WAWAKILISHI WAASWA KUWA MABALOZI WA KUULINDA MUUNGANO - SINGIDANI BLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Friday, 27 February 2026

WAWAKILISHI WAASWA KUWA MABALOZI WA KUULINDA MUUNGANO

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni akizungumza wakati akifungua Semina kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar kuhusu Elimu ya Muungano iliyofanyika katika Ukumbi wa Mkutano wa Baraza la Wawakilishi Unguja, Zanzibar, Februari 27, 2026.
Baadhi ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar wakiwa katika semina kuhusu Muungano iliyofanyika katika Ukumbi wa Mkutano wa Baraza la Wawakilishi Unguja, Zanzibar, Februari 27, 2026.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Richard Muyungi (kushoto) akiwa miongoni mwa viongozi walioshiriki semina kuhusu elimu ya Muungano iliyotolewa kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar katika Ukumbi wa Mkutano wa Baraza la Wawakilishi Unguja, Zanzibar, Februari 27, 2026.
---------------------

Na Mwandishi Wetu- Unguja

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Hamad Yussuf Masauni, amewaasa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuelimisha wananchi kuhusu misingi, faida na wajibu wao katika kulinda na kuutetea Muungano, 


Pia amewataka Kupinga na kusahihisha upotoshaji wa taarifa kuhusu Muungano, hususani kupitia mikutano ya hadhara na mitandao ya kijamii.


Amesema, kwa kufanya hivyo, Wawakilishi watakuwa mabalozi wa amani, umoja na mshikamano wa kitaifa, kusikiliza na kuwasilisha.


Waziri Masauni aliyasema hayo Februari 27,2026 wakati akifungua semina ya elimu ya Muungano kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, ikiwa ni sehemu ya mpango unaoendelea wa kutoa elimu hiyo kwa makundi mbalimbali ya jamii.


Amesema, kwa ujumla Wawakilishi ni nguzo muhimu ya kulinda na kuimarisha Muungano wa Tanzania kwa kupitia kutunga sheria, kusimamia Serikali na kuelimisha wananchi.


“Wawakilishi mnabeba dhamana ya kihistoria ya kuhakikisha Muungano unaendelea kuwa chanzo cha amani, mshikamano wa pande mbili na maendeleo,” alisema


Amesema, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ni nguzo muhimu katika kuendelea kuuelimisha na kuulinda Muungano wa Tanzania kwa kuwa wako karibu zaidi na wananchi.


Amesema, Wajumbe hao wana nafasi kubwa ya kuifikisha elimu ya Muungano kwa wananchi kwa sababu wanawakilisha na kukutana na wananchi mara kwa mara katika majimbo yao.


 “Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ni nguzo muhimu katika kuulinda Muungano wetu, wanawafikia wananchi wengi zaidi, hivyo wana wajibu wa kueneza elimu ya Muungano katika maeneo yao,” amesema


Ameeleza kuwa kwa kiasi kikubwa mpango huo unawalenga vijana ili waweze kufahamu fursa zilizopo ndani ya Muungano na kuzitumia kwa maendeleo yao na taifa kwa ujumla.


Amesema, fursa za Muungano ni nyingi, lakini changamoto iliyopo ni kutokuzitangaza na kuzifafanua ipasavyo kwa wananchi.


Kupitia semina hiyo mada mbali mbali zimewasilishwa kama vile Chimbuko, Misingi, Umuhimu wa Muungano, na Upekee wa Muungano.


Amesema, kupitia mada hizo wawakilishi hao watakuza na kuongeza uelewa na kutoa taswira pana juu ya umuhimu wa uwepo wa Muungano na kuibua hamasa ya katika kujenga uzalendo wa dhati kwa nchi, kuudumisha na kuuenzi Muungano kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.


Kwa upande wake, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Dkt. Richard Muyungi, amesema ofisi hiyo itaendelea kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ili kuhakikisha uelewa wa masuala ya Muungano unaongezeka na kuimarika.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad