NSSF YAJIVUNIA MATUMIZI YA TEHAMA - SINGIDANI BLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Monday, 6 October 2025

NSSF YAJIVUNIA MATUMIZI YA TEHAMA

Meneja wa NSSF Mkoa wa Singida, Oscar Kalimilwa, akizungumza wakati wa ufunguzi wa Maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja yaliyoanza leo Oktoba 6, 2025.

.................................

Na Mwandishi Wetu

WAKATI Maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja yakiadhimishwa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) linajivunia hatua ya matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), ambayo imerahisisha utoaji wa huduma kulingana na kasi ya ukuaji wa teknolojia duniani.

Hayo yamebainishwa na mgeni rasmi wa ufunguzi wa maadhimisho hayo Mrakibu Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Singida (ASP) Mwantumu Bakari wakati akifungua maadhimisho hayo kwa niaba ya Kamanda wa jeshi hilo Mkoa wa Singida.

Mwantumu alisema kwa sasa mfuko huo umewezesha wanachama kufungua madai ya mafao mbalimbali kwa njia ya mtandao (Online claim lodging) na kutoa fursa kwa wanachama walioko mbali na matawi ya shirika hilo kuweza kufungua madai mahali popote walipo na hatimaye kulipwa kwa mujibu wa sheria na kanuni za ulipaji wa mafao.

Alisema Wiki ya huduma kwa wateja ilianzishwa rasmi kimataifa mwaka 1987 na kupata utambuzi rasmi mwaka 1992 nchini Marekani na kupewa hadhi kama sherehe ya kimataifa kwa lengo la kutambua umuhimu wa huduma bora kwa wateja na juhudi za wafanyakazi wanaotoa huduma bora kwa wateja.

“Kwa mwaka huu (2025) maadhimisho yanaanza leo Oktoba 6, 2025 na kilele chake ni Oktoba 10, 2025, “ alisema Mwantumu.

Alisema kwa kutambua umuhimu wa wanachama, waajiri, wadau na wateja , mfuko huo umeandaa hafla hiyo fupi ili kuwashukuru wateja kwa ushirikiano wanaotoa katika nyanja mbalimbali kama vile kujiandikisha, kulipa michango, kununua au kutumia bidhaa na huduma zitolewazo na  mfuko kama vile nyumba, viwanja, daraja la mwalimu Nyerere au kupanga katika majengo mbalimbali yanayomilikiwa na mfuko nchi nzima na hivyo kuufanya kukua na kuendelea kumudu kulipa mafao ya wanachama wa NSSF wakiwemo wastaafu.

Mwantumu aliongeza kuwa kwa kuona umuhimu huo mfuko umeamua kuadhimisha kwa pamoja na wateja wake kama shukrani kwa ushirikiano wao na kuwapa hamasa ya kuendelea kuchagua kuhudumiwa na Mfuko wa NSSF.

“ Kama ilivyo kauli mbiu ya mwaka huu, Kidijitali Tumeweza’’ Mfuko unajivunia hatua kubwa uliyofikia katika matumizi ya Tehama ambayo yamerahisisha sana utoaji wa huduma,” alisema Mwantumu.

Alisema vilevile wastaafu wa mfuko wamewezeshwa kuhakiki taarifa zao kwa njia ya mtandao (online verification) na hivyo kuwapunguzia adha wazee ya kufika katika ofisi zao kwa ajili ya zoezi la kujihakiki.

Aliongeza kuwa waajiri hawajaachwa nyuma kwani Mfuko umewawezesha kulipa michango yao moja kwa moja kwa kutumia lango la waajiri (Employers portal) ambapo wanaweza kujihudumia kwa kuwasilisha michango na kupata risiti za uchangiaji na pia kuona maendeleo ya michango ya wafanyakazi wao bila kufika katika matawi.

Alisema kwa kupitia mfumo huo mwajiri pia anaweza kuona malimbikizo yake ya michango na kuweza kupata namba ya malipo (Control number) pasipo kulazimika kufika katika tawi la NSSF hivyo kuokoa muda wa uzalishaji.

“ Nitoe rai kwa waajiri wote kuhakikisha wanajiandikisha na kuanza kuchangia wafanyakazi wao kwa mujibu wa Sheria kwani Mfuko umejidhatiti kuwafikia waajiri wote ambao hawajajiandikisha na kuwachukulia hatua stahiki wale wote wanaolimbikiza michango ya wanachama,” alisema.

Aidha, Mwantumu alisema mfuko pia umewezesha wanachama wake kujihudumia wenyewe kutumia Mfumo wake wa lango la wanachama (Member portal) ambapo wanachama wanaweza kuangalia michango yao pasipo kufika katika matawi.

Alisema mfuko unatoa fursa kwa wanachama wake kuweza kupitia taarifa zao za uandikishwaji na kuomba marekebisho pale wanapoona haziendani na taarifa zao zilizoko katika Mfumo wa vitambulisho vya Taifa (NIDA). Kupitia lango husika wanachama pia wanaweza kuwasilisha malalamiko kwenye Mfuko.

Mwantumu alisema mfuko umeendelea kupata mafanikio hayo kutokana na jitihada za Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Mfuko unatumia hafla hii kumpongeza na kumshukuru kwa juhudi kubwa zilizofanywa na zinazoendelea kufanywa na Serikali ya awamu ya sita kwa namna inavyoendelea kutoa  kipaumbele katika kuboresha huduma za jamii na kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji wa ndani yaliyowezesha Mfuko kukua na hatimaye kumudu kupandisha kima cha chini cha Pensheni ya wastaafu kutoka kiasi cha Sh.100,000 mpaka kufikia Sh. 150,000," alisema Mwantumu.

Akizungumzia kwa upande wa watumishi, alisema Serikali ya awamu ya sita imeboresha mifumo ya watumishi kujipima kwa malengo kwa kuandaa mfumo wa (PEPMIS) ambao umewezesha watumishi kujiwekea malengo na hatimaye kujipima kwa kutumia malengo ambayo wamejiwekea.

Mwantumu alisema mfumo huo umesaidia sana katika kuongeza ufanisi na utendaji kazi wa watumishi wa Mfuko na watumishi wa Serikali kwa ujumla ambapo alitoa rai kwa watumishi wote wa Mfuko kuhakikisha wanatumia Mfumo huo kujaza utekelezaji wa malengo yao kwa muda waliopangiwa.

Aidha, Mwantumu alitumia fursa hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu na Bodi ya wadhamini kuwashukuru na kuwapongeza watumishi wote kwa juhudi kubwa za pamoja wanazozifanya katika kuwahudumia wanachama wa NSSF na kuwa mfuko unatambua mchango wao katika kutekeleza majukumu waliyonayo.

Mwantumu alikumbusha kuwa maadhimisho ya mwaka huu yamejikita katika kusheherekea mafanikio yaliyofikiwa na Mfuko lakini wasisahau kutambua kwa upekee umuhimu wa wanachama wa NSSF katika mafanikio yote ambayo Mfuko umeyafikia kwani bila wao Mfuko usingeliweza kuyafikia.

Aliwataka watumishi wa Mfuko huo kuvaa viatu vya wateja na kuzingatia kauli zenye staha, utu na ubinadamu wanapokuwa wanatoa Huduma za Mfuko lakini pia wazingatie miongozo ya utendaji ili kutoa haki na usawa.

Meneja wa NSSF Mkoa wa Singida, Oscar Kalimilwa akizungumza wakati akimkaribisha mgeni rasmi alisema wamekuwa wakishiriki kuadhimisha wiki hiyo na wateja wao kama njia mojawapo ya kuwatambua na kuwaenzi kwani wao ndiyo  nguzo yao muhimu.

“Tunafanya hivyo ili nao waweze kutambua kwamba ni watu wa dhamani kwetu na ndiyo wanao tufanya tuendelee kuwepo,” alisema Kalimilwa.

Kwa upande wake Afisa Matekelezo Mwandamizi wa NSSF Mkoa wa Singida, Marini Kimario alitaja majukumu manne ya shirika hilo kuwa ni kuandikisha wanachama, kukusanya michango kutoka kwa wanachama na waajiri, uwekezaji kwa lengo la kuongeza mtaji kutokana na michango ya wanachama ili wanapostaafu waweze kulipwa kwa wakati na jukumu la mwisho ni ulipaji wa mafao ya wanachama wao.

Katika maadhimisho hayo Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Singida lilitoa elimu ya namna ya kujikinga na majanga ya moto, elimu iliyotolewa na ASP Mwantumu Bakari kwa kushirikiana na Konstebo John Mduma.

Mrakibu Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Singida (ASP) Mwantumu Bakari akizungumza wakati akifungua maadhimisho hayo kwa niaba ya Kamanda wa jeshi hilo Mkoa wa Singida.

Afisa Matekelezo Mwandamizi wa NSSF Mkoa wa Singida, Marini Kimario, akizungumza kwenye maadhimisho hayo kuhusu majukumu manne ya NSSF.
Wateja wa NSSF na wageni waalikwa wakiwa kwenye maadhimisho hayo.
Wafanyakazi wa NSSF wakiwa kwenye maadhimisho hayo ya wiki ya huduma kwa mteja. Kutoka kushoto ni  Mfaume Mfaume, Asha Iddi, Hafsa Ally na Latifa Singano.
Maadhimisho yakiendelea. Mwenye fulana nyeupe ni Afisa Matekelezo Mwandamizi kutoka PSSSF Mkoa wa Singida, Valency Masebu.
Meneja wa NSSF Mkoa wa Singida, Oscar Kalimilwa na ASP Mwantumu Bakari wakiwa kwenye maadhimisho hayo.
Wateja wa NSSF na wageni waalikwa wakiwa kwenye madhimisho hayo.
Muonekano wa keki maalum wakati wa maadhimisho hayo.
Meneja wa NSSF Mkoa wa Singida, Oscar Kalimilwa (kushoto),Mrakibu Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Singida (ASP) Mwantumu Bakari (katikati) ambaye alikuwa mgeni rasmi na Mteja wa shirika hilo kutoka Iguguno mkoani hapa Mzee Ansay Shila wakikata keki maalum ya maadhimisho hayo.

Mrakibu Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Singida (ASP) Mwantumu Bakari akimlisha keki Konstebo John Mduma.
Mfanyakazi wa NSSF Mkoa wa Singida, Mfaume Mfaume. akilishwa keki.
Mfanyakazi wa NSSF Mkoa wa Singida, Hafsa Ally akilishwa keki.
Afisa Mambo ya Ndani wa NSSF Makao Makuu, Leopold Kambona akilishwa keki.
Afisa Huduma kwa Wateja NSSF Mkoa wa Singida, Latifa Singano, akilishwa keki.
Picha ya pamoja wakati wa maadhimisho hayo.
 

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad