Na Mwandishi Wetu
MFANYABIASHARA Shaban Kapelele, maarufu Mapete, amedaiwa ametekwa nyumbani kwake, Chamazi, Temeke jijini Dar es Salaam na watu wasiojulikana.
Akizungumza juzi, mke wa Mapete, Mariam Kasembe, alisema mumewe alivamiwa Januari 13, mwaka huu, akiwa nyumbani kwake.
Mariam alisema siku hiyo watu wanne waliovaa kiraia waliruka ukuta wa fensi na kwenda moja kwa moja kwenye chumba alikokuwa mumewe na kumkamata na baadaye kuondoka naye.
Alisema mumewe alikamatwa saa tisa alasiri na baadaye walitoka na kuingia naye kwenye gari nyeusi iliyokuwa imepaki nje ya jeti na kuondoka.
Mariam alisema watu wanne waliofika kumkamata mumewe walikuwa wameshika aina ya bastora na mmoja alikuwa na bunduki kubwa.
Alisema baada ya kuhoji mumewe anakamatwa kwa kosa gani alijibiwa aende Kituo cha Kati cha Polisi (Centrol), atapata jibu.
Pamoja na kwenda katika kituo hicho cha polisi alijibiwa mumewe hakupelekwa kituoni hapo.. Mariam alisema kuwa ameangaika kumtafuta vituo vyote wa polisi, lakini hajafanikiwa kumwona mpaka sasa.
Alisema kutokana na tukio hilo, familia yake inaishi kwa hofu kubwa, hivyo ameliomba jeshi la polisi kumpa ushirikiano ili kubaini aliko mumewe.
Kwa upande wake, mdogo wa Mapete, Abuu Kapelele alisema baada ya kupigiwa simu na shemeji yao, kwamba kaka yao ametekwa na watu, familia ilianza kumtafuta vituo vyote vya polisi, lakini hadi leo hawajamwona.
Abuu alisema jitihada ya kumpata kaka yao imeshindikana kutokana na kila wanapofika kituo cha polisi wanajibiwa hajaletwa na hayupo.
Ameliomba jeshi la polisi kutoa ushirikiano wa kumpata ndugu yao na kama anakabiliwa na mashtaka aweze kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum jijini Dar es Salaam, Faustine Mafwele, alisema Mapete hayupo katika kituo chochote cha polisi.
Mafwele alisema hakuna kituo cha polisi kilichoripoti tukio la kutekwa kwa Mapete, lakini wanaendelea na uchuguzi ili waweze kufahamu aliko.







No comments:
Post a Comment