RC TANGA MGENI RASMI KONGAMANO LA WANAWAKE KUKARIBISHA RAMADHANI - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Thursday, 29 January 2026

RC TANGA MGENI RASMI KONGAMANO LA WANAWAKE KUKARIBISHA RAMADHANI

Mratibu wa Kongamano la Wanawake wa Kiislam la kukaribisha mwezi mtukufu wa Ramadhani Mwanakombo Kipanga akizungumza na waandishi wa habari Januari 29, 2026 Jijini Tanga kuhusu maandalizi ya kongamano hilo. Kushoto ni Mratibu wa kongaamano hilo , Shamsa  Diwani na kulia ni Muhamasishaji wa kikundi hicho, Hamida Khoja 

.....................


Na Dotto Mwaibale, Tanga

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt. Batild Burian anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Kongamano la wanawake wa Kiislam la kuukaribisha mwezi mtukufu wa Ramadhani ambalo litafanyika Januari 31, 2026 Jijini Tanga.

Katika kongamano hilo mgeni maalumu anatarajiwa kuwa Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakar Zubeir Bin Ally ambapo pia watahudhuria masheikh na viongozi mbalimbali wa Serikali na wananchi.

Kongamano hilo limeandaliwa na Wanawake wa Kiislam wa kikundi cha Subra na Nusra cha Mkoa wa Tanga.

Mratibu wa Kongamano hilo Mwanakombo Kipanga akizungumza na waandishi wa habari alisema kama jamii na kama waislam wanatambua kuwa Ramadhani siyo mwezi wa kawaida bali ni mwezi wa ibada, rehema, maghfira na kujitathimini upya katika maisha ya kila siku.

“Kwa Muktadha huu tumeona ni muhimu sana kuandaa kongamano hili ili kutoa nafasi ya elimu, mawaidha na maandalizi ya kina hususani kwa wanawake ambao ni mhimili mkubwa wa familia na malezi ya jamii,” alisema Kipanga.

Alisema lengo kuu la kongamano hilo ni kuwaandaa Waislam hasa wanawake na familia kuupokea mwezi mtukufu wa Ramadhani  kwa uelewa sahihi katika ibada zinazotakiwa, maadili mema pamoja na wajibu wao ndani ya familia na jamii kwa ujumla.

Kipanga alisema katika kongamano hilo kutakuwa na mada mbalimbali zitakazo tolewa na Masheikh na walimu wa dini kutoka maeneo mbalimbali wenye uzoefu wa masuala ya dini na jamii.

Alisema mada hizo zimeandaliwa kwa kuzingatia changamoto halisi wanazokutana nazo katika maisha ya kila siku.

Alizitaja baadhi ya mada zitakazo jadiliwa kuwa ni pamoja na maandalizi ya mwanamke na familia kuukaribisha mwezimtukufu wa Ramadhani ikizingatia ibada, malezi na majukumu ya kifamilia.

Kujenga uoga wa Mwenyezi Mungu, subira na ikhlasi katika ibada ili Ramadhani iwe na tija ya kweli, jinsi ya kulea , hasa watoto katika mazingira ya Ramadhani ili wajifunze ibada, adabu na nidhamu pamoja na umuhimu wa maadili mema katika mwezi mtukufu na hata baada ya Ramadhani.

Kwa upande wake Katibu wa Kikundi hicho Hawa Mweri alitumia nafasi hiyo kutoa wito kwa wanawake wote, vijana, familia na jamii kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kushiriki kongamano hilo muhimu na kueleza kwamba elimu na mawaidha yatakayopatikana yatakuwa na manufaa makubwa siyo tu kwa kipindi cha Ramadhani bali pia kwa maisha yao ya kila siku. 

Mratibu wa kongamano hilo, Shamsa  Diwani akichangia jambo kuhusu maandalizi ya kongamano hilo. Kushoto ni mtunza fedha wa kikundi cha Subra na Nusra waandaaji wa kongamano hilo. Kibibi Kibao na kulia ni Mratibu wa Kongamano hilo, Mwanakombo Kipanga.

Waandishi wa habari wakiwa kwenye mkutano huo.
Katibu wa Kikundi hicho, Hawa Mweri akichangia jambo kwenye mkutano huo na waandishi wa habari. Kulia ni Makamu Mwenyekiti wa Kikundi hicho, Rukaiya Ally.

 

 Viongozi wa Kikundi hicho wakiwa kwenye mkutano huo na Waandishi wa Habari.

Taarifa hii imeandaliwa na Dotto Mwaibale simu namba 0754362990 

 

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad