........................................
Na Mwandishi Wetu, Songwe
Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Mhe. Hamadi Mbega ametoa wito kwa wanufaika wa mikopo ya asiliamia 10 inayotolewa na Halmashauri kuhakikisha wanaitumia kwa malengo yaliyokusudiwa ili kutimiza malengo yao na kubadilisha maisha kiuchumi.
Mhe. Mbega ametoa wito leo Ijumaa Juni 11, 2025 wakati wa hafla ya kukabidhi mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi.
Amesema kuwa mikopo hiyo ni fursa mahsusi ya kuinua maisha ya wananchi kiuchumi na kutoa mchango chanya katika maendeleo ya jamii.
"Kubwa katika yote la kuzingatia ni kwamba mnapaswa kuhakikisha mikopo hii mnaitumia kwa malengo mliyo kusudia. Lengo la Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ni kuona wananchi wake wanajikwamua kiuchumi kupitia shughuli mbalimbali" amesema DC Mbega na kuongeza;
"Sisi kama Serikali tunasisitiza yale mliyoyaainisha kwenye maandiko yenu ya maombi ya mikopo mkayatekeleze kama mlivyopanga. Tumewapa fedha hizi baada ya kuridhika na mlichokiainisha tumepima tumejiridhisha tukaona mlichoandika kinafaa na mtakwenda kujikwamua kiuchumi na si vinginevyo" amesisitiza.
Mhe. Mbega ameeleza kuwa awali katika kutoa asiliamia nne ya vijana ilikomea miaka 30 lakini baada ya kujiridhisha Serikali kupitia maelekezo ya Mhe. Rais ikaongeza umri mpaka miaka 45 kwa vijana hivyo amewasisitiza vijana kutumia fursa hiyo.
Katika hafla hiyo, Halmashauri ya Wilaya ya mbozi imetoa mikopo ya zaidi ya Shilingi Milioni 516 kwa vikundi vya wakinamama, vijana na watu wenye ulemavu ikiwa ni awamu ya pili.Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Mhe. Hamadi Mbega akizungumza wakati wa hafla hiyo.
Shamra shamra zikipamba moto wakati wa hafla hiyo.








No comments:
Post a Comment