RAMADHANI KIELELEZO CHA UTII KWA VIONGOZI - SINGIDANI BLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Monday, 16 February 2026

RAMADHANI KIELELEZO CHA UTII KWA VIONGOZI

Mwenyekiti wa JUQUSUTA Taifa, Shekh Mohamed Said Ruiya Ashjar (wa tatu kutoka kushoto), akizungumza baada ya kupokea Zafa katka uwanja wa Nyamagana.
Mlezi wa JUQUSUTA na Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Hasan Kabeke (wa nne) kutoka kushoto, leo, akiongoza Zafa ya kuuribisha Mwezi wa Ramadhani.
Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Hasani Kabeke, akifafanua kwa waandishi wa habari jambo kuhusu Zafa, leo .

Vijana wa Madrasa Sainnaa ya Ilemela, wakonesha manjonjo yao wakati wa Zafa iliyofanyika, leo.

Na Baltazar Mashaka, Mwanza

WAUMINI wa Dini ya Kiislamu jijini Mwanza, leo wamefanya maandamano ya amani (Zafa) kuukaribisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, huku wakikumbushwa umuhimu wa kuwatii viongozi wa dini na serikali kama sehemu ya mafundisho ya mwezi huo.

Akizungumza baada ya kupokea maandamano hayo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kuendeleza Q’uran na Sunna Tanzania (JUQUSUTA), Sheikh Mohamed Said Ruiya Ashjar, alisema Ramadhani ni kielelezo cha utii kwa kuwa humjenga Muislamu kuwa tayari kuacha vyakula, vinywaji na matendo yasiyompendeza Mwenyezi Mungu kwa hiari na kwa nidhamu ya hali ya juu.

Alisema Zafaa ya kuelekea Ramadhani ya mwaka huu ni ya 18 ikiwa na kaulimbiu ya kuhimiza utii, ikiwa na ujumbe usemao: ‘Kuwatii Viongozi ni Wajibu na Ramadhani ni Kielelezo’.

“Utii ni wajibu. Kama ambavyo Waislamu huacha kula na kunywa kwa hiari bila kusimamiwa, ndivyo wanavyopaswa kuwatii viongozi wao wa dini na serikali wanapotoa maelekezo yaliyo halali, na kuyatekeleza,” alisema Sheikh Ruiya Ashjar.

Aliongeza kuwa viongozi wa serikali wakiongozwa na Samia Suluhu Hassan pamoja na viongozi wa dini wanastahili kupewa heshima na ushirikiano kwa kuwa wanalenga ustawi na maendeleo ya jamii.

Kwa upande wake, Mlezi wa JUQUSUTA na Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Sheikh Hasani Kabeke, alisema Zafa si maandamano ya kisiasa bali ni mkusanyiko wa waumini kwa lengo la kujiandaa kiroho na kuelimishana kabla ya kuanza kwa ibada ya Saumu, ambayo ni miongoni mwa nguzo tano za Uislamu.

Alisema kuwa, Ramadhani ni kipindi cha ibada, toba na kusaidiana, hivyo taasisi na watu binafsi wanapaswa kuepuka kuutumia mwezi huo kama fursa ya kujinufaisha kibiashara au kukiuka maadili.

“Wafanyabiashara na matajiri wanapaswa kufungua nyoyo na mifuko yao kwa kuwasaidia wenye uhitaji kwa kuwapatia futari na mavazi. Huu ni mwezi wa rehema na mshikamano,” alisema Sheikh Kabeke.

Aidha, aliwataka wafanyabiashara kuepuka kupandisha bei za vyakula kiholela katika kipindi hicho, akisisitiza kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha maadili ya dini na wanakuwa wanaawadhulumu waislamu

Pia aliwahimiza waumini kuacha vitendo vya uongo, utapeli, matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii, pamoja na maasi mengine, na badala yake wajikite katika ibada na matendo mema.

Sheikh Kabeke aliwataka Watanzania wa dini zote kuendelea kudumisha amani na utulivu nchini, akibainisha kuwa maendeleo hayawezi kupatikana bila mazingira ya amani.

“Ni wajibu wetu kuiombea nchi amani na kuwaombea viongozi wetu wa dini na serikali. Amani ikivurugika hakuna jambo litakalofanyika,” alisisitiza.

Aliongeza kuwa jamii inapaswa kurejea katika maadili mema kwa kuwalea watoto katika misingi ya dini, kuwaheshimu wazazi na viongozi, na kujenga utamaduni wa uwajibikaji kuanzia ngazi ya familia hadi taifa kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad