ya waandishi wa habari kufika ofisini kwake na kuambiwa na katibu wake kuwa alikuwa kwenye mbio za mwenge.

Hata hivyo Katibu Tawala wa Wilaya ya Mkuranga Omary Mwanga akizungumza kwa niaba ya mkuu wa wilaya hiyo alikiri kulifahamu suala hilo na kueleza kuwa ni la muda wa miaka mitano sasa na kuwa wananchi hao walimfungulia kesi mwekezaji huyo ambaye alishinda.

“Ninachokijua kama munachouliza kinahusu shamba la Hamidu Barani, wananchi walifungua kesi dhidi ya mwekezaji huyo na mahakama kuu ilimpa ushindi na sisi kama Serikali tunasimamia hukumu na maamuzi ya mahakama na si vinginevyo,” alisema Mwanga.

Alisema umiliki wa hati ya ardhi inapositishwa kunataratibu nyingi zinazofanywa ikiwa ni pamoja na kutangazwa kwenye gazeti la Serikali.

Alisema hivi sasa mwekezaji huyo anaendelea na zoezi la kufufua mipaka ya shamba hilo kwa kuweka bikoni mpya. 

 Bibi Nuru Mbonde (64)  akionesha bendera ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inayodaiwa kuchanwa na walinzi wa kampuni inayolinda shamba la mwekezaji huyo.

Kikongwe Mwanahamisi Binti Hassan (80) akizungumzia changamoto wanazo kabiliwa nazo kwenye shamba hilo.
Katibu wa wa Jumuhiya ya Maridhiano na Amani Tanzania, Mashauri Musa akichangia jambo kwenye mkutano huo.
Wakazi wa Kazole wakiwa kwenye mabaki ya matofali baada ya moja ya nyumba iliyokuwa kwenye shamba hilo kubomolewa na walinzi wa shamba hilo.
Mzee Ahmadi Mpate akizungumzia misukosuko wanayo kumbana nayo kwenye shamba hilo.
Wananchi wakionesha shamba la mihogo iliyoharibiwa na walinzi hao.

Wananchi wa Kijiji cha Kazole wakipita kwenye mpaka wa shamba hilo iliyowekwa hivi karibuni na mwekezaji huyo.
Bikoni mpya zikiwa kwenye shamba hilo tayari kwa kuwekwa.
Bikoni ya zamani ikioneshwa.
Bikoni mpya zinazodaiwa kuwekwa na mwekezaji huyo katika shamba hilo baada ya kuzitoa za zamani

Muonekano wa bikoni za zamani zikiwa kwenye shamba hilo.

Wananchi wakiwa kwenye shamba hilo wakiwaonesha waandishi wa habari uharibifu wa mazao yao yanayodaiwa kuharibiwa na walinzi wa shamba hilo.
Muonekano wa shamba la mihogo iliyolimwa na wananchi katika shamba hilo.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad