WANANCHI ni Mabingwa tena. Hii si hadithi ya kubahatisha, bali ni sura nyingine ya mafanikio yaliyopikwa kwa maono, nidhamu, na uthabiti wa kiutawala unaovuka mipaka ya kawaida. Klabu ya Young Africans SC imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mara ya 31 kihistoria, na kwa msimu wa nne mfululizo, ikimaliza kileleni kwa pointi 82 dhidi ya Simba SC waliomaliza na pointi 78.
Katika mchezo wa kufunga msimu uliozikutanisha timu mbili kubwa nchini — Yanga 2-0 Simba, mabao kutoka kwa Pacome Zouzoua (penalti dakika ya 66) na Stephane Aziz Mzize (dakika ya 86) yameweka rasmi alama ya uthibitisho wa utawala wa Yanga kwenye ramani ya soka la Tanzania.
Uongozi Bora wa Eng. Hersi — Ramani ya Mafanikio
Mchambuzi wa soka, Hans Rafael, alilieleza hili kwa uzito unaostahili:
> “Mpira ni mipango. Na mipango inahitaji ubongo thabiti. Eng. Hersi ni ‘mastermind’ wa Yanga. Kama Real Madrid walivyo na Perez na Al Ahly walivyo na El-Khatib, basi Tanzania tuna Eng. Hersi.”
Ni kweli isiyofichika — klabu ya Yanga imedhihirisha kuwa na uongozi imara, wenye maono, weledi na uamuzi wa haraka. Mabadiliko ya benchi la ufundi, usajili wa wachezaji sahihi na uthabiti wa kimfumo umeifanya Yanga isiwe tu timu ya ushindi, bali taasisi ya kutazamwa na kuheshimiwa ndani na nje ya mipaka ya nchi.
Kocha Milloud Hamdi — Ubora Bila Kujitangaza
Alipotua Jangwani, wengi walimwona kama ‘kocha wa majaribio’. Lakini leo, Milloud Hamdi amethibitisha kuwa si jina la CV linaloshinda, bali mbinu, uthubutu na uchu wa ushindi. Hajajiinamia hata mara moja. Ameshinda mechi kubwa kwa maamuzi ya kiufundi yaliyowabeba vijana wake hadi kufika kileleni.
Kwa mujibu wa Haji Manara, Yanga inapaswa kumwongezea mkataba kocha huyu na kumpa mradi wa muda mrefu:
“Ni kocha mwenye njaa ya mafanikio hata timu ikiongoza tano, bado anasisitiza bao zaidi. Rotation yake ni ya kiwango.”
Wachezaji: Mashujaa wa Jukwaa la Ushindi
Katika orodha ya waliotukuka, jina la Pacome Zouzoua linang’aa kama almasi. Akiwa amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mechi ya Dabi ya Kariakoo, huu ni ushindi wake wa tuzo ya tisa msimu huu. Kupitia ukurasa wake wa Instagram, ameandika kwa hisia:
> “Ubingwa huu ni thawabu ya kazi ngumu, ari ya timu, na upendo wa kweli kwa mchezo.”
Kwa upande mwingine, Jean Charles Ahoua amemaliza msimu kama mfungaji bora wa ligi (magoli 16), akiendeleza mila ya Yanga ya kuibua mashujaa kila msimu.
Kumbukumbu Kutoka kwa Sead Ramovic
Kocha wa zamani wa Yanga, Sead Ramovic, kwa sasa akiwa CR Belouizdad, ameandika kwa mapenzi makubwa:
> “Ninajivunia kuwa sehemu ya safari hii. Huu ni ushindi mkubwa dhidi ya kocha wa daraja la juu kama Fadlu Davids. Hongera kwa Rais Hersi, benchi la ufundi na wachezaji.”
Msimu Mpya: Hatua Mpya ya Ubora
Ingawa kombe limekabidhiwa, mafanikio haya ni mwanzo wa ukurasa mpya. Kama alivyosema Pacome, “Huu ni mwisho wa pambano gumu, lakini ni hatua moja tu... hebu tushukuru na tujiandae kwa yajayo.”
Kwa wapenzi wa Yanga, mashabiki wa kweli, viongozi, wachezaji na familia ya Wananchi kwa ujumla — mna kila sababu ya kujivunia. Huu ni ushindi wa maono, nidhamu, mpangilio na imani ya pamoja.
HITIMISHO: Yanga ni Timu ya Kariba ya Ubingwa
Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Kasheku ‘Musukuma’, alihitimisha kwa sentensi moja yenye uzito:
“Yanga ni timu yenye kariba ya ubingwa toka enzi na enzi.”
Na kwa msimu wa 2024/2025, ukweli huu umeandikwa rasmi katika kitabu cha historia ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
HONGERA YOUNG AFRICANS SC – MABINGWA WA KWELI, USIKU NA MCHANA!
Makala haya yameandikwa na Victor Bariety namba ya simu 0757856284








No comments:
Post a Comment