Wageni wakionesha umahiri wa kuruka eneo la Fungu la Mchanga Mafui walipokuwa kwenye ziara ya kutembelea vivutio vya utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Saadani.
.......................................
Na Mashaka Kibaya,Hifadhi ya Taifa ya Saadani,Tanga.
FUNGU la mchanga Mafui lililopo katikati ya bahari ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Saadani, ni eneo linaloweza kutumiwa na wageni wa ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kuvalishana pete, birthday na hata kufunga ndoa 'pingu za maisha'.
Ama kwa hakika kwa Wageni wa ndani na nje ya nchi waliopata fursa kushiriki Shangwe la Sikukuu na Tanapa kwenye Hifadhi ya Taifa ya Saadani kwa mwaka huu wanayo mengi mazuri ya kukumbuka na yasiyosahaulika.
Shangwe la Sikukuu na Tanapa ni matamasha ambayo huandaliwa na Kitengo cha utalii Tanapa, lengo likiwa kuhamasisha watu kufanya utalii kwenye hifadhi mbalimbali zilizopo hapa nchini Tanzania.
Leo hii hapa nazungumzia hifadhi ya Taifa ya Saadani inayopatikana katika mikoa miwili yaani Tanga na Pwani nchini Tanzania, hifadhi ambayo mwaka huu imeadhimisha Shangwe la Sikukuu na Tanapa kwa mtindo uliyo wa kipekee kabisa.
Pengine labda ni kutokana na hifadhi hii jiografia yake kuwa ya kipekee, kwani inapakana na bahari ya Hindi huku eneo jingine maji ya mto Wami yakikutana na yale ya bahari ya Hindi, ama kwa hakika hifadhi ya Saadani ni ya kipekee.
Sasa nijikita katika kuzungumzia Shangwe la Sikukuu na Tanapa Season 2, shughuli ambayo imefanyika mwaka huu wa 2025, ilipambwa na wageni wengi kutoka ndani na hata wale wa nje ya nchi.
Daud Gordon ni Afisa Mwandamizi Kitengo cha utalii Hifadhi ya Taifa ya Saadani,na katika mazungumzo yetu anasema,Saadani ina vivutio vingi ila anaamini sasa wageni walio wengi watakuwa wakivutiwa zaidi kutembelea kivutio cha fungu la mchanga Mafui.
Kwa nini Mafui? Gordon anasema, fungu hili linapatikana katikati ya bahari ya Hindi ambayo ni sehemu ya Hifadhi ya Taifa ya Saadani.Hapa watalii hufika kwa usafiri wa boti zilizo za kisasa.
Anasema kuwa, wageni wanaofika hapa watafurahia mandhari nzuri ya fungu la mchanga linaloonekana na kudumu kwa muda maalum, fungu hili linaweza kutumika kwa watu kufunga harusi, kuogelea,kujionea viumbe mbalimbali wa majini wakiwemo Kasa wa kijani na star fish.
"Hapa Mafui ni kivutio bora kabisa, kuna nafasi ya kutosha kuogelea ,watu wakitaka kuvishana pete,kufunga harusi, picnic na mambo mengine kama birthday wageni wanakaribishwa kutembelea" anasema Gordon.
Katika kuthibitisha uzuri wa kivutio hiki, Salma Omar akiwa miongoni mwa watu wa kwanza kukitembelea katika wakati huu wa Shangwe la Sikukuu na Tanapa,akiwa na familia yake alielezea kuridhishwa kwake na mambo mazuri aliyopata kuyaona.
"Hii ni mara yangu ya kwanza kufika fungu la mchanga Mafui, is a good place for wedding, snooker na hata picnic,kiukweli tume enjoy" hapa anasema Salma Omar.
Maajabu mengine yaliyopo ndani ya hifadhi ya Taifa ya Saadani ni pamoja na eneo la 'Porokanya', eneo hili linapatikana kwenye mto Wami ambapo maji ya mto hukutana na yale ya bahari ya Hindi yaani Delta.
Kwa kutumia usafiri wa boti uwapo kwenye eneo hili unaweza kuona wanyama kama Viboko, Mamba,ndege wa angani wakiwemo wale wanaohama bara moja kwenda jingine na miti ya Mikoko ambayo ni mazalia ya Samaki, Prawns na wengine wengi.
Mbugani utakutana na wanyama mbalimbali wakiwemo Simba,Nyati,Twiga,Pundamilia,Tembo,Swala na wengineo ambao wamekuwa wakionekana kirahisi na kuwafanya wageni kuburudika.
Kwa upande wa huduma, zimekuwa zikitolewa na waongoza wageni 'guides' waliobobea kwenye taaluma hiyo huku malazi na chakula vikipatikana kwa viwango vyevye ubora wa hali ya juu.
Suala la usalama, kwa hifadhi ya Taifa ya Saadani hili ni kipaumbele chao ambapo wanahakikisha mgeni anakuwa salama muda wote kuanzia pale anapoingia hifadhini hadi anapotoka na kurejea kule alikotoka akiwa kwenye usalama.
Kwanini wageni wengi wamekuwa wakifurahia Saadani? ni baada ya hamasa ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kupitia filamu yake ya Royal Tour inaonekana kuchagiza ongezeko la wageni hifadhini.
Ili kufika hifadhi ya Taifa ya Saadani unaweza kutumia usafiri wa barabara,reli na hata ndege kwa vile upo uwanja unaoruhusu ndege ndogo kutua, kimsingi hali ya miundombinu inaridhisha.
Taarifa hii imeandaliwa na Mashaka Kibaya namba ya simu
+255 766 00 33 95/ 713 25 45 50, Email: mashakakibaya@gmail.com.
Karibu Saadani National Park!







No comments:
Post a Comment