......................................
Na Mwandishi Wetu.
MBUNGE wa Jimbo la Ukonga kupitia Chama Cha ACT Wazalendo, Bakari Shingo, amesema atahakikisha wanajenga soka la kisasa kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo wadogo maarufu wamachinga wanaofanya biashara za Gongo la Mboto, Ilala jijini Dar es Salaam.
Shingo aliyasema hayo, Machi 7, 2026 wakati wa mkutano wa wafanyabiashara hao, uliofanyika Gongo la Mboto.
Mkutano huo ambao pia ulihudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam, Edward Mpogolo na viongozi wengine wa serikali, ulitenga kutatua kero ya wafanyabiashara hao.
Mbunge huyo alisema kuwa kwa kushirikiana na serikali wanaendelea na mchakato wa kujenga soko kwa wafanyabiashara wa Gongo la Mboto ili waweze kufanya biashara zao katika sehemu salama.
Alisema kwa kuwa kazi mojawapo ya mbunge ni kuisimamia serikali atahakikisha soko hilo linajengwa ifikapo Julai, mwaka huu.
Shingo alisema kuwa kwa sasa wapo katika mpango wa kupata eneo kwa ajili ya ujenzi wa soko hilo.
"Mimi kama mbunge wenu wa Jimbo la Ukonga nitawapigania kuhakikisha soko linajengwa kwa ajili ya biashara zenu," alisema Shingo.
Alisema kuwa wafanyabiashara hao kuendelea kufanya biashara zao pembezoni mwa barabara ni athari kubwa katika maisha yao.
Mbunge huyo alisema soko hilo litakalojengwa litawezesha kutambulika kuwa katika mfumo rasmi wa kufanyabiashara zao.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya Ilala, Mpogolo alisema imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa soko kwa wafanyabiashara wadogo wadogo wa Gongo la Mboto.
Mpogolo alisema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri nchini kutenga fedha kwa ajili ya kujenga masoko kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo wadogo.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kwa kuzingatia hilo, wanatarajia kujenga soko la kisasa kwa ajili ya wamachinga wa Gongo la Mboto.
Pia, Mpogolo aliwaomba wafanyabiashara wadogo wadogo kutopanga bidhaa zao barabarani ili kuepuka ajali ambazo zinaweza kutokea.








No comments:
Post a Comment