WAHITIMU TIA KAMPASI YA SINGIDA WATAKIWA KUKUMBATIA TEKNOLOJIA - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Tuesday, 2 December 2025

WAHITIMU TIA KAMPASI YA SINGIDA WATAKIWA KUKUMBATIA TEKNOLOJIA

Mkuu wa Mkoa wa Singida,  Mhe. Halima Dendego ambaye alikuwa mgeni rasmi akihutubia kwenye mahafali ya 23 ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida yaliyofanyika Desemba 2, 2025.
........................................

Na Dotto Mwaibale, Singida

MKUU wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendego amewataka Wahitimu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida wa mwaka wa masomo 2024/2025 kukumbatia Teknolojia na Akili Unde (AI) ili kwenda sanjari na zama hizi za mapinduzi ya kidijitali.

 Mhe. Dendego ambaye alikuwa mgeni rasmi ameyasema hayo leo Desemba 2, 2025 wakati akihutubia katika mahafali ya 23 ya taasisi hiyo Kampasi ya Singida.

“Katika zama hizi za mapinduzi ya kidijitali na Akili Unde (AI), soko la ajira limebadilika kwa kasi kubwa. Ajira nyingi sasa zinahitaji ujuzi wa teknolojia, ubunifu  na uwezo wa kubadilika,” alisema Dendego.

Aidha, Dendego aliwataka wahitimu hao kutumia mitandao ya kijamii kwa maendeleo, kutangaza biashara, kujifunza na kuunda mtandao wa fursa badala ya kuitumia vibaya.

Dendego alitumia nafasi hiyo kuwapongeza wahitimu hao 1,490 kwa bidii, uvumilivu na nidhamu waliyoionesha hadi kufikia hatua hiyo.

Wakati huo huo  Dendego alitoa shukurani zake za dhati kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa TIA, Profesa William Pallangyo, pamoja na Bodi ya Ushauri ya Wizara na Uongozi wote wa Taasisi hiyo kwa kazi kubwa wanayoendelea kufanya katika kuendeleza elimu ya juu nchini.

Afisa Mtendaji Mkuu wa TIA, Profesa William Pallangyo akizungumza kwenye mahafali hayo, alisema katika mwaka huu wa masomo TIA Kampasi ya Singida inajivunia kutoa jumla ya wahitimu 1,490 (wanawake 733 sawa na asilimia 49.2, na wanaume 757 sawa na asilimia 51.8)

Alisema Kati yao ngazi ya cheti cha awali ni wahitimu ni 388, Astashahada 389, shahada 373 na shahada 340.

Profesa Pallangyo alisema wahitimu hao wanawakilisha takribani asilimia 14.4 ya wahitimu wote 10,334 wa mwaka wa masomo 2024/2025 katika kampasi zote nane za TIA.

Pallangyo alisema takwimu hizo zinaonesha wazi kuwa Kampasi ya Singida inaendelea kukua kwa kasi na inachangia kwa kiasi kikubwa katika kuzalisha wataalamu wa Uhasibu, Ununuzi na Ugavi, Biashara, Rasilimali Watu na Masoko.

Aisema Kampasi ya Singida imepata mafanikio makubwa kwenye eneo la miundombinu, mafunzo, utafiti na ushauri wa kitalaamu.

Profesa Pallangyo alisema ili kuhakikisha wanaendelea kutoa elimu yenye ufanisi, Taasisi hiyo imeendelea kuboresha miundombinu ya kimkakati katika kampasi ya Singida.

Alisema kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), unaofadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Kampasi ya Singida imenufaika na Sh. Bilioni 13.5 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Taaluma.

Afisa Mtendaji Mkuu huyo wa TIA, Profesa Pallangyo alitumia nafasi hiyo kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji huo mkubwa unaolenga kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia na kuongeza tija katika utoaji elimu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wizara, Profesa Jehovaness Aikael alisema Udahili katika Kampasi ya Singida umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka mathalan katika mwaka wa masomo 2024/ 2025 kampasi hiyo ilidahili jumla ya wanafunzi 2,623 ikiwa ni ongezeko la asilimia 24, ikilinganishwa na wanafunzi 2,115 kwa mwaka 2021/ 2022 (kwa kipindi cha miaka mitano ya nyuma) na kuwa hiyo inaonesha kuongezeka kwa Imani ya elimu itolewao TIA.

Profesa Aikael aliwataka wahitimu hao kuendelea kutumia ufahamu wa kidijitali na teknolojia kufanya biashara kwa njia bunifu.

Alisema Ubunifu wa Kidijitali utawawezesha kuunda bidhaa na huduma mpya, kuongeza ushindani katika soko, na kufanikisha biashara ndogondogo kuwa kubwa, hatimaye kuchangia katika Tanzania yenye uchumi imara, jumuishi na wezeshi.

Mahafali hayo yalihudhuriwa na Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na vyama vingine vya siasa, Viongozi wa Serikali na Taasisi zisizo za kiserikali katika ngazi mbalimbali, Wahadhiri , Watumishi Waendeshaji, Wanachuo wote wa TIA na Waandishi wa Habari.

Kuhusu kozi zinazotolewa TIA Singida ni Accountancy , Procurement and logistic management, Human resource management, Business Administration na Marketing and public relation.

Kozi zote hizo zinaanzia ngazi ya cheti mpaka masters.

Kwa mawasiliano zaidi kuhusu chuo hicho unaweza kupiga simu namba 0752540341 au kupitia mtandao wao (Website) https://www.tia.ac.tz/

Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Profesa Pallangyo akizungumza wakati akitoa taarifa kwenye Mahafali ya 22 ya taasisi hiyo Kampasi ya Singida yaliyofanyika jana Desemba 2, 2025.
Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wizara, Profesa Jehovaness Aikael, akizungumza kwenye mahafali hayo.
Mkurugenzi Mkuu wa TIA Kampasi ya Singida, Dkt. James Mrema akizungumza.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo, Taaluma,, Utafiti na Ushauri  Profesa Momole Kasambala akiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wizara, Profesa Jehovaness Aikael kwenye mahafali hayo.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Singida Naima Chondo akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Godwin Gondwe.
Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Profesa Pallangyo, akimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego  kwa hotuba aliyoitoa.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego akipata maelezo ya kazi mbalimbali za ubunifu zinazofanywa na Wanafunzi wa taasisi hiyo wakati  alipotembelea banda la wabunifu hao kuona kazi zao.
Maelezo ya kazi mbalimbali za ubunifu zinazofanywa na Wanafunzi wa taasisi hiyo yakitolewa.
Brass Band ya Polisi ikiongoza maandamo ya wahitimu wa chuo hicho.
Wahitimu wakiwa katika maandamano.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego (katikati) akiongoza maandamano hayo.
Viongozi meza kuu wakishiriki wimbo wa Taifa.
Wahadhiri wa Chuo hicho wakiwa kwenye mahafali hayo.
Wahitimu hao wakionesha furaha zao wakati wa mahaflai hayo.
Wanafunzi wa chuo hicho wakiimba wimbo maalumu wa Taasisi hiyo.
Wahitimu ngazi ya shahada wakiwa kwenye mahafali hayo. Kulia ni Keneth Kalinjuma na Telesha Juma.
Taswira ya mahafali hayo.
Wahitimu wakiwa kwenye mahafali hayo.
Mahafali yakiendelea.
Wasanii wa ngoma ya kabila la Wanyaturu wakitoa burudani kwenye mahafali hayo.
Mkuu wa Kitengo cha Mitihani TIA Kampasi ya Singida, Wilson Mwakyusa akiwajibika.
Mhitimu namba moja aliyefanya vizuri katika masomo yake akipongezwa na kupatiwa zawadi.
Wahitimu wakitunukiwa vyeti vyao.
Viongozi wa TIA wakiwa kwenye mahafali hayo. Kutoka kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Masoko, Lilian Rugaitika, Mkuu wa sehemu ya vyeti, Lucas Ngwebea na Mkuu wa sehemu ya vyeti, Wilson Mwakyusa.
Wahitimu wakitunukiwa vyeti vyao.
Wageni waalikwa wakiwa kwenye mahafali hayo.
 Mhadhiri wa chuo hicho, Lukio  Mrutu akizungumza.
Mhadhiri wa chuo hicho Magreth Mapunda akizungumza

Viongozi wa TIA wakiwa kwenye mahafali hayo.
Wahitimu wakiserebuka
Brass Band ya Polisi ikiendelea kutumbuiza kwenye mahafali hayo.
Shamra shamra zikitamalaki kwenye mahafali hayo.
Shamra shamra zikiendelea
Furaha ya kuhitimu ikionekana dhahiri kwa kuserebuka
Mgeni rasmi akiwa katika picha ya pamoja na waadhiri wa chuo hicho.
 

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad