JESHI LA POLISI MKOA WA TANGA LAJIDHATITI KUIMARISHA USALAMA KWA WAPIGA KURA - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Friday, 24 October 2025

JESHI LA POLISI MKOA WA TANGA LAJIDHATITI KUIMARISHA USALAMA KWA WAPIGA KURA

RPC Mchunguzi awaonya wanaokusudia kuleta vurugu, asema watakaothubutu kufanya hivyo kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria 


Kamanda wa Polisi Mkoa wa  Tanga Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Almachius Mchunguzi, akizungumza na waandishi wa habari.

.........................................

Mashaka Kibaya, Tanga 

JESHI la Polisi Mkoani Tanga limejipanga kuhakikisha kuwa usalama na amani unaimarika siku ya Oktoba 29 kwa ajili ya wananchi kupiga na limeasa wanaokusudia kuleta vurugu kutothubitu kufanya hivyo kwa vile watakaokwenda kinyume watashughulikiwa kikamilifu kwa mujibu wa Sheria.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga Kamishna Msaizi wa Polisi (ACP) Almachius Mchunguzi ametoa taarifa hiyo jana zikiwa zimesalia siku tano (5) kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa  Rais, wabunge pamoja na madiwani.

Katika taarifa yake hiyo, Mchunguzi amewatoa hofu Wananchi kwamba jeshi la polisi limejipanga kuhakikisha hakutajitokeza hali yeyote itakayomsababisha mtu kushindwa kutimiza haki yake ya kidemokrasia huku akiwataka Wananchi kujitokeza kwa wingi kwenda kupiga kura.

"Wale wanaokusudia kujaribu kufanya vitendo ambavyo ni kinyume cha sheria wasijaribu, watakaothubutu watashughulikiwa kikamilifu kwa mujibu wa sheria" alisema..

Aidha Kamanda Mchunguzi alisema, jeshi la Polisi limejidhatiti kuhakikisha siku ya kupiga kura ya Oktoba 29 hali inakuwa shwari kwa Usalama na amani kutawala ambapo watu wakitoka na kurejea nyumbani wakiwa kwenye hali ya usalama. 

"Watu wasione hofu yeyote kwenda kupiga kura,waende kwa kujiamini kwamba jeshi lao la polisi liko vizuri kuhakikisha Usalama wao toka wanapotoka nyumbani hadi wanaporudi" alisema.

Kamanda huyo wa Jeshi la Polisi Mkoani Tanga alisema Wananchi hawapaswi kuwa na hofu juu ya habari wanazoziona kupitia mitandao kwamba kutakuwa na uvunjifu wa amani alisema hayo hayana ukweli ambapo jeshi la Polisi limejidhatiti kuimarisha amani.

ACP Mchunguzi aliongeza kusema kwamba, katika wilaya zote za mkoa wa Tanga ulinzi na usalama umeendelea kuimarika huku kampeni zikifanyika kama kawaida na  wagonbea wa uongozi wakiendelea kunadi Sera zao.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad