MTOTO ATEMBEA KILOMETA 10 KILA SIKU KUOMBA MSAADA WA MATIBABU YA MAMA YAKE ANAYEUMWA FIGO - SINGIDANI BLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Friday, 22 August 2025

MTOTO ATEMBEA KILOMETA 10 KILA SIKU KUOMBA MSAADA WA MATIBABU YA MAMA YAKE ANAYEUMWA FIGO

Jua linapozama mjini Geita, macho ya wengi huelekea majumbani kwao kupumzika. Lakini kwa mtoto mdogo mwenye umri wa miaka 11, Emanuel Omari Shubi, huo ndio mwanzo wa safari ya maumivu na matumaini. Emanuel, mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Uwanja, hulazimika kubeba jukumu lisilo lake: kuzunguka mitaani kila jioni kuomba msaada wa kifedha ili mama yake, Bi Joyce Jeremiah, apate matibabu ya figo.

Kwa wastani, Emanuel hutembea kati ya kilomita nane hadi kumi kila siku, akibeba barua yenye kibali rasmi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Geita (Kumb. Namba AB 192/199/01/...) kinachomruhusu mama yake kuchangisha fedha. Huu ndio uhalisia wa maisha yake: badala ya michezo ya utotoni, anatembea mitaani akiwa na macho yenye huzuni, lakini pia matumaini kwamba kesho huenda mambo yatabadilika.

Maisha Yaliyogeuka Mapema

Safari hii ya mateso haikuanza jana. Emanuel alipozaliwa, baba yake – aliyewahi kuwa mwalimu mkuu wa shule moja ya wilayani humo – alimwacha mama yake akiwa na miezi miwili tu. Tangu wakati huo, maisha ya familia hii yakawa mapambano ya kila siku.

Bi Joyce aliwahi kuendesha mgahawa mdogo kujikimu, lakini ugonjwa wa figo ulimpunguza nguvu, akabaki nyumbani chini ya msaada wa mwanawe mdogo. 

“Badala ya kunisaidia kwa mambo madogo ya nyumbani, huyu mtoto amenibebea mzigo mkubwa kuliko umri na nguvu zake,” anasema Bi Joyce kwa sauti dhaifu. “Badala ya kuniletea makaratasi ya shule, Emanuel huniletea matumaini ya kuishi.”

Emanuel naye anasema:

 “Ningepata nafasi ya kukutana na Rais Samia, Makamu wa Rais au Waziri Mkuu, ningewaomba msaada wa matibabu ya mama yangu. Hata sare za shule sina, daftari sina. Lakini kubwa zaidi – nataka mama yangu apone.”

Kumbukumbu ya Ndoa na Kuachwa

Bi Joyce anasimulia historia yake kwa uchungu mkubwa:

 “Tarehe 17 Desemba 2000 tulifunga ndoa ya kimila. Baada ya kubarikiwa watoto, tarehe 23 Februari 2012 tukafunga ndoa ya serikali. Mwaka 2014 akaniacha kwa fedheha kubwa – alinifukuza kama mbwa na kutupia mizigo yangu nje. Nilimlelea watoto wake watatu wa mwanamke aliyewahi kuachana naye, niliwachukulia kama wanangu, lakini hayo yote hakuyatambua.”

Kwa maneno haya, machozi humtiririka. Haikuwa rahisi kulea watoto wa mwingine, kisha kuachwa katika ugonjwa na uhitaji.

Ushuhuda wa Mama

Bi Joyce anaendelea kwa sauti ya majonzi lakini yenye chembe ya matumaini:

 “Figo ya kushoto inaonyesha nafuu kidogo lakini ya kulia imeharibika sana. Madaktari bingwa waliotumwa na Mama yetu, Rais Samia, walinitibu nikapata nafuu ya muda. Walinielekeza nifuatilie Bugando, lakini sina nauli. Hapo ndipo nikatafuta kibali cha kuchangisha. Niliwahi pia kuhojiwa na wanasheria waliodai wametumwa na Rais Samia, lakini hadi leo sijapata mrejesho wowote.”

Kauli ya Baba

Omari Shubi, mwalimu mstaafu na baba wa Emanuel, anakiri walikuwa pamoja lakini walitengana kisheria. “Kuhusu huyu mtoto, sina uhakika kama ni wangu.

 Kama inahitajika uthibitisho wa kitaalamu, nipo tayari,” alisema kwa simu. Kauli hii imeacha jeraha jipya – kwani hata kama damu haipo, mateso ya Emanuel na mama yake hayawezi kupuuzwa.

Nafasi ya Jamii na Taasisi

Kisa cha Emanuel si cha familia moja tu. Ni sauti ya mamia ya watoto wanaovutwa mapema kwenye mzigo wa maisha. Mashirika ya kijamii, taasisi za dini, Red Cross Tanzania, TAWLA na NGO mbalimbali za afya na elimu zinapaswa kushirikiana ili kuhakikisha mama huyu anapata matibabu, na mtoto hapotezi haki yake ya msingi ya elimu.

Wito wa Msaada

Hii ni hadithi ya mateso, lakini pia ni hadithi ya matumaini. Emanuel anatamani maisha ya kawaida: shule, michezo na ndoto. Mama yake anatamani pumzi ya afya. Tumpe sababu ya kuamini kuwa binadamu bado ni kaka na dada wa kweli.

Msaada unaweza kutumwa kupitia namba ya Bi Joyce Jeremiah: 0686 961 042 (Joyce Manoni).

Kwa msaada wako, si tu utakuwa umeokoa maisha ya mama, bali pia umemrudishia mtoto huyu nafasi ya kuwa mtoto.

Bi Joyce Jeremiah anayeomba msaada wa matibabu ya figo.

Imeandaliwa na:Victor Bariety Simu: 0757 856 284

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad