Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Juma Homera kushoto,akimkabidhi Mganga Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Aron Hyera funguo za gari la Wagonjwa la kituo cha Afya Lusewa Wilyani humo lililotolewa na Serikali ili kuhudumia wagonjwa hasa wale watakaopewa rufaa kwenda Hospitali ya Wilaya Namtumbo mjini au Hospitali ya rufaa Songea mjini.
......................................
Na Mwandishi Wetu, Namtumbo
SERIKALI imetoa gari la wagonjwa kwa kituo cha afya Lusewa Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, ili kuimarisha huduma za afya na kurahisisha rufaa za dharura kwa wagonjwa kwenda Hospitali ya Wilaya au Mkoa.
Akikabidhi gari hilo kwa Mganga Mkuu wa Wilaya ya namtumbo Aron Hyera,Waziri wa Katiba na Sheria ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Dkt. Juma Homera amesema,gari hilo ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa vitendo.
Dkt. Homera alisema kuwa,Serikali ya awamu ya sita imedhamiria kusogeza huduma muhimu karibu na wananchi hasa wale wanaoishi mbali na Hospitali ya Wilaya na mkoa ili nao waweze kupata huduma bora za afya karibu na maeneo yao.
“Serikali inatekeleza ahadi zake kwa vitendo,gari hili ni sehemu ya mkakati mkubwa wa kuondoa kero za wananchi na kuboresha huduma za afya”alisema Dkt Homera.
Aidha amesisitiza kuwa,gari hilo litoe huduma ya kusafirisha wagonjwa bure bila mwananchi kutozwa gharama yoyote ambapo amewataka watumishi wa afya na viongozi wa Serikali ngazi ya vijiji na kata ya Lusewa, kuhakikisha matumizi sahihi ya gari hilo na linatunzwa ili liweze kuhudumia wananchi hususani wagonjwa.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya Namtumbo Aron Hyera alisema,gari hilo litarahisisha rufaa za dharura kwenda Hospitali ya wilaya na mkoa na kupunguza kwa kiwango kikubwa vifo vya uzazi kwa kuwahisha akina mama wajawazito Hospitalini.
Dkt. Hyera alitaja faida nyingine ni uwepo wa vifaa vya kitabibu ndani ya gari hilo utasaidia wagonjwa matibabu wakiwa njiani,kupunguza adha na gharama kwa wananchi ambao awali walilazimika kukodi magari ya kiraia ili kuwahi kwenye vituo vya kutolea huduma za matibabu.
Dkt. Hyera amehaidi kuwa,gari hilo litatumiwa kwa malengo yaliyokusudiwa ya kuhudumia wagonjwa wa dharura na Halmashauri itahakikisha linafanyiwa matengenezo ya kitaalamu na kwa wakati ili liweze kudumu.
Katika hatua nyingine Dkt. Hyera alisema,kituo cha afya Lusewa kinahitaji ukarabati mkubwa au kujengwa upya kwa baadhi ya majengo yake ili kuendena na hadhi ya huduma zinazotolewa pamoja na kukosekana kwa mtaalam wa mionzi ili kuwapunguzia wananchi safari za mbali kufuata huduma hizo.
Pia,amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuonyesha kwa vitendo utekeleza wa Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi(CCM)ndani ya siku 100 za awali kwani upatikanaji wa gari hilo ni uthibitisho wa dhamira yake ya kuimarisha sekta ya afya.
Dkt Hyera,amempongeza Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Dkt Juma Homera kutekeleza kwa vitendo na kufuatilia vifaa tiba,magari ya wagonjwa na miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali ya Jimbo hilo.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wenzake Juma Ali,ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya afya kwa kuona umuhimu wa kutoa gari hilo ambalo litakwenda kuokoa maisha ya wananchi hususani mama wajawazito wanaopewa rufaa kwenda Hospitali ya Wilaya au rufaa kwa ajili ya kwenda kupata huduma za matibabu.
Waziri wa Katiba na Sheria na Mbunge wa Jimbo la Namtumbo mkoani Ruvuma Dkt. Juma Homera,akikata utepe kuashiria kukabidhi gari la wagonjwa katika kituo cha afya Lusewa wilayani Namtumbo Januari 18, 2026. Kulia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo, Fransis Pili.









No comments:
Post a Comment