Meneja wa TANESCO Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Donasiano J. Shamba.
..........................................
Na Godwin Myovela, Dodoma
Ni kishindo cha mageuzi na matumaini mapya kwa wakazi wa Jiji la Dodoma! Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imeweka historia mpya kupitia maboresho makubwa ya miundombinu ya usambazaji umeme katikati ya jiji na viunga vyake.
Tarehe 20.09.2025 inabaki kwenye kumbukumbu kufuatia kukamilika rasmi kwa upanuzi wa kituo cha mjini kati.
Kwa uwekezaji wa zaidi ya shilingi bilioni 7 ambao umetolewa na Serikali umepelekea wananchi wa Dodoma kushuhudia kituo kipya cha kisasa —kwa kiwango kinachopatikana katika nchi za dunia ya kwanza.
Kituo hicho kimepanuliwa kutoka uwezo wa awali wa MVA 20 hadi MVA 40, kupitia usimikaji wa transfoma mbili zenye uwezo wa MVA 20 kila moja.
Kwa lugha rahisi, hii ni sawa na megawati 36 zinazohakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa maelfu ya wananchi na wajasiriamali wa Dodoma, jiji linalokua kwa kasi.
Akizungumza wakati zoezi la kurekebisha mifumo ya usambazaji umeme likiendelea, Meneja wa TANESCO Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Donasiano J. Shamba, alisema maboresho haya ni mapinduzi ya kweli yanayoendana na kasi ya ukuaji wa jiji.
“Serikali kupitia Mhe. Rais Samia imetupatia fedha za upanuzi wa kituo na kufanya maboresho haya. Sasa jukumu letu ni kuhakikisha uwekezaji huu unawanufaisha wananchi kwa vitendo," alisema Shamba na kusisitiza;
"Dodoma inapaswa kuwa na umeme wa uhakika kwa shughuli zote za kijamii na kiuchumi.”
Alisema kupitia uwezeshaji wa Menejimenti Kuu ya TANESCO, tayari njia mpya ya umeme ya kilometa 7.8 kutoka Zuzu hadi katikati ya jiji, ikitumia nguzo imara za zege na nyaya zenye uwezo mkubwa zaidi imejengwa.
Aidha, ujenzi unaendelea kwa njia nyingine ya kilometa 10.5 kuelekea Swaswa, Ilazo na Mlimwa C — maeneo yanayoshuhudia kasi kubwa ya uwekezaji na ongezeko la ujenzi wa makazi.
Meneja huyo alibainisha kuwa Zuzu pekee inazalisha zaidi ya megawati 200, wakati Dodoma kwa sasa inatumia takribani megawati 85 pekee.
Hivyo, maboresho haya yanahakikisha miundombinu inapokea na kusambaza nishati hiyo kwa ufanisi zaidi, ili kuchochea uwekezaji katika viwanda, biashara na huduma.
Mhandisi Shamba ametoa rai kwa wananchi kulinda miundombinu ya umeme kwa wivu mkubwa, akisisitiza kuwa TANESCO ni shirika la umma na miundombinu yake ni mali ya umma.
“Wapo wanaoiba nyaya au kuhujumu miundombinu ya umeme hasa nyaya za shaba (earthwire) kwa maslahi binafsi. Hii ni hatari kwa usalama na ni hujuma kwa uchumi wetu. Tunapaswa kuilinda kwa nguvu zetu zote,” alisema.
Maboresho haya yanaiweka Dodoma kwenye ramani kama kitovu cha upatikanaji wa huduma ya umeme endelevu na imara, sambamba na kutoa taswira ya mageuzi makubwa katika sekta ndogo ya nishati ya umeme yaliyosimamiwa na Serikali ya Awamu ya Sita.
Pia, Mhandisi Shamba alishukuru Menejimenti ya Shirika chini ya Mkurugenzi Mtendaji Mkuu Lazaro J. Twange kwa uongozi na uwekezaji unaoendelea kuimarisha huduma ya nishati katika mkoa huo, sasa na kwa miaka mingi ijayo.
Kwa uwekezaji huu, wananchi wa Dodoma wanaahidiwa huduma ya umeme wa uhakika — nguzo ya uchumi thabiti, chachu ya uwekezaji na dira ya mustakabali wa taifa.
Dodoma si tu kitovu cha siasa, bali sasa pia ni kitovu cha nishati imara, mfano wa mageuzi makubwa ya nishati yanayojengwa na Serikali.
Mafundi wa Tanesco MMkoa wa Dodoma wakiwa kazini.
Mafundi wa Tanesco wakiwa kazini
Mafunzi wa Shirika hilo wakionesha namna mitambo inavyofanya kazi.
Muonekano wa mitambo ya Shirika hilo.
Muonekano wa Transfoma ya shirika hilo.







No comments:
Post a Comment