UTEUZI WA DKT.MIGIRO UMEDHIRISHA KUAMINIWA KWA WANAWAKE NCHINI - SINGIDANI BLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Monday, 25 August 2025

UTEUZI WA DKT.MIGIRO UMEDHIRISHA KUAMINIWA KWA WANAWAKE NCHINI

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Mstaafu Ban Ki Moon akiwa na Dkt. Asha-Rose Migiro.

.............................

 Na Dotto Mwaibale

UTEUZI wa Dkt. Asha-Rose Migiro  kuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), umeonesha kuwa wanawake sasa wamefikia hatua kubwa ya kuaminika katika uongozi.

Kikao cha Halmashuri Kuu ya CCM (Taifa) chini ya Mwenyekiti wake na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kilichoketi Agosti 23, 2025 pamoja na mambo mengine kilimteua Dkt. Migiro (Balozi) kushika nafasi ya katibu mkuu wa chama hicho.

Akiongea katika mahojiano maalum na mwandishi wetu kuelezea maoni yake kufuatia uteuzi wa mwanadiplomasia huyo, Mwenyekiti Mstaafu wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) na Mhariri Mtendaji wa Clouds FM, Joyce Shebe  alisema uteuzi wake ni ishara ya mabadiliko makubwa ya kuaminika kwa wanawake katika nafasi za uongozi.

”Hii ni tofauti na hapo nyuma ambapo ilikuwa ngumu kwa wanawake kupewa nafasi kama hiyo au wanawake kushika nafasi kubwa”, alisema Shebe.

Aliongeza kuwa sasa jamii imeanza kuwaamini wanawake kwamba wanaweza kushika nafasi za uongozi na inatoa picha kujua uwezo wa kitaaluma wa Dkt. Migiro.

“Sasa mtu anaweza kuhamaki kwamba huyu ataweza, Lakini moja kati ya sifa ambazo mimi nazijua Dkt. Migiro anazo ni kwamba yeye ni mwanadiplomasia mzuri na amehudumu kwenye chama kwa muda mrefu. Hii maana yake chama kimemwamini na tunaamini kuwa ataitendea haki nafasi hiyo,” alisema.

Hata hivyo Shebe amesema wengine wataendelea kuwaamini wanawake kwani wanapompa mwanamke nafasi ya juu namna hiyo maana yake ni kwamba wanatengeneza kizazi cha watoto wa kike kwa kufanya uamuzi wa kusomesha watoto hao ambapo mwisho wa siku wote wanakuja kuleta mchango kwenye taifa letu.

Katibu wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma Angelo Madundo anasema uteuzi huo katika kumbukumbu umeweka rekodi kwa kada wa CCM mwanamke kushika nafasi kubwa ya Katibu Mkuu tangu nchi yetu ipate uhuru.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan  alipokuwa Makamu wa Rais akizungumza na aliyekuwa Balozi wa Tanzania Nchini Uingereza Dkt. Asha_Rose Migiro alipotembelea Ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam.

..........................

Alisema uteuzi huo ni hamasa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM Taifa  Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuwahamasisha wanawake kushika nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama na Serikali.

Aliongeza kuwa uteuzi huo siyo kwamba ulenge muktadha wa mwanamke lakini Dkt. Migiro ni mmoja wa wanawake mashuhuri duniani na si tu kwa Tanzania, tukikumbuka kwamba mwaka 2007 na 2012 Katibu Mkuu Mstaafu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon alimteua kuwa msaidizi wake ambapo aliweza kuyahudumia mataifa zaidi ya 194 ambayo ni wanachama wa umoja huo.

“Uteuzi wa Dkt. Migiro siyo wa kubahatisha kikubwa tutakachoweza kukizungumzia ni historia mpya ya mwanamke kushika madaraka ya katibu mkuu wa chama na tuna amini ni mwanadiplomasia mahiri, uzoefu wake katika uongozi na siasa, dunia na Afrika anafaa kukisimamia chama cha CCM ambacho ni kikubwa Afrika,” alisema Madundo.

Kada wa CCM kutoka IItigi mkoani Singida Mhandisi Felix Dagaki naye anasema Dkt. Migiro ni kiongozi mbobezi wa masuala ya kimataifa,  hivyo uteuzi huo ni wa viwango vya hali ya juu na kuwa chama sasa kinakwenda kufanya mapinduzi makubwa ya utendaji.

“Nitumie nafasi hii kuipongeza Halmashuri Kuu ya CCM (Taifa) chini ya Mwenyekiti wake Dkt.Samia kwa uteuzi huo mpana na uliotukuka na wa kipekee”, alisema Dagaki.  

Rose Ngunangwa Mkurugenzi Mtendaji, Shirika la Vyombo vya Habari kwa Maendeleo ya Jamii (TAMCODE) kwa upande wake naye alisema chama hicho kimefanya vema kwa kumuweka mwanamke kwenye nafasi hiyo ya juu kwa sababu kumekuwa na changamoto ya mfumo dume kwenye vyama vingi.

Alisema Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) inakifungu ambacho kinasisitiza umuhimu wa kuwepo na madawati ya kijinsia yenye sera ya kutokomeza ukatili kwa wanawake wakati wa siasa na uchaguzi.

Aliongeza kuwa miaka ya nyuma kulikuwa na malalamiko mengi kuhusu wanawake kushindwa kupata nafasi za uongozi kutokana na safu ya viongozi wa vyama kuwa ni wanaume hivyo kuwa vigumu kwao kuupata.

“ Kwawalicho kifanya CCM ni kitu kizuri mwenyekiti wake ni mwanamke na katibu sasa ni mwanamke hiyo ni fursa nzuri kwao wanawake kupitisha ajenda zao na kuzijadili”, alisema Ngunangwa.

Hata hivyo alisema kuwekwa Katibu mkuu mwanamke kwenye chama kutachagiza utekelezaji wa sera ya jinsia na pia miundombinu yote au mikakati yote na kuhakikisha wanawake waliopo kwenye siasa wanalindwa dhidi ya ukatili wa aina zote.

Ngunangwa aliongeza kuwa wanawake wa chama hicho watakuwa huru zaidi kwenda kwake kumueleza madhira watakayo kuwa wakikumbana nayo kuliko kama angekuwa mwanaume.

Alisema Dkt. Asha-Rose Migiro anauzoefu mkubwa kimataifa na kitaifa na mwenye umri wa busara na ni mtu mzima ameona mengi anaweza kumshauri mtu, kumkosoa na akaeleweka atakapokuwa akiongea kwenye chama.

Aliongeza kuwa Dkt.Migiro anatajwa kuwa ni mwenye elimu ya kutosha  na kuwa ni mmoja wa wanawake waliofanya vizuri sana kwenye masomo ya sheria katika historia ya nchi yetu kwani alipata ufaulu wa kiwango cha juu.

Mwanachama wa CCM kutoka Zanzibar, Hussein Ramadhan Layya (maarufu Msokolo),  ameipongeza Halmashauri Kuu ya CCM chini ya Mwenyekiti wake Dkt. Samia na Makamu Mwenyekiti Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa uongozi wao thabiti wa kuimarisha safu ya chama hicho.

Alisema uteuzi wa viongozi hao unaonesha imani kubwa juu ya uwezo wao na kueleza kuwa Dkt.  Asha-Rose Migiro anauzoefu mkubwa na ni mwanadiplomasia ambaye anakwenda kukifanyia makubwa chama hicho.

Aliongeza kuwa Ali Mwinyi ambaye ameteuliwa kuwa ni Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) ni kielelezo cha dhamira ya chama kuendeleza usawa wa kijinsia na kumsaidia mwanamke kushiriki ipasavyo katika uongozi na maendeleo ya taifa.

Aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Uingereza na sasa ni Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Dkt. Asha-Rose Migiro alipokuwa na wanamichezo wa Tanzania kwenye Michezo ya Jumuiya ya Madola alipowatembelea katika kijiji cha wanamichezo katika Chuo Kikuu cha Birmingham Julai 25, 2025 

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad