SERIKALI YAKARIBIA KUZINDUA MPANGO WA BIMA YA AFYA KWA WOTE - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Thursday, December 18, 2025

SERIKALI YAKARIBIA KUZINDUA MPANGO WA BIMA YA AFYA KWA WOTE

● ITAANZA KWA MAKUNDI YA WATOTO, AKINA MAMA WAJAWAZITO, NA WAZEE.

Waziri Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ipo katika hatua za mwisho za maandalizi ya uzinduzi wa Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote. Mpango huu unalenga kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma za afya kwa uhakika bila vikwazo vya kifedha.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uyole, mkoani Mbeya, Dkt. Mwigulu alibainisha kuwa utekelezaji wa awali wa mpango huo utaanza kwa makundi ya watoto, akina mama wajawazito, na wazee. Uzinduzi rasmi unatarajiwa kufanyika Januari 2026.

Waziri Mkuu alieleza kuwa sambamba na maandalizi ya mpango huo, Serikali imeendelea kuimarisha sekta ya afya kwa kuboresha miundombinu na kuongeza rasilimali watu. Hadi sasa, hospitali 119 zimejengwa katika wilaya na halmashauri ambazo awali hazikuwa na hospitali za wilaya. Vituo vya afya 649 vimejengwa katika tarafa na kata za kimkakati, huku zahanati 2,800 zikijengwa katika vijiji vilivyokuwa na uhitaji. Aidha, ajira za watumishi wa afya 5,000 zipo katika hatua za mwisho na wanatarajiwa kuanza kazi Januari 2026.

Dkt. Mwigulu pia alibainisha mafanikio katika sekta ya elimu. Serikali imefanikisha ujenzi wa madarasa 79,000, shule mpya za sekondari zaidi ya 1,300 na shule mpya za msingi zaidi ya 2,700. Aidha, mchakato wa ajira za walimu 7,000, wakiwemo walimu wa sayansi na hesabu, unaendelea na walitarajiwa kuanza kazi Januari 2026.

Pia Waziri Mkuu ameelekeza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kufanya tathmini ya miradi yote iliyolipwa fedha ili kuhakikisha thamani ya fedha inalingana na kazi iliyotekelezwa. Amesisitiza kuwa wakandarasi wa miradi ya Serikali hawaruhusiwi kupeleka malipo katika akaunti za nje ya nchi, bali wanapaswa kutumia akaunti za ndani.

Aidha, amewataka viongozi wa Serikali katika ngazi zote kutatua kero za wananchi kwa uwajibikaji na kwa wakati, bila urasimu usio wa lazima.

Dkt. Mwigulu pia ameeleza kuwa ndani ya siku 100, Serikali imefanikisha ulipaji wa madeni yote ya wakulima wa Kiwira na ulipaji wa fidia kwa wananchi waliopisha ujenzi wa barabara ya njia nne (bypass) katika Jiji la Mbeya. Ujenzi wa barabara ya Igawa – Mbeya – Tunduma umeshaanza, hatua ambayo itapunguza msongamano wa magari na kuchochea shughuli za kiuchumi.

Aidha, Dkt. Mwigulu amehimiza wananchi kuendelea kudumisha amani na mshikamano, akisisitiza kuwa amani ni msingi muhimu wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Viongozi wa Serikali wametakiwa kusimamia miradi kwa uwazi, uwajibikaji na kuhakikisha thamani ya fedha inaleta manufaa kwa wananchi.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad