Meneja wa Maabara ya Chakula na Dawa, Everlight Matinga, akizungumza na wananchi kwenye banda la mamlaka hiyo katika Maonesho ya Wiki ya Tiba Asili ya Mwafrika yanayoendelea kwenye viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma.
....................................
Na Judith Meingarai, Dodoma
Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) imesisitiza umuhimu wa kufanyiwa uchunguzi wa kimaabara wa dawa asili ili kuhakikisha zinakidhi viwango vya ubora na usalama kabla ya kuanza kusajiliwa na Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala.
Akizungumza jana kwenye banda la mamlaka hiyo katika Maonesho ya Wiki ya Tiba Asili ya Mwafrika yanayoendelea kwenye viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma, Meneja wa Maabara ya Chakula na Dawa, Everlight Matinga, alisema Maabara hiyo imejipanga kuhakikisha kila dawa inayowasilishwa inachunguzwa kwa kutumia mitambo ya kisasa, wataalamu na kwa kufuata viwango vya kitaifa na kimataifa.
"Kila dawa tunayopokea tunaichunguza ili kujiridhisha kama ina viambata dawa, kuangalia uwepo wa vimelea vinavyoweza kusababisha magonjwa, madini tembo, mabaki ya viuatilifu, kemikali hatarishi, sumu kuvu na mengineyo. Lengo ni kuhakikisha ubora na usalama wake kabla haijaingia kwenye matumizi ya kijamii " alisema.
Matinga aliongeza kuwa majibu ya uchunguzi huo ndiyo hutumika kumsaidia mgunduzi au mtengenezaji wa dawa anapokwenda kusajili bidhaa yake kwenye Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala.
"Huwezi kusajili dawa yako kwenye baraza hilo bila kuulizwa kama umeipima kwa Mkemia Mkuu wa Serikali. Ndiyo maana sisi ni wadau muhimu katika maonesho haya," alifafanua.
Kwa sasa, alisema serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imewekeza kwenye mitambo ya kisasa, hatua inayowezesha mamlaka hiyo kufanya uchunguzi wa kimaabara wa kina na wa kisayansi.
Aidha, wazalishaji wa dawa asili wamepunguziwa gharama kwa kulipia nusu ya bei halisi ya huduma hizo ili kuongeza mwamko wa kurasimisha tiba asili.
"Inapotokea dawa iliyopimwa haijakidhi viwango vya ubora na usalama, tunatoa ushauri wa kitaalamu ambao utasaidia kuboresha uchakataji wa dawa hiyo ili iweze kukidhi viwango. Zipo dawa zilizokidhi na zimesajiliwa na Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala na sasa zimesambazwa kwenye baadhi ya maduka ya dawa yanayotambulika. hivyo ni muhimu kila mtengenezaji kufika kwetu kwa uchunguzi wa kimaabara ili kujiridhisha katika swala zima la ubora na usalama," alisema.
Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni: "Tuimarishe Huduma za Tiba Asili zenye Ushahidi wa Kisayansi."
Meneja wa Maabara ya Chakula na Dawa, Everlight Matinga, akisisitiza jambo wakati akizungumza na mwananchi aliyetembelea banda hilo.
0 Comments