UZALENDO ni hali ya mtu kuipenda, kuithamini na kujitoa kwa
ajili ya nchi yake.
Mzalendo wa kweli
daima anaweka maslahi ya nchi mbele na ya kwake nyuma.
Kwa maana hiyo mzalendo ni mtu yeyote mzawa na mwenye
kuipenda na kujitoa mhanga na wakati mwingine ikibidi kufa kwa ajili ya nchi
yake.
Uzalendo unabeba dhana pana ikianzia asili, utamaduni,
lugha, siasa, historia na dhana kuu ikiwa ni utaifa.
Tanzania imekuwa na wazalendo wengi wanaolitumikia taifa
vizuri na waliokwisha kulitumikia akiwemo Rais wetu wa kwanza Hayati Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere, Mzee Rashid Mfaume Kawawa, Edward Moringe Sokoine na
Mwanasiasa maarufu Bibi Titi Mohamed na wengine wengi ambao waliipigania nchi
na baadhi yao kupoteza maisha.
Miongoni mwa watanzania kuna wazalendo wanaotumia elimu na taaluma zao kulitumikia taifa kwa nguvu zao
zote baada ya kuaminiwa na mamlaka za juu kushika nafasi za uongozi.
Leo napenda kumzungumzia Mtaalam wa masuala ya fedha na
uongozi, Nehemia Kyando Mchechu Msajili wa Hazina ambaye ni mzalendo wa kweli
kutokana na kazi kubwa anayolifanyia taifa.
Mchechu kabla ya kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kushika nafasi hiyo amefanya kazi katika
maeneo mbalimbali, Mkuu wa Ukaguzi Chuo Kikuu cha Tumaini, Mkurugenzi wa Kituo
cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Mjumbe wa Kamati za Baraza la Biashara la Taifa.
Maeneo mengine aliyofanya kazi ni Afisa Mtendaji Mkuu na
Mkurugenzi Mtendaji wa CBA Bank, Standard Chartered Bank Tanzania Limited,
Citibank na Barclays Bank Tanzania Limited, Mwenyekiti wa Serengeti Breweries
Ltd, Mwenyekiti wa Amboni Sisal Properties Limited, Mwenyekiti wa Amboni Beach
Limited, Mwasisi na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Rightway Schools,
Mjumbe wa Bodi ya Benki ya KCB Tanzania Limited na Mwenyekiti wa East Africa
Breweries Limited.
Mchechu akiwa Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Commercial Bank of
Africa chini ya uongozi wake benki hiyo ilipata
mafanikio makubwa hapa nchini, na ni moja kati ya benki tano zilizoanza
utaratibu wa kutoa mikopo ya nyumba kwa Watanzania.
Baada ya kufanya kazi katika maeneo hayo kwa mujibu wa
kifungu Na. 18 (1) cha Sheria Na. 2 ya 1990, iliyounda Shirika la Nyumba la
Taifa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi alimteua kuwa Mkurugenzi
Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), uteuzi ulioanza rasmi Machi 1, 2010.
Mchechu alianza kazi kwa kasi kubwa akishirikiana na bodi na
timu ya menejimenti ya shirika hilo huku akiwa amepewa jukumu la kulifanyia
mageuzi makubwa shirika hilo.
Shirika hilo lilitakiwa liingie katika biashara kubwa ya
kujenga nyumba katika mikoa yote na kuziuza kwa mikopo kwa watanzania wa kipato
cha chini na kati, ambalo ndilo lengo kuu la shirika tangu lilipoanzishwa mara
tu baada ya Tanganyika kupata Uhuru Desemba 9, 1961.
Kazi kubwa na nzuri na ya kizalendo ilifanyika chini ya
uongozi wake ambapo karibu kila mkoa zilijengwa nyumba hizo kwa kiwango cha
juu.
Mbali ya kujenga nyumba hizo nyumba za shirika hilo ambazo
zinapangishwa alizifanyia ukarabati na kuzipaka rangi pamoja na kuzihakiki ili
zitambulike kwani baadhi ya nyumba zilifanywa kama mali ya watu binafsi.
Hata hivyo, kitu kizuri hakikosi kuwa na changamoto au mti
wenye matunda ndiyo unaopigwa mawe. Ndivyo. ilivyokuwa kwa Mchechu kwani licha
ya kazi hiyo nzuri na kubwa aliyoifanya Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John
Pombe Magufuli alimuondoa katika nafasi hiyo pengine kwa kupotoshwa na
wasaidizi wake.
Baadaye Rais Samia alipoingia madarakani alimteua tena kuwa
mkurugenzi wa shirika hilo la nyumba ambapo moto wake wa kazi ulikuwa mara dufu,
jambo lililoendelea kuonesha uzalendo
wake kwa taifa.
Kwa kutambua uchapakazi na uzalendo wake kwa nchi, Rais
Samia kwa mara nyingine alimteua kuwa Msajili wa Hazina nafasi ambayo
anaendelea kuitendea haki kwa viwango vya juu.
Moja ya kazi yake kubwa anayoifanya ni utaratibu
aliouanzisha wa taasisi zote zilizo chini ya Serikali kufanya mikutano na
wahariri na waandishi wa habari kuelezea shughuli zinazozifanya ili wananchi
wazijue jambo ambalo lilikuwa halifanyiki hapo awali.
Msajili wa Hazina, Nehemia Kyando Mchechu.
Mchechu hakika ni hazina, mzalendo na tunu ya watanzania
kutokana na utumishi wake uliotukuka na ni miongoni wa vijana waliandaliwa
vizuri kwa ajili ya kulitumikia taifa.
Lengo la kuyaandika
haya yote ni kutaka kufanya mizania ya uongozi katika utendaji wa
utumishi wa umma na Serikali na namna viongozi wanavyotakiwa kuwa.
Ndhairi kuwa taifa likiwa na viongozi wa aina ya Mchechu litapiga
hatua kubwa kiutendaji.
MIifano ipo mingi kama nilivyoitaja hapo juu, hivyo ni
jukumu la Serikali sasa kuwaandaa vijana vyuoni na maeneo mengine ili waweze
kufanya kazi kwa uzalendo na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.
Kumuandika Msechu ni mfano tu wa viongozi wanaopaswa kufanya
mambo katika kulitumikia taifa kwa misingi ya uadilifu na moyo.
Lengo lingine ni kutaka kuonesha jinsi viongozi wanavyopaswa
kuwa baada ya kuandaliwa na kuwa na utendaji bora kama huo.
Licha ya kuwa ni asili na uwezo wa mtu mmoja mmoja lakini
Serikali inaweza kutengeneza viongozi wa namna ya Mchechu hata katika uongozi wa kisiasa.
Nchi za wenzetu zilizoendelea zina utaratibu wa kuwaandaa
viongozi na Serikali yetu ikifanya hivyo tutaweza kuwapata viongozi watakaokuwa
mahiri sehemu zao za kazi.
Utendaji mzuri wa Mchechu kila alipofanya kazi ndio
uliomsukuma Mhe. Rais Samia kumpa nafasi hiyo ili kulisukuma mbele taifa
kimaendeleo na watu wa aina ya Mchechu sio waliibuka tu bali walitengenezwa
kuanzia vyuoni na kuwa na uwezo huo mkubwa.
Mbegu ya watu kama akina Mchechu ambaye alipata nafasi ya
kuwa Mtendaji Mkuu mwenye umri mdogo katika ukanda wa Afrika Mashariki
inatakiwa kuoteshwa ili tuwapate wengi zaidi.
Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanamtafsiri Mchechu kama
hazina ya taifa kwa alichokifanya katika maeneo yote aliyopita, ni mambo
yanayopaswa kuigwa hivyo kuna kila sababu ya kuonekana ni mtu muhimu kwa taifa.
Wahariri na Waandishi wa habari Waandamizi walipohojiwa na
mwandishi wa makala haya walimzungumzia Mchechu kama ifuatavyo;
Jabir Idrisa, Mhariri Mwandamizi wa Gazeti la Mwanahalisi
anasema Ofisi ya Msajili wa Hazina ipo tangu miaka mingi lakini watu wengi na
wanahabari walikuwa hawajui majukumu yake kupitia Mchechu ofisi hiyo sasa inaonekana
kama ni mpya.
“ Zamani tulikuwa hatujui kama Serikali imewekeza hisa kwenye
makampuni binafsi, mambo ambayo hatukuyajua hapo awali,” alisema Idrisa.
Alisema kazi anayoifanya Mchechu ya kuzilea taasisi
hizo na kusema sasa magawio wayatoe
hadharani na kuonesha ni shirika gani bora zaidi ni kitu kikubwa na anatekeleza
hata matakwa ya katiba ya nchi ambayo inataka watu kushirikishwa katika
usimamizi wa mamlaka ya Serikali.
Alisema sasa kumekuwa na uchangamfu wa taasisi hizo za Serikali kutambua mamlaka yake na wajibu wake wa kuchangia mfuko wa Serikali, basi ionekane kwamba kazi anayoifanya Mchechu ni faida kubwa kwa taifa.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipokea mfano wa Hundi kama Gawio na Michango kutoka kwa Mashirika mbalimbali na Taasisi za Umma kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam.
...........................................
“Kutokana na utendaji wake mzuri wa kazi wa uwazi na
kuboresha mifumo ya malipo na miamala ya kifedha kwa njia ya TEHAMA imeleta
uchangamfu huku tukiona kwenye ripoti zake zikieleza kwa mfano, taasisi hii
mwaka jana ilitoa gawio la Sh. Milioni 10 lakini mwaka uliofuata ikitoa gawio
kubwa.
Hii inaonesha jinsi utendaji wake ulivyo chagiza ufanisi wa
kazi kwenye taasisi hizo za umma.
Kwa upande wake Joyce Shebe Mhariri wa Clouds FM alisema
uongozi ni karama, inawezekana muktadha ukachangia na namna ambavyo amepitia
hatua zipi za uongozi au mikono ya nani.
“Tofauti ya Mchechu kila anapopita huwa anaacha alama ya
tofauti, maana yake ni kwamba pengine ni mtu mwenye karama yake na wakati huo
huo ni mtu anayependa kuyaona matokeo na amekuwa mtu wa uwazi sana ‘ transparent’,
hivyo kusaidia kujulikana kwa kazi zake,” alisema Shebe.
Aliongeza kuwa Mchechu alitilia mkazo taasisi zote zilicho
chini yake zifanye kazi zao ili watanzania wajue zinafanya nini, hiyo ni staili
tofauti aliyokuja nayo.
Alisema ni muhimu kuwa na viongozi kama Mchechu ambao
wanakuwa na shauku ya kuona matokeo ya nini kimefanyika na kwa kuzingatia
sehemu ya kazi anapoongoza ni nyeti sana, hivyo taasisi za umma zinahitajika
kuwajibika ipasavyo ili huduma za jamii ziweze kuimarika pia zipeleke gawio.
Alisema Msechu anatakiwa asimame imara na iwapo atakuwa
legelege taasisi hizo zitafanya vibaya na mwisho wa siku zitashindwa kupeleka gawio na jinsi
anavyozisimamia kila taasisi ina jichekecha na kujiuliza tusipo peleka gawio
itakuwaje.
Mwanahabari Hamisi Magendela anasema hatua hiyo ya Mchechu ya kuzitaka taasisi za umma kukutana na wahariri na waandishi wa habari imesaidia wananchi kuzifahamu kazi zinazofanywa na taasisi hizo.
Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH) imeanzishwa kupitia kifungu cha 3 cha Sheria ya Msajili wa Hazina (Mamlaka na Majukumu), Sura 370. Lengo kuu la kuanzishwa kwa OMH ni kusimamia uwekezaji na mali zingine za Serikali katika taasisi na mashirika ya umma, pamoja na kampuni ambazo Serikali ina umiliki wa hisa au kuna maslahi ya umma kwa niaba ya Rais na kwa ajili ya Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania.
Mwaka 2014 kufuatia kufutwa kwa lililokuwa Shirika Hodhi la Mali za Mashirika ya Umma (CHC), OMH ilirithi majukumu yake. Kufuatia mabadiliko hayo, OMH ikaongezewa jukumu la kusimamia ubinafsishaji wa mali za umma, usimamizi na ufuatiliaji wa mashirika ya umma, ukusanyaji wa madeni ya Serikali yaliyorithiwa kutoka CHC, na urekebishaji na ufilisi wa mali zisizozalisha faida katika kampuni au mashirika yaliyobinafsishwa.
MAJUKUMU YA OFISI YA MSAJILI WA HAZINA
Kwa mujibu wa Kifungu cha 10 cha Sheria ya Msajili wa Hazina Sura 370 kama ilivyorekebishwa, Ofisi imepewa majukumu yafuatayo: –
1. Kufanya mapitio ya kudumu ama kuhakikisha kunafanyika mapitio ya kudumu ya shughuli na mwenendo wa watu ama Taasisi ambazo Msajili wa Hazina anamiliki mali ama ana maslahi kwa mujibu wa Sheria.
2. Bila kuathiri Kifungu kidogo cha (1) kwa ujumla wake, Msajili wa Hazina anatakiwa:
• Kutoa
ushauri kwa Serikali kuhusu uanzishaji wa mashirika ya umma na kusimamia
biashara au mali zilizowekezwa kwenye mashirika hayo;
•Kupitia
utendaji wa kifedha wa mashirika kwa lengo la kushauri hatua za kuchukua katika
kuunganisha, kuboresha muundo, kufuta au kuboresha utendaji wa mashirika na
taasisi za umma;
•Kuweka
malengo ya kifedha na vigezo vingine vya utendaji vitakavyotumiwa na mashirika
na taasisi za umma;
•Kufanya
tathmini mara kwa mara ili kupima utendaji wa bodi menejimenti za mashirika na
kutoa mapendekezo kwa Serikali ya hatua za haraka au zilizopo za kuboresha
usimamizi wa rasilimali;
•Kuidhinisha
uwekezaji wa hisa unaofanywa na mashirika ya umma kwenye mashirika au kampuni
nyingine;
•Kuwekeza
au kuuza mali za mashirika ya umma;
•Kuhakikisha
kuwa kila shirika la umma linaingia mkataba wa Utendaji na Msajili wa Hazina
mara moja baada ya kuteuliwa kwa bodi ya wakurugenzi;
•Kufuatilia
na kutathmini programu za mafunzo katika mashirika na taasisi za umma;
•Kuelekeza
au kuidhinisha matumizi au marekebisho ya kanuni za fedha ili kuhakikisha
usahihi wa taarifa za mapato na matumizi ya mashirika ya umma;
•Kuchambua
na kuidhinisha miundo na mifumo ya mishahara, kanuni za utumishi na mpango wa
motisha kwa mashirika na taasisi za umma;
•Kufuatilia
misaada, ruzuku, fedha za mtaji, akiba au malimbikizo ya faida katika mashirika
ya umma na kwenye uwekezaji mwingine wa umma;
•Kupendekeza
au kuidhinisha mipango ya mwaka ya mashirika na taasisi za umma;
•Kufuatilia
na kutathmini utendaji wa mashirika na taasisi za umma; na
•Kufanya
ufuatiliaji na kuhakikisha gawio, michango na mikopo kutoka katika mashirika na
taasisi za umma inalipwa kwa wakati.











No comments:
Post a Comment