MWALIMU ANAYESUMBULIWA NA KISUKARI KWA MIAKA 15 AOMBA MSAADA WA MATIBABU - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Saturday, January 3, 2026

MWALIMU ANAYESUMBULIWA NA KISUKARI KWA MIAKA 15 AOMBA MSAADA WA MATIBABU

Mwalimu Helena Nyahuru Mahamba akiwa nyumbani kwake Unyankhae Manispaa ya Singida

.............................

Na Dotto Mwaibale

Mwalimu Helena Mahamba (42) mkazi wa Unyankhae Manispaa ya Singida ambaye kwa miaka 15 anasumbuliwa na ugonjwa wa kisukari anaomba msaada wa matibabu ili aweze kupona na kuondokana na madhira anayoyapitia.

Mwalimu huyo anaishi kwa kujidunga insulin  baada ya kongosho kushindwa kufanya kazi na ametokwa vidonda katika sehemu ya mwili wake na kumfanya hashindwe kufanya kazi yoyote zaidi ya kulala kutokana na kujisikia uchovu wakati wote.

“Ugonjwa huu umeharibu kabisa mfumo mzima wa mmeng’enyo wa chakula na mifumo mingine ya mwili wangu nawaombeni watanzania nisaidieni mwenzenu sina furaha kabisa ya maisha,” anasema Mahamba huku akionesha kukata tamaa kabisa ya maisha.

Mahamba anasema alipokuwa bado msichana alianza kusumbuliwa na presha kwa kipindi cha mwaka mmoja alipokwenda hosptali na kufanyiwa vipimo ndipo alipogundulika kuwa na ugonjwa wa kisukari ambao umerudisha nyuma maisha yake.

Anasema licha ya kupata matibabu katika hospitali mbalimbali bado hajapata nafuu kila siku mwili wake umekuwa ukidhoofu huku akiandamwa na madeni.

Anasema hata utendaji wake wa kazi umeteteleka ambapo alilazimika kuhamia shule iliyojirani na mjini kutoka shule ya pembezoni mwa mji alikokuwa akifundisha ili iwe rahisi kupata huduma ya hospitali ambapo anaushukuru uongozi wa Manispaa ya Singida (mwajiri wake) kwa kumsaidia kutokana na changamoto aliyonayo.

Anasema alipokwenda Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma aliambiwa matibabu yake ni Sh. Milioni 4.8 fedha ambazo ameshindwa kuzipata.

Ndugu watanzania kila mmoja kwa imani yake, iwe taasisi yoyote ya kiserikali, sekta binafsi, wafanyabiashara na mtu mmoja mmoja mwenzetu  Mwalimu Helena amekuja kwetu anahitaji msaada apate fedha zitakazo msaidia kupata matibabu ya uhakika baada ya kuangaika kwa zaidi ya miaka 15.

Mwalimu huyu ambaye ni mama wa watoto wawili tegemeo lake kubwa kwa sasa amelielekeza kwa watanzania shime anaomba tumsaidie kwa kila hali iwe fedha na ushauri atashukuru.

Kwa yeyote atakayeguswa kumsaidia anaweza kuwasiliana naye moja kwa moja kwa namba 0787820053/ 0759521565 au Akaunti Namba 0152364578800 Benki ya CRDB Jina Helena Nyahuru Mahamba na Mwenyezi Mungu atakubariki kwa utoaji wako kwani kiasi chochote utakacho mpa kitamsaidia ili kufikisha pesa hiyo inayohitajika kwani wahenga walisema chururu si ndo-ndo-ndo.

Mwalimu Helena Nyahuru Mahamba

Taarifa hii imeandaliwa na Dotto Mwaibale namba ya simu 0754362990

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad