AKWILAPO ASISITIZA MAENEO YA UMMA KUPIMWA NA KULINDWA KUEPUKA UVAMIZI - SINGIDANI BLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Wednesday, 18 February 2026

AKWILAPO ASISITIZA MAENEO YA UMMA KUPIMWA NA KULINDWA KUEPUKA UVAMIZI

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo akizungumza na wananchi wa Soni katika halmashauri ya Bumbuli wilaya ya Lushoto mkoani Tanga wakati wa ziara ya Waziri Mkuu Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba tarehe 17 Februari 2026.
Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba akiwasili Majulai Mlalo kuzindua shule mpya ya Amali ya Majulai wakati wa ziara yake wilayani Lushoto mkoa wa Tanga. Wa pili kulia ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Leonard Akwilapo
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Leonard Akwilapo (wa pili kulia) akiwa na baadhi ya Mawaziri waliokuwa kwenye ziara ya Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchema wilayani Lushoto mkoa wa Tanga.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Leonard Akwilapo akimsikiliza mmoja wa mwananchi aliyewasilisha kero yake ya ardhi mbele ya Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchema wakati wa ziara wilayani Lushoto mkoa wa Tanga.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Leonard (Kushoto), Ashatu Kijaji, Waziri wa Maliasili na Utalii pamoja pamoja na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Balozi Dkt. Bashuru Ally wakiwa keenye ziara ya Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchema wilayani Lushoto mkoa wa Tanga.
Sehemu ya wananchi wa Mlalo waliojitokeza kushuhudia uzinduzi wa shule mpya ya Amali ya Majulai wakati wa ziara ya Waziri Mkuu wilayani Lushoto mkoa wa Tanga.
 Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba akiweka jiwe la msingi kwenye shule Mpya  ya Amali ya Majulai wakati wa ziara yake wilayani Lushoto mkoa wa Tanga. Kulia ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Leonard Akwilapo.
Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba akizungumza na wananchi wa Soni katika halmashauri ya wilaya ya Bumbuli wakati wa ziara yake wilayani Lushoto mkoa wa Tanga tarehe 17 Februari 2026.
-------------------------------------

Na Munir Shemweta, Lushoto WANMM

Katika jitihada za kuhakikisha maeneo ya umma hayavamiwi na kusababisha migogoro ya ardhi, Serikali imeendelea kusisitiza taasisi za umma nchini kupima na kuyalinda maeneo yake.


Kauli hiyo ya Serikali inafuatia kujitokeza kwa changamoto za ardhi katika eneo la Ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Lushoto (Bomani) pamoja na Halmashauri ya wilaya ya Bumbuli ambapo baadhi ya wananchi wamedai kuondolewa kwenye maeneo wanayomiliki wakati wa ziara ya Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba wilayani Lushoto mkoa wa Tanga.


Akizungumza kwa nyakati tofauti katika mikutano ya hadhara kwenye eneo la Lushoto, Soni pamoja na Mlalo tarehe 17 Februari, 2026, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Leonard Akwilapo, amesema kuwa katika kukabiliana na tabia ya uvamizi wa maeneo ya umma, taasisi za Serikali zinatakiwa kuchukua hatua za kupima maeneo yake yote pamoja na kuyalinda.


“Nitoe maelekezo kwa taasisi zote za Serikali, Wizara ya Ardhi tupo; tupo kutoa hati katika maeneo ya Serikali,” amesema Mhe. Dkt. Akwilapo.


Pamoja na kuzitaka taasisi za Serikali kuchukua hatua hiyo, Dkt. Akwilapo amesisitiza pia wananchi kupima maeneo yao wanayomiliki, sambamba na kuacha kujenga kiholela ambapo aliwataka kuomba vibali vya ujenzi pale wanapotaka kufanya maendelezo.


“Ninyi wananchi msijenge kiholela. Tupo kuwapa hati; ombeni hati, tutawapa, na baadaye muombe vibali vya ujenzi ili mjenge nyumba mkiwa na amani na muwe na furaha,” amesema Waziri wa Ardhi.


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amehitimisha ziara yake mkoani Tanga jana ambapo alizindua Jengo la Oxygen katika Hospitali ya Wilaya ya Lushoto pamoja na Shule Mpya ya Amali ya Majulai, Mlalo pamoja na kuzungumza na wananchi wa Soni katika halmashauri ya Bumbuli.


Katika ziara yake hiyo Dkt Mwigulu Nchemba alikagua na kuzindua miradi ya maendeleo, iliyoambatana pia na kupokea kero kutoka kwa wananchi, pamoja na kuchukua hatua stahiki katika maeneo yenye changamoto.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad