Katibu Mkuu Taifa wa Chama cha kutetea Haki na maslahi ya Walimu Tanzania (CHAKAMWATA), Mwalimu Meshack Kapange akizungumza na waandishi wa habari Aprili 5, 2025 ofisini kwake Jijini Mbeya.
.....................................
Na Zuhura Jafari, Mbeya
CHAMA cha kutetea Haki na maslahi ya Walimu Tanzania (CHAKAMWATA) kimedai kusikitishwa na hotuba Iliyosomwa na Umoja wa Wafanyakazi Tanzania (TUKTA) katika Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani Mei Mosi mbele ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano Wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan yaliyofanyika kitaifa mkoani Singida.
Katibu Mkuu Taifa wa Chakamwata, Mwalimu Meshack Kapange akizungumza na waandishi wa habari Aprili 5, 2025 ofisini kwake Jijini Mbeya ,alisema hotuba hiyo ambayo alidai ni chonganishi dhidi ya vyama vya wafanyakazi ilimtaka Rais arekebishe sheria na kuzuia kuanzishwa kwa vyama vingine vya wafanyakazi .
"Sisi kama chama cha kutetea maslahi ya walimu tumesikitishwa na sehemu ya kipande cha hotuba hiyo ambacho kilikuwa kikiomba sheria zirekebishwe ili wafanyakazi wakose uhuru wakuanzisha vyama vya kuwatetea," alisema Kapange.
Kapange alisema uchochezi na uchonganishi wa namna hiyo hauwezi kuvumiliwa na watetezi wa maslahi ya wafanyakazi popote pale duniani.
Aidha, Kapange alikosoa sababu za Tukta za kudai kuwa kuanzishwa kwa vyama vingi katika sekta moja vinaweza kuondoa amani na utulivu jambo ambalo amelipinga vikali .
Katika hatua nyingine Kapange amewakosoa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), kwa kuchunguza mapato ya Chakamatwa na kuwataka kuanza kujichunguza wao namna wanavyotumia fedha za walimu huku akiwataka viongozi wa chama hicho watoe maelezo kwa wanachama wao jinsi michango yao inavyotumika na kuacha kufuatillia utendaji kazi wa Chakamwata.
Mvutano huu ambao umeanza kuibuka dhidi ya vyama hivyo hapa nchini hasa katika sekta ya Elimu Chakamwata kama chama kipya kinaonekana kukabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa vyama vilivyozoeleka kama CWT na TUKTA.









No comments:
Post a Comment