TSIA YAIOMBA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KUSIMAMIA SEKTA HIYO - SINGIDANI BLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Tuesday, 24 February 2026

TSIA YAIOMBA SERIKALI KUTUNGA SHERIA KUSIMAMIA SEKTA HIYO

Mwenyekiti wa Chama cha Sekta Binafsi ya Ulinzi  Tanzania (TSIA), Kanda ya Kati Dodoma, Lukanus Kayombo, akizungumza na waandishi wa habari Februari 24, 2026 kuhusu maandalizi ya mkutano mkuu wa kwanza wa sekta hiyo Jijini Dodoma. Kushoto ni Mweka Hazina wa chama hicho wa kanda hiyo na Mkurugenzi wa Kampuni ya Tele Security,  Fidelis Luhunga. 

.................................... 

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

CHAMA cha Sekta Binafsi ya Ulinzi  Tanzania (TSIA), kimeiomba Serikali kuunda sheria itakayosimamia sekta ya ulinzi binafsi jambo litakalosaidia kujiendesha kwa ufanisi.

Hayo yamezungumzwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Kanda ya Kati, Lukanus Kayombo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Februari 24, 2026 kuhusu maandalizi ya mkutano mkuu wa kwanza wa sekta hiyo utakaofanyika kesho Jijini Dodoma.

“ Kwenye sekta yetu hii changamoto kubwa tuliyonayo ni kukosekana kwa sheria, kumbukeni kwamba tuliianzisha tangu mwaka 2005 ukipiga mahesabu ina miaka zaidi ya 42 pamoja na kuwa ni sekta kubwa haina sheria licha ya kuwa na makampuni mengi nchini,” alisema Kayombo.

Kayombo aliongeza kuwa kuwepo kwa sheria hiyo kutasaidia mambo mengi ikiwa na kupanga bei elekezi ya mishahara pamoja na maslahi ya wafanyakazi.

Akizungumzia maandalizi ya mkutano huo ambao utafanyika sanjari na uchaguzi wa viongozi wa sekta hiyo Mkoa wa Dodoma alisema yamekamilika na kuwa kufuatana  na katiba ya ulinzi ya sekta hiyo  kila baada ya miaka mitano  wanafanya uchaguzi.

Alisema kesho Februari 25, 2026 watafanya uchaguzi wa viongozi Mkoa wa Dodoma na kueleza kuwa makampuni yote wanachama wa TSIA yatawakilishwa na wajumbe watatu kwenye mkutano huo ambao utafanyika ukumbi wa maktaba ya mkoa kuanzia saa 4:00 asubuhi na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Dodoma.

Aidha, Kayombo alisema uchaguzi huo ngazi ya mkoa utafanyika katika mikoa yote ya kanda hiyo ambayo ni Dodoma, Manyara, Singida na Tabora.

Kayombo alitumia nafasi hiyo kuyahimiza makampuni yote ya sekta hiyo yaliyopo Dodoma na Mameneja kuhamasika kufika kuhudhuria mkutano huo muhimu.

Mwenyekiti wa Chama cha Sekta Binafsi ya Ulinzi  Tanzania (TSIA), Kanda ya Kati Dodoma, Lukanus Kayombo, akisisitiza jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari.
Mweka Hazina wa chama hicho wa kanda hiyo,  Fidelis Luhunga, akizungumza kwenye mkutano huo.
Mweka Hazina wa chama hicho wa kanda hiyo,  Fidelis Luhunga, akisisitiza jambo kwenye mkutano huo na kusisitiza umuhimu wa kuwepo kwa sheria ya kusimamia sekta hiyo.
 

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad