WANANCHI KIWAMBE WALILIA UMEME, WAMPIGIA MAGOTI RAIS SAMIA - SINGIDANI BLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Friday, 27 February 2026

WANANCHI KIWAMBE WALILIA UMEME, WAMPIGIA MAGOTI RAIS SAMIA

                             Wananchi wa Kijiji cha Kitanga. Kitongoji cha Kiwambe, wilayani Kisarawe, Mkoa wa Pwani, wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kuzungumza na waandishi wa habari walipokuwa wakitoa kilio chao cha kuomba huduma ya umeme.

................................... 

 Na Mwandishi Wetu, Pwani. 

WANANCHI wa Kijiji cha Kitanga. Kitongoji cha Kiwambe, wilayani Kisarawe, Mkoa wa Pwani, wamemwomba Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, kuwawezesha kuwapatia umeme  ili waweze kufanya shughuli za maendeleo ambazo zitainua uchumi wao. 

Wakizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika jana, kijijini hapo, wananchi hao walisema Kitongoji chao kama kimetengwa kutokana na kutopitiwa na miundombinu ya umeme, licha ya serikali kuwaahidi mara kwa mara, lakini hakuna utekelezaji.

Mmoja wa wananchi hao Luce Elias alisema Kitongoji chao kinakosa maendeleo kutokana na hawajaunganishiwa miundombinu ya umeme   ambayo ingewasaidia kufanya biashara muda wote.                                

 Luce alisema kero kubwa katika kitongoji hicho ni umeme ukizingatia baadhi wa Kitongoji vya mbali vimepata miundo mbinu hiyo, lakini wao wamerukwa huku wakiishia kupewa aahadi na viongozi mbalimbali wa serikali. 

Alisema kutokana na kupewa aahadi ya kupatiwa umeme zisizotekelezeka amemwomba Rais Samia kuwatupia jicho la tatu ili waweze kupatiwa umeme. 

 Pia alisema baadhi ya watu wanashindwa kwenda kujenga viwanja vyao kutokana na hakuna umeme katika eneo hilo. 

Naye, Bahati Nicodemus alisema kukosekana kwa umeme katika Kitongoji chao ni mateso makubwa.       Nicodemus alisema inashangaza Kiwambe kukosa umeme wakati baadhi ya Kitongoji viko mbali kutokana Jiji la Dar es Salaam, lakini vimefikiwa na umeme. 

Alisema pamoja na viongozi mbalimbali wakiwamo wa TANESCO Wilaya ya Kisarawe kuwaahidi kuwapatia umeme, lakini utekelezaji wake umekuwa mdogo. 

Alisema kutokana na kupewa aahadi zisizotekelezeka na baadhi ya viongozi wa serikali, amemwomba mbunge wa Kisarawe, Seleman Jafu kuwafikishia kero yao kwa Rais Samia, kwa alichaguliwa kwa ajili ya kuwatumikia wananchi. 

Alisema pamoja na Kiwambe wamejengewa Zahanati, lakini inashindwa kutoa baadhi ya huduma kutokana na hakuna umeme.


Kwa upande wake, Venance Baridi alisema tangu Januari mwaka jana, waliahidiwa wangepatiwa umeme lakini wameendelea kupigwa danadana. 

 "Tunamwomba Waziri wa Nishati, Mbunge na Rais watusaidie, tumewachagua watutumikie," alisema Baridi. 

Meneja wa TANESCO Mkoa wa Pwani, Mahawa Mkaka, amewataka wakazi wa Kiwambe kuendelea kuwa wavumilivu, kwani viongozi vyote vitapatiwa umeme kwa awamu tofauti.

Mkaka alisema serikali itatekeleza miradi yote, baada ya vijiji vyote ya mkoa wa Pwani kufikiwa na umeme na sasa Kitongoji 64 vya Kisarawe vitaanza kupatiwa umeme katika awamu ya kwanza.

Meneja huyo, aliwaondoa wasiwasi wakazi wa Kitongoji cha Kiwambe kuwa serikali itawapatia umeme, licha kwa awamu tofauti.

"Kitongoji vyote vitapatiwa umeme na serikali kwa hatua kwa hatua, wakazi wa Kiwambe wawe wavumilivu," alisema Mkaka. 

Alisema Pwani kuna Kitongoji 330 na vyote vitafikiwa na miundombinu ya umeme kwa awamu tofauti.   

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad