Waombolezaji wakiwa wamebeba jeneza lenye mwili wa Marehemu Mwalimu Helena Nyahuru Mahamba (42), wakati wa ibada yake ya kumuaga iliyofanyika leo Machi 29, 2026 nyumbani kwao Nkuhungu Chama Jijini Dodoma.
Mwalimu Helena Mahamba enzi zake kabla ya kuanza kuumwa.
Mwalimu Helena Mahamba alivyokuwa wakati anapigania uhai wake............................
MAZIKO ya Mwalimu
Helena Mahamba (42) wa Shule ya Msingi Unyakhae katika Manispaa ya Singida ambaye
alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kisukari kwa miaka 17 na kufariki Hospitali
ya Benjamin Mkapa Jijini Dodoma alipokuwa akipatiwa matibabu kufanyika nyumbani kwao mkoani
Mara.
Mwili wa
marehemu Mahamba umeagwa leo Machi 29, 2026 nyumbani kwao Nkuhungu jijini
Dodoma ambapo ilifanyika ibada fupi iliyoongozwa na Katekista wa Kanisa
Katoliki Parokia ya Nkuhungu, Rafael Mlingula akishirikiana Joseph Ghumpi.
Ibada hiyo
ilihudhuriwa na ndugu, jamaa, marafiki wakiwepo maafisa wa Jeshi la Magereza wakiongozwa
na Kamishna Msaidizi wa jeshi hilo (ACP) Lumumba Kashura kwa niaba ya Kamishna Generali wa jeshi hilo, ambao walifika
kumfariji mwenzao Sajenti Waero Thong’ro kwa kufiwa na mke wake Helena Mahamba.
Katekista
Rafael akihubiri katika ibada hiyo alisema kila mtu anapaswa kujitafakari
kwanini yupo hapa duniani na baada ya kifo atakwenda wapi na kueleza kuwa Mungu
yupo na wanadamu katika maisha yao ya kila siku.
“Mungu
amekuwa akitukumbusha wakati wote kutenda mema na kuwaombea ndugu zetu
waliofariki kama Helena Mahamba ili wapate uzima wa milele,” alisema Mlingula.
Mwalimu
Philipina Mboya akizungumza kwa niaba ya Mwajiri wa Helena Mahamba, alisema
wamesikitika sana kwa kifo chake na kuwa ameumwa kwa muda mrefu.
“Helena ni
Mwalimu wetu, tunasikitika sana kwa kifo chake ukweli ameugua muda mrefu na
sisi kama walimu wenzake na mwajiri wake tumeweza kushirikiana naye kuhakikisha
anapata matibabu na mara ya mwisho aliomba tumpeleke Hospitali ya Benjamin
Mkapa ili aweze kuwa karibu na baba yake mzazi katika kumuuguza,” alisema
Mboya.
Mboya aliongeza
kuwa Mwajiri wake Helena yupo na familia hiyo bega kwa bega na kuhakikisha
mwili wake unasafirishwa kutoka Dodoma hadi nyumbani kwao mkoani Mara na kuwa
salamu zao za rambirambi watazitoa kesho mkoani Singida watakapokuwa wakiuaga rasmi
mwili wake.
Kwa mujibu
wa Mama wa Marehemu Helena, Regina Muhere (Mahamba), alisema mwili huo unaondoka
leo Machi 29,2026 kwenda nyumbani kwake Singida.
Alisema
kesho (Jumatatu) Machi 30, 2026 ndugu, jamaa, majirani na walimu wenzake
watatoa heshima za mwisho na kisha kuelekea mkoani Mara na Machi 31, 2026 maziko
yake yatafanyika Kijiji cha Sota Shirati.
Mahamba
ambaye alikuwa amelazwa katika hosptali hiyo alifariki Machi 28, 2026 saa 9
usiku.
Mwalimu Mahamba
baada ya kushindwa kumudu gharama za matibabu alilazimika kubaki nyumbani
akijiuguza huku hali yake ikiendelea kudhoofu kila siku.
Taarifa zake zilipotolewa kwenye mitandao ya
kijamii akiomba msaada wa matibabu na kwa jitihada za Naibu Waziri wa Afya Dkt.
Florence Samizi alipoisoma taarifa hiyo aliagiza mgojwa huyo apelekwe Hospitali
ya Rufaa ya Mkoa wa Singida kuanza matibabu upya.
Pamoja na
kuanza matibabu hali yake iliendelea kuwa mbaya na Machi 14, alipata rufaa ya
kuhamishiwa Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma kwa ajili ya kuendelea
kupata matibabu.
Mwalimu
Mahamba wakati akipigania uhai wake akiwa nyumbani kwake eneo la Unyakhae alidai
kuwa tangu alipokuwa anaumwa katika kipindi cha miaka 17 Chama cha Walimu
Tanzania (CWT) Manispaa ya Singida kama
mwana chama wao kilimpatia Sh. 100,000 tu huku mwajiri wake naye akidaiwa
kushindwa kumsaidia.
Baadhi ya
viongozi wa chama hicho wakielezea suala hilo walisema katika katiba yao hakuna
kipengele ambacho kinaeleza mwanachama wao anapokuwa na changamoto yoyote
ikiwemo kuumwa apatiwe msaada na kama atapatiwa ni msaada tu wa vitu vidogo
vidogo kama matunda ambavyo atapatiwa kama hisani.
Kauli hiyo
iliwaibua baadhi ya walimu na kuomba katika
katiba yao kuwepo kipengele cha kuwasaidia walimu wanapo kuwa na changamoto
mbalimbali ikiwemo ya magonjwa kutokana na michango yao wanayoichangia kila
mwezi.
Mmoja wa Walimu
hao Robert Mtinga alisema katika Manispaa ya Singida wapo zaidi ya waimu 800 na kila mwezi kila mmoja hukatwa siyo chini ya Sh. 33,000 na wale ambao
wapo daraja la juu hukatwa zaidi ya kiwango hicho na kueleza kuwa ni fedha
nyingi zinazokusanywa.
Aliongeza
kueleza kuwa yakipigwa mahesabu ni fedha nyingi ambazo zinapatikana katika manispaa
ambapo wanaomba ziwe zinatumika kuwasaidia wanapokuwa na changamoto badala ya
kusubiri kusaidiwa jeneza na kusafirishwa kwenda makwao wakifariki.
Kwa upande
wake Mwalimu Helman Magoti alisema ni vema kuipitia katiba yao vizuri ili
kuielewa kama hakuna kipengele cha kutambuliwa wanapokuwa na changamoto ya
maradhi ili wapiganie kiwekwe kwa maslahi mapana ya walimu.
Mwalimu
Helena Mahamba ameacha watoto wawili wa kike na wakiume.
Buriani Mwalimu
Helena Mahamba mwendo umeumaliza kapumzike kwa amani huku ukiwaachia walimu
wenzako changamoto za kupigania haki na maslahi yao kwa mwajiri na CWT.
Bwana Alitoa
na Bwana Ametwaa jina lake Lihimidiwe Milele Daima.
Taarifa hii imeandikwa na Dotto Mwaibale simu namba 0754362990.
Katekista wa Kanisa Katoliki Parokia ya Nkuhungu, Rafael Mlingula, akiombea mwili wa Marehemu Helena Mahamba nyumbani kwao Nkuhungu Chama Jijini Dodoma.Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida, Mwalimu Mwalimu Philipina Mboya akizungumza kwenye ibada hiyo.Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Magereza (ACP), Lumumba Kashura, akizungumza kwa niaba ya Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza nchini (CGA), Jeremiah Katungu wakati akitoa salamu za rambirambi kwenye ibada hiyo.Gari la Magereza lililobeba mwili wa marehemu Helena Mahamba likiwasili nyumbani kwao Nkuhungu Chama jijini Dodoma kwa ajili ya kuugwa na baadaye kusafirishwa kwenda kwao mkoani Mara kwa maziko.
Waombolezaji wakiwa wamebeba jeneza.
Baba wa marehemu Mzee Nyahuru Mahamba, akitoa shukrani kwa watu wote waliomsaidia mtoto wake wakati wote wa kuumwa kwake.
Mtoto wa Marehemu Edwin Waero Thong'ro, akitoa heshima za mwisho kwa mama yake.
Baba waa Marehemu Mzee Nyahuru Mahamba, akiwa amepigwa butwaa kufuatia kifo cha mwanaye wa kwanza wa kike Mwalimu Helena Mahamba.
Mume waa Marehemu Helena Mahamba, Waero Thong'ro akiwa na huzuni wakati akimuaga mpendwa wake.
Jeneza lenye mwili wa marehemu Helena Mahamba likipelekwa eneo lilotengwa kwa aajii ya ibada yake ya kuagwa.
Mama yaake Helena Mahamba Bi. Regina Muhere akiwa na huzuni kubwa kwa kuondokewa na binti yake.
Mtoto wa marehemu, Edwin Waero Thong'ro akifarijiwa.
Huzuni ukitamalaaki kwenye ibada hiyo.
Waombolezaaji wakiwa kwenye ibada hiyo
Huzuni ukitawala wakati wa kumuaga mpendwa wao Mwalimu Helena Mahaamba.
NNNi huzuni tupu katika ibada hiyo.
Ukimya ukiwa umetawala kwenye ibada hiyo.
Taswira ya ibada hiyo.
Chakula kikigawiwa wakati wa ibada hiyo.
Jeneza la marehemu likiwa limebebwa
Waombolezaji wakiwa kwenye msiba huo.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Nkuhungu Chama akizungumza wakati wa ibada hiyo.
Waombolezaji wakitoa heshima za mwisho kwa marehemu.









No comments:
Post a Comment