MSHINDI WA NISHANI YA VITA YA KAGERA, ACHAGULIWA KULIONGOZA BUNGE LA 13 - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Wednesday, November 12, 2025

MSHINDI WA NISHANI YA VITA YA KAGERA, ACHAGULIWA KULIONGOZA BUNGE LA 13

Ni Mbunge wa Ilala Mussa Azzan Zungu

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Azzan Zungu.
..............................................

Na Dotto Mwaibale, Dodoma

​BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kikao chake cha kwanza cha bunge la 13 kimemchagua rasmi Mbunge wa Jimbo la Ilala Jijini Dar es Salaam, Mhe. Mussa Azzan Zungu kuwa Spika wa Bunge la 13 la Tanzania akichukua nafasi ya mtangulizi wake Dkt.Tulia Ackson .

Mhe. Zungu anakuwa Spika wa Nane wa bunge hilo baada ya kupigiwa kura na wabunge katika uchaguzi uliofanyika Novemba 11, 2025.

Katika uchaguzi huo Mhe. Zungu amepata kura 378 kati ya kura 383 hivyo kupata ridhaa ya kuongoza chombo hicho muhimu kwa kipindi cha miaka mitano 2025 hadi 2030.

Makada wa Chama Cha Mapinduzi waliowahi kushika nafasi hiyo ya Uspika tangu Tanzania ipate Uhuru wake ni Adamu Sapi Mkwawa aliyechaguliwa Novemba 27, 1962, Erasto Andrew Mbwana Mang'enya Novemba 20, 1973, Pius Msekwa Aprili 28, 1994, Samuel Sitta Desemba 28, 2005, Anna Makinda Novemba 10, 2010, Job Ndugai Novemba 17, 2015 na Dkt. Tulia Ackson Februari 4, 2022.

Mhe Zungu ambaye katika Bunge la 12 lililopita alikuwa Naibu Spika kuchaguliwa kwake kuwa Spika ni wazi kuwa amepanda ngazi kwa kushika nafasi hiyo ambayo awali ilikuwa ikishikiliwa na Dk.Tulia  ambaye alijitoa katika kinyang’anyiro hicho.

 Zungu ameibuka kidedea baada ya kuwashinda wagombea wa vyama vingine vitano waliojitosa katika kinyang’anyiro hicho.

Wagombea hao ni Veronica Charles kutoka Chama cha NRA, Anitha Mgaya wa NLD, Chhrisant Ndege wa Chama cha DP, Ndonge Said Ndonge kutoka Chama cha AAFP na Amin Yongo kutoka Chama cha ADC

Kabla ya zoezi la kupiga kura kufanyika, wagombea wa nafasi ya Spika wa Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania waliomba kura mbele ya wabunge wateule kila mmoja akieleza nia yake ya kuliongoza Bunge lenye uwajibikaji, ushirikiano na kuwatumikia wananchi.

Mgombea wa kwanza kujinadi kwa wabunge ni Veronica Charles kutoka Chama cha NRA, ambaye alisema akichaguliwa kuwa Spika atalifanya Bunge  liwe la usawa na la wananchi.

Veronica alisema ataondoa kambi rasmi ya upinzani na kuanzisha kambi ya majadiliano kwa lengo la kuimarisha umoja na ushirikiano bungeni.

Aidha, alimpongeza Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kuwa mfano wa kuigwa, akisema ni kiongozi aliyempa ujasiri wa kuwania nafasi hiyo.

Naye Anitha Mgaya kutoka Chama cha NLD amesema dhamira yake ni kuhakikisha nidhamu, heshima na utulivu vinatawala mijadala yote bungeni.

Mgaya alisema kama kijana ataweka mkazo kwa  kuwaelimisha vijana juu ya thamani ya amani, upendo na utulivu.

Kwa upande wake, Chrisant Ndege wa Chama cha DP amesema ana nia ya kusimamia Bunge litakalokuwa na uwezo wa kuishauri na kuisimamia Serikali kwa mujibu wa Katiba.

 Amesema  kuwa mihimili mitatu ya dola ambayo ni Serikali, Bunge na Mahakama  inapaswa kufanya kazi kwa ushirikiano, huku kila mhimili ukitekeleza majukumu yake kwa uadilifu.

Ndege amesema atahakikisha sheria zinazotungwa zinakuwa na tija kwa maendeleo ya wananchi .

Ndonge Said Ndonge kutoka Chama cha AAFP ameanza kwa kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa ushindi alioupata.

 Aidha, Ndonge alitumia falsafa ya neno KIONGOZI kueleza misingi yake ya uongozi akisema K ni kukubali kukosolewa, I kujua tabia za unaowaongoza, O kuonyesha kwa vitendo, N kunena kauli thabiti, G kugawa madaraka, O kuondoa uonevu, Z kuzuia migogoro na I kuinua kipato.

Kwa upande wake Amin Yongo, kutoka Chama cha ADC amesema endapo atachaguliwa kuwa Spika, atahakikisha Bunge linasimamia amani, umoja wa kitaifa na katiba ya nchi.

Kwa upande wake, Mhe. Musa Azan Zungu kutoka CCM alisema akipata nafasi ya Uspika, ataunganisha Bunge kwa maslahi ya wananchi na kuhakikisha linafanya kazi kwa ufanisi ili kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.

Zungu alisema ataendelea kuimarisha uhusiano kati ya Bunge na wananchi ili kuhakikisha hoja zinazojadiliwa bungeni zinagusa moja kwa moja maisha ya Watanzania.

WASIFU WA SPIKA MPYA WA BUNGE LA TANZANIA MHE. MUSSA AZZAN ZUNGU.

Mussa Azzan Zungu ni mwanasiasa mkongwe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye amehudumu bungeni kwa muda wa miaka 20 mfululizo, huku akijipatia heshima kubwa kutokana na uzoefu wake wa muda mrefu katika shughuli za Kibunge na utumishi wa umma.

Mussa Azzan Zungu ni Mhandisi wa ndege aliyepata mafunzo nchini Tanzania na Canada, akionyesha umahiri katika taaluma ya kiufundi kabla ya kuingia kwenye siasa.

Kwenye uzoefu wa kibunge amekuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tangu miaka ya 2000.

Amekuwa mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Bunge kati ya mwaka 2016 na 2025, amekuwa

Mwenyekiti wa Bunge kati ya mwaka  2012 na 2021, na pia amekuwa Naibu Spika kati ya mwaka 2022 na 2025 kabla ya kuchaguliwa kuwa Spika wa Bunge la 13.

Akiwa bungeni amewahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kwa zaidi ya miaka 16.

Mussa Azzan Zungu amewahi kufanya kazi na Maspika wanne tofauti, jambo linalompa uzoefu mkubwa wa kiutawala na Kibunge.

Kwenye uongozi wa Kimataifa, amewahi kuwa kiongozi wa Bunge la Tanzania katika mikutano ya Umoja wa Mabunge ya Nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki (ACP) pamoja na Bunge la Umoja wa Ulaya (EU).

Pia amewahi kuwa kiongozi wa Chama cha Mabunge ya Jumuiya ya Madola (CPA – Tanzania Branch) na mwakilishi wake katika vikao vya kimataifa.

Ameshiriki ziara za mafunzo ya Kibunge katika zaidi ya nchi 23, akijenga uelewa mpana wa mifumo ya Mabunge duniani.

Kwenye Serikali amewahi kuhudumu kama Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), nafasi iliyompatia uzoefu katika masuala ya utawala wa Serikali na ushirikiano wa Muungano.

Kwa heshima na sifa binafsi Mhe. Zungu ni mweledi wa kanuni na taratibu za uendeshaji wa Bunge, mtumishi wa umma mwenye uadilifu, aliyejitolea kulitumikia Taifa kwa uwazi na uaminifu, na ni mshindi wa Nishani ya Vita ya Kagera, kama ishara ya uzalendo na mchango wake kwa Taifa.

Makala hii imeandaliwa kutoka vyanzo mbalimbali lengo likiwa ni kuhabarisha umma kuhusu kumjua vizuri Spika Mpya wa Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Mussa Azzan Zungu.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad