Kaimu Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Kampasi ya Singida Dkt. David Msokwe akizungumza na Wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Taasisi hiyo wakati akifungua mafunzo ya kuwaelekeza taratibu mbalimbali za taasisi hiyo Novemba 19, 2025.
................................................
Na Dotto
Mwaibale, Singida
WANAFUNZI msimu wa masomo 2025/ 2026 katika Taasisi ya
Uhasibu Tanzania (TIA), Kampasi ya Singida wametakiwa kufuata sheria na taratibu
mbalimbali zilizowekwa na kujikita kwenye masomo na si vinginevyo.
Hayo yameelezwa na Kaimu Mkuu wa Taasisi hiyo Dkt. David
Msokwe wakati akizungumza na wanafunzi wa mwaka wa kwanza (Orientation for first year student) na wazamani kwa ajili ya kuwaelekeza na kuwakumbusha taratibu na kanuni za taasisi hiyo katika nyanja
mbalimbali.
Alisema Serikali kupitia taasisi hiyo jukumu lake kubwa ni
kuwapa elimu hivyo ni wajibu wao kuzingatia masomo wakati wote na kufuata
taratibu zilizowekwa.
“Taasisi yetu ipo kwa ajili ya kuwaandaa hivyo wakati wote mkiwa chuoni hapa muwe huru kueleza changamoto zenu kwa walimu na walezi wenu ili muweze kupata msaada,” alisema Msokwe.
Afisa Utumishi na
Msimamizi wa Huduma za Rasilimali Watu na Utawala wa Taasisi hiyo, Sanura Mohamed
akizungumza katika tukio hilo alisema limelenga kuwapa uelewa kuhusu masuala ya udahili,
mitihani, ulipaji wa ada, huduma za maktaba, kujisajili kupitia mfumo wa
wanafunzi na kujua mazingira mbalimbali ya chuo hicho.
Alisema mambo mengine waliyoelekezwa ni pamoja na kujua
huduma zingine ambazo wanaweza kuzipata nje ya masomo.
Alitaja mambo mengine kuwa ni kuvaa mavazi yenye staha kwani
wanawaandaa kuwa watumishi wa baadae hivyo wanapaswa kuvaa mavazi yenye
heshima, kuwa na nidhamu kwa jamii inayowazunguka na walimu.
Aidha, Sanura alitumia nafasi hiyo kuwahasa wanafunzi wa
chuo hicho kutojihusisha na maandamano yanayodaiwa yatafanyika Desmba 9, 2025
yanayohamasishwa kupitia mitandao ya kijamii.
Mhandisi wa Taasisi hiyo, Godfrey Seni akizungumza na
wanafunzi hao aliwata kutunza miundombinu mbalimbali ya chuo hicho kama vile
samani, viyoyozi, miundombinu ya maji safi na usafi wa mazingira na kutojifanya
mafundi wa kitu chochote ambacho kitakuwa kimeharibika kwani wapo mafundi kwa
ajili ya kazi hiyo.
Mambo mengine waliyoelekezwa wanafunzi hao ni masuala ya
Afya ya Uzazi yaliyotolewa na Mtaalamu wa Huduma Rafiki kwa Vijana katika Vituo
vya Afya Manispaa ya Singida Dkt. Fatuma
Ndoile, Elimu kuhusu masuala ya mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa vyuoni
iliyotolewa na Benjamin Masyaga Afisa wa
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Singida.
Eneo lingine waliloelekezwa ni masuala ya Sheria
yaliyotolewa na Mwanasheria wa chuo hicho Wakili Joseph Wawa, masuala ya
maktaba yaliyotolewa na Mkutubi wa taasisi hiyo, Joseph Mwalubanda, masuala ya
ununuzi na ugavi yaliyotolewa na Mratibu wa masuala hayo wa chuo hicho, Faraji
Saidi na masuala ya Dawati la Jinsia yaliyotolewa na Innocent Msumanji kutoka
taasisi hiyo.








No comments:
Post a Comment