BUYUNI KUPANDA MITI 5000 KUMUUNGA MKONO RAIS SAMIA - SINGIDANI BLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Wednesday, 25 March 2026

BUYUNI KUPANDA MITI 5000 KUMUUNGA MKONO RAIS SAMIA

  Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Buyuni, Sylvanus Mwenda, (kushoto) na Afisa Mtendaji, Marry Innocent, akipanda miti katika zoezi lililofanyika Machi 23, 2026.
..............................

Na Mwandishi Wetu.

WAKAZI wa Buyuni, Ilala jijini Dar es Salaam, wameshiriki katika zoezi la upandaji miti kwa lengo la kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan.

  

Zoezi hilo lilifanyika jana na wakazi wa  Buyuni, wakiongozwa na Mwenyekiti wa serikali ya mtaa, Sylvanus Mwenda, kupanda miti katika maeneo mbalimbali.


 Akizungumza katika zoezi hilo la upandaji miti, Mwenda alisema wanakusudia kupanda miti 5000 katika mtaa wake. 


Mwenda alisema lengo la kupanda miti hiyo ni kuunga mkono kauli mbiu ya Rais Dk. Samia ambaye amekuwa akiwahimiza  watanzania nchini kupanda miti kila mwaka.


 Alisema pamoja na kuungana na rais katika zoezi hilo, lakini alimpongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ilala jijini Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya kwa kumpa miti 5000 bure.

  

Mwenyekiti huyo aliyeshiriki zoezi la upandaji miti akiwa na mtendaji wake wa mtaa, Marry Inocent na wakazi wa eneo hilo,  alisema wataendelea kupanda miti katika maeneo ya wazi kwa lengo la kuleta uoto mpya  baada ya ule wa asili kutoweka kufuatia  wenyeji wa Buyuni kukata miti ovyo. 


Mwenda alisema dhamira yake ni kutaka kuona Buyuni inakuwa ya madhari ya kijani huku akihimiza kila mkazi wa Buyuni kushiriki katika zoezi la upandaji miti na kuituza.  


Pia, Mwenda alimshukuru Diwani wa Kata ya Buyuni, Jessica Msolla, kwa kuungana naye katika jitihada za kufanikisha zoezi la upandaji miti.


"Namshukuru diwani ananipa ushirikiano  katika kila jambo la kimaendeleo  ni mchapakazi sana, wakazi wa Buyuni wamepata diwani mpenda maendeleo," alisema Mwenda. 


Naye, Halid Zuber, alisema kitendo cha wanabuyuni kushiriki katika zoezi la upandaji miti ni jambo nzuri, kwani miti ni uhai wa mazingira.  


 "Miti ni uhai wa nchi yetu, kwani hutengeneza uoto katika mazingira yetu," alisema Zuber.        

Pia alimpongeza mwenyekiti wa mtaa huo, kwa jitihada zake za kumuunga mkono Rais Dk Samia katika zoezi la upandaji miti," alisema.

 Kwa upande wake, Shufara Mchomvu alisema kwa kushirikiana na viongozi na wakazi  wa Buyuni anahitaji kuona zoezi la upandaji miti likiwa endelevu kila mwaka, kwani miti hutunza mazingira.

Shufara aliwataka wakazi wa mtaa huo, kuendelea kujitokeza katika zoezi la upandaji miti.                    

Kasim Litulu alisema miti ina faida nyingi, kwani huleta mazingira bora, lakini madhari nzuri katika makazi yao.    Litulu alisema dhamira ya mwenyekiti wao ni kuweka mazingira yanayopendeza katika mtaa wake kwa kupanda miti, ikizingatia yeye ni mwanamazingira. 


No comments:

Post a Comment

Post Top Ad