Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mohamoud Thabit Kombo ameongoza ujumbe Tanzania kushiriki Mkutano wa Kati wa19 wa Mawaziri wa Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM) unakaofanyika Kampala, Uganda tarehe 15–16 Oktoba 2025. Mkutano huo, ulitanguliwa na Mkutano cha Ngazi ya Wataalam tarehe 13–14 Oktoba 2025.
Mkutano huu unajadili namna ya kutatua changamoto za kisiasa, kiuchumi na kijamii zinazokabili nchi wanachama wa NAM kwa nyakati za sasa. Mhe. Chumi wakati wa akitoa hotuba amezitaka nchi wanachama wa NAM kuendelea kushikamana kwa pamoja kwenye majadiliano mbalimbali ya kimataifa na kutetea maslahi ya nchi zinazoendelea. Amesema Tanzania ipo tayari na itashirikiana na nchi nyingine ili kkutetea na kulinda maslahi ya zetu. Baada ya majadiliano, Mkutano huo utapitisha Azimio ikiwemo Azimio la Mwisho la Kampala na Tamko kuhusu Palestina.
NAM ni umoja wa Nchi na Serikali 120 zenye msimamo wa sera ya kutofungamana na upande wowote. Umoja huo ulianzishwa wakati wa enzi za vita baridi kwa lengo la kusaidia nchi wanachama wake kutoka mabara ya Asia, Afrika na Latin Amerika kuondokana na ukoloni ili kuweza kujitawala kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Mkutano huo umefunguliwa na Mhe. Yoweri Kaguta Museveni, Rais wa Jamhuri ya Uganda.
0 Comments