UCHAGUZI MKUU 2025: CCM YAJIVUNIA MTAJI WA WANACHAMA MILIONI 13 - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Thursday, June 5, 2025

UCHAGUZI MKUU 2025: CCM YAJIVUNIA MTAJI WA WANACHAMA MILIONI 13


Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan alipokuwa akizungumza kwenye mkutano mkuu maalum wa CCM ambao ulifanyika jijini Dodoma kuanzia Mei 29, 2025 hadi Mei 30, 2025.

..........................................

CHAMA cha kisiasa ni maungano ya watu wanaotafuta mamlaka katika dola na hasa serikali kwa kusudi la kutekeleza shabaha za kisiasa au za kifalsafa pamoja na faida za kimaendeo kwa wanachama na wananchi.

Tanzania tangu ipate uhuru kutoka kwa wakoloni chama ambacho kimekuwa madarakani ni Chama Cha Mapinduzi (CCM) na hiyo ni kutokana na uongozi dhabiti wa viongozi wake na sera nzuri ambazo zimekifanya chama hicho kuwa na wanachama wengi kutokana na kujiunga nacho.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni Chama kikongwe, chenye nguvu na mvuto si kwa Tanzania tu bali na barani Afrika na kuwa ni chama pekee cha ukombozi kilichoshiriki kupigania uhuru katika nchi nyingi zilizokusini mwa jangwa la sahara.

Baadhi ya nchi duniani hasa bara la Afrika zimekuwa zikifika Tanzania kujifunza namna CCM inavyofanya shughuli zake.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilianzishwa rasmi Februari 5, 1977 baada ya kuunganishwa kwa vyama vya Tanganyika African National Union (TANU) kilichokuwa chama tawala Tanzania Bara, kikiongozwa na Rais wa Kwanza wa Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Chama cha Afro-Shirazi Party (ASP) kilichokuwa chama tawala Zanzibar, kikiongozwa na Rais wa kwanza wa Zanzibar Sheikh Hayati Amaan Abeid Karume.

Chama hiki tangu kuanzishwa kwa vyama vingi mwaka 1992 kutokana na kuwa na sera nzuri na viongozi makini kimendelea kushinda katika chaguzi mbalimbali huku kikipata idadi kubwa ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Viongozi walioshinda Urais kwa tiketi ya CCM kwenye chaguzi hizo ni Hayati Benjamin Mkapa, Jakaya Mrisho Kikwete na Hayati Dk. John Joseph Pombe Magufuli na viongozi wengine ambao wamekiongoza chama hicho kupitia nafasi ya Urais ni Hayati Ali Hassan Mwinyi na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye aliingia madarakani kufuatia kifo cha mtangulizi wake Hayati Dkt. John Pombe Magufuli,

Dkt. Samia aliingia madarakani kikatiba kutokana nafasi ya makamu wa rais aliyokuwa nayo.

Mwaka huu Taifa la Tanzania litakuwa na tukio kubwa la uchaguzi mkuu wa kuwachagua madiwani, wabunge na Rais ambapo  vyama mbalimbali vitashiriki uchaguzi huo baada ya kupita uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Mitaa,

CCM inaingia kwenye uchaguzi huo huku ikiwa na mtaji wa wanachama zaidi ya Milioni 13 ikiwa ni ongezeko kubwa ambalo alijawahi kutokea tangu kuanzishwa kwa chama hicho mwaka 1977.

Ongezeko hilo la wanachama limetokana na kazi nzuri ya Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kuratibu zoezi la kitaifa la chama hicho la kusajili wanachama wote na wapya kwa njia ya kimtandao kwa kushirikiana na watendaji wake kupitia Jumuiya za chama hicho.

Dkt. Samia akizungumza kwenye mkutano mkuu maalum wa CCM ambao ulifanyika jijini Dodoma kuanzia Mei 29, 2025 hadi Mei 30, 2025 alisema hadi kufikia Mei 29 mwaka huu, idadi ya wanachama wa chama hicho ni 13,000,670. 

Idadi hiyo kubwa ya wanachama imepatikana baada ya Dkt. Samia kuhimiza kila jumuiya kwenda kuzungumzia kazi nzuri zilizofanywa na Serikali chini ya chama hicho katika kutekeleza ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020/ 2025 ambayo imefanya mapinduzi makubwa ya maendendeleo kwenye sekta za afya, elimu, maji, barabara, umeme na maeneo mengine. 

Kutokana na kunadi mafanikio hayo ya Serikali ambayo yanaonekana wananchi wakaanza kujiunga na CCM kwa makundi na kujisajili katika mfumo wa kimtandao (Kieletroniki) ulioanzishwa na Dkt. Samia ambaye alitoa vishikwambi nchi nzima kwa ajili ya kufanya kazi hiyo ambayo imezaa matunda kwa  kupata wanachama hao. 

Ushirikiano mkubwa wa watendaji wa chama hicho kupitia jumuiya zake na viongozi wengine ambao waliwiwa kuunga mkono jitihada za Mwenyekiti wao wa Taifa Dkt. Samia za kunadi mafanikio ya utekelezaji wa ilani ya CCM na kujitoa kwao kununua simu na vishikwambi kwa ajili ya kusaidia kuongeza kasi ya kusajili wanachama zimesaidia kupatikana ongezeko hilo la wanachama. 

Ziara za viongozi na mikutano ya hadhara ambayo ilikuwa ikifanyika nchi nzima kuanzia viongozi wa juu wa kitaifa wa CCM, kusiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi, kukagua miradi ya maendeleo na kuelezea mafanikio ya Serikali katika kutekeleza miradi ya maendeleo zimesaidia kuwafanya wananchi na wanachama wa vyama vingine kuiamini Serikali na kujiunga na chama hicho. 

WANA CCM WANAZUNGUMZIAJE ONGEZEKO HILO LA WANACHAMA

 

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Tanzania Bara, Stephen  Wasira, alisema idadi kubwa ya wanachama waliosajiliwa ndani ya chama hicho inatosha kukifanya CCM kuendelea kushika dola na kubaki madarakani.  

Wasira alitoa kauli hiyo Januari 23, 2025, baada ya kupokewa na wanachama wa CCM Makao Makuu ya chama hicho, jijini Dodoma.

Akizungumza mbele ya mamia ya wanachama waliojitokeza, Wasira alisema, "Kwa mtaji wa wanachama tuliowasajili, CCM ina nguvu ya kuendelea kushika madaraka na kuleta maendeleo endelevu kwa Watanzania."  

Akiwa kwenye mkutano huo, Wasira aliwakumbusha wanachama na viongozi kuwa mwaka 2025 ni mwaka muhimu wa uchaguzi wa Rais, Wabunge, na Madiwani, na hivyo aliwataka wanachama waendelee kuwa imara na kushirikiana kuhakikisha chama kinapata ushindi wa kishindo.  

"Huu ni mwaka wa uchaguzi, ni lazima tuhakikishe tunadumisha mshikamano, tukitekeleza sera zetu kwa ufanisi, na kuendelea kuwahudumia Watanzania kwa uadilifu," alisema Wasira. 

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Michael Lushinge Masanja (Smart), ambaye naye kwa namna moja alichangia vishikwambi kwa ajili ya kusaidia kusajili wanachama alipokuwa Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Misungwi alianza kwa kumshuru Mwenyekiti wa Taifa wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha jambo hilo baada ya kulichukulia uzito mkubwa kwa kuliwezesha na wao  kama chama wanajivunia sana jambo hilo la msingi.

“Sisi wafanyabiashara mtaji wetu ni kuwa na rasilimali ya wateja kwani ili kujua  kama imekuwa ni ile idadi ya watu inayoongezeka  na halikadharika mtaji mkubwa wa siasa ni kuwa na wanachama wengi na hasa wakati huu tunapoingia kwenye uchaguzi mkuu tunajivunia kuwa na wingi wa wanachama,” alisema Smart  .

Alisema kwanza tu wana mtaji wa wanachama zaidi ya Milioni 13 hapo bado marafiki, ndugu, jamaa wa wanachama hao huku akijitolea mfano kuwa katika shughuli zake za biashara ameajiri watu karibu 300 ambao wanamuombea mema huku akisisitiza kuwa wafanyakazi wake hao na wao wana marafiki zao ambao moja kwa moja watakuwa ni sehemu ya wanachama hao hivyo wanajivunia sana.

“Tunampongeza Mhe. Rais mafanikio yake ni makubwa sana kwa haraka haraka chama chetu kinakwenda kuwa na rasilimali ya wanachama zaidi ya Milioni 20 hapo hakuna muujiza wa kumfanya mtu ajitokeze akilalamikia ushindi wa CCM kwani mtaji tulionao ni mkubwa mno,” alisema.

Katibu wa CCM Wilaya ya Nkinga, Stamili Dendego alisema kazi kubwa aliyoifanya mwenyekiti wao Taifa ni kubwa mno hasa katika ongezeko la wanachama ambao ni mtaji mkubwa katika uchaguzi mkuu.

“Idadi hiyo itaendelea kuongezeka kutokana na maelekezo tuliyopewa katika mkutano maalum uliofanyika jijini Dodoma,” alisema Dendego.   

Mwana CCM na Mdau wa Maendeleo, Joseph Nyarandu kutoka Kintiku Wilaya ya Manyoni Mkoa wa Singida, alisema wanajivunia uimara wa CCM na Serikali chini ya Rais Samia kwa uongozi dhabiti na wa wazi ndio unaokifanya  chama hicho kupendwa na kukimbiliwa na watu wengi.

“CCM kimejengwa kwa misingi ya demokrasia, utu na kujali maslahi ya watu wote pasipo ubaguzi wa aina yoyote ni chama chenye viongozi wenye weledi wa hali ya juu na ni chama cha mfano,” alisema Nyarandu.

Alisema ongezeko hilo la wanachama ni kazi nzuri anayoifanya Rais Samia ya kukijenga na kukiimarisha chama hicho na kukifanya kuwa cha kisasa zaidi hivyo wanajivunia mafanikio hayo.   

Kwa upande wake Katibu wa CCM Wilaya ya Chamwino, Ibrahim Said Mpwapwa alimshukuru Mwenyekiti wa chama hicho Taifa Dkt. Samia kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kukiwezesha vitendea kazi hasa usafiri wa magari, pikipiki na baiskeli jambo ambalo limewafanya watendaji wa chama hicho kupitia jumuiya zake kufika kila sehemu kutekeleza majukumu yao.

“ Jambo hili la kuwezeshwa vifaa vya usafiri limechagiza kwa kiasi kikubwa kuongeza idadi hiyo ya wanachama hakika tunamshukuru sana mwenyekiti wetu,” alisema Mpwapwa.

Alisema jambo lingine ambalo limewafanya wananchi kukiamini chama hicho na kujiunga nacho ni Serikali chini ya CCM jinsi ilivyofanya kazi kubwa ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo huku mingine ikiwa imekwisha kamilika.

Naye Katibu wa CCM Wilaya ya Ruangwa, Abbas Mkweta alisema ili chama kiwe hai ni lazima kiwe na wanachama hivyo kupata idadi hiyo ya wanachama kinaonesha jinsi chama kilivyo na nguvu na hai..

“Jambo hili haliji tu hivi hivi bali inatokana na kazi nzuri iliyofanyika kama unavyojua hivi sasa siasa ni kama biashara ambayo inakuwa na ushindani kwani ukipeleka bidhaa mbovu sokoni hakuna mteja ambaye ataweza kununua na ndivyo ilivyo hata kwenye siasa sisi bidhaa zetu ni huduma,” alisema Mkweta.

Alisema kama chama wanatoa huduma kwa wananchi kama walivyoahidi na yamefanyika kwa kiwango kikubwa hivyo watanzania wengi kuvutiwa na chama hicho na hilo ndio jambo kubwa.

Alisema Rais Samia alipokuwa anaachiwa nchi kutoka kwa mtangulizi wake Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kufuatia kifo chake kuna watu walimbeza kuwa ni mwanamke hataweza lakini tumeona jinsi anavyoiongoza nchi kwa misimamo yake na uimara na hatua ambazo amekuwa akizichukua pale anapoona mambo hayaendi sawa.

Alisema wakati anaingia madarakani baadhi ya watu walikuwa na mashaka naye lakini chini ya uongozi wake nchi imetulia, kuna usalama wa kutosha na amefanikiwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa kiwango cha juu na mingine ikiendelea.

Alitaja baadhi ya miradi hiyo ni Bwawa la kufua umeme la Nyerere, Daraja la Kigongo la Busisi, Reli ya Kisasa ya SGR, Daraja la Selander hiyo na kuwa hiyo ni sehemu ya miradi ya Dar es Salaam na kwa Wilaya ya Ruangwa ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami kutoka Nanganga hadi Ruangwa mjini jambo ambalo linawafanya wananchi wafurahi na kusafirisha mazao yao ya biashara kama korosho, ufuta, mbaazi na mengineyo ya chakula.

 Mwana CCM na Mdau wa maendeleo wa chama hicho kutoka Mkoa wa Mara Mhandisi Yazid Mabala alisema ongezeko hilo la wanachama ni mtaji mkubwa wa CCM huku akielezea kwamba katika sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 watanzania wote walikuwa ni  Milioni 61, 841, 924 watoto chini ya miaka 18 wakiwa ni Milioni 30, 257, 196 na watu wenye umri wa kupiga kura ambao walikuwa na umri kuanzia miaka 18 kwenda juu wakiwa ni Milioni 31, 583, 924.

Alisema kwa takwimu hizo inaonesha wana CCM ambao wapo juu ya umri wa kupiga kura ni asilimia 41. 2 hivyo tafsiri yake kisiasa chama hicho kitaingia kwenye uchaguzi tayari kikiwa na wanachama ambao watakuwa ndani ya chama hicho.

“ Hii ni hazina kubwa ya chama chetu kutokana na watu kukielewa kwa kila kitu kwani iwapo kutakuwa na wapiga kura 100 CCM tutakuwa na asilimia 41 ya wapiga kura ambao hawatingishiki, hawahami na wapo na chama hicho kihisia na kiitikadi,” alisema Mabala.

Aliongeza kuwa asilimia ya wanachama hao waliobaki watafanya mikakati mbalimbali ili kuongeza asilimia hizo zilizobaki na kukifanya chama hicho kupata ushindi.

Alisema CCM ilijenga imani kubwa  kupitia kusajili wanachama na kukifanya kieleweke na ongezeko hilo ni faida kubwa kwa chama hicho hasa kwa Dkt. Samia ambaye alikuja na mkakati huo wa kusajili wanachama ambao umekiimarisha.

Alisema mkakati wa kwanza aliokuja nao Dkt. Samia ni kununua simu nne ambazo zilipekekwa katika kila kata nchi nzima huku kila eneo likiwa na mkakati wake na kauli mbiu za kuhamasisha watu kujisajili ambapo kwa Mkoa wa Mara walikuwa na kauli mbiu yao waliyoipa jina la siku kumi za moto za mama iliyokuwa na lengo la kutoa hamasa watu kwenda kujisajili na kuwekwa kwenye kanzidata kwa ajili ya kutambulika.

Makala hii imeandaliwa na Dotto Mwaibale namba ya simu (O754362990)

Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi akiwa kwenye mkutano huo.

Mwenyekiti Mstaafu wa CCM na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete na Makamu Mwenyekiti wa CCM

na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi wakishiriki katika mkutano huo. 
Wajumbe wakiwa kwenye mkutano huo.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Ndugu Michael Lushinge Masanja  (Smart), akimuelekeza jambo Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), CPA Amos Makalla alipokuwa katika moja ya ziara zake mkoani humo.
Mwana CCM na Mdau wa maendeleo wa chama hicho kutoka Mkoa wa Mara Mhandisi Yazid Mabala
 Katibu wa CCM Wilaya ya Chamwino Dodoma, Ibrahim Said Mpwapwa
Mwana CCM na Mdau wa Maendeleo, Joseph Nyarandu akionesha ' miaka mitano tena kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan'
Katibu wa CCM Wilaya ya Nkinga, Stamili Dendego. 

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad