..................................................
Na Dotto Mwaibale Dodoma
Mgonjwa
Ester John Furaha (32) hali yake ni tete na hajiwezi kwa lolote baada ya kupata
rufaa kwenda Taasisi ya Kansa Ocean Road Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya
matibabu amezuiliwa kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa Jijini Dodoma mpaka
atakapolipa deni la Sh. 1,175,000 anazodaiwa baada ya kupatiwa matibabu.
Rufaa hiyo
alipewa Machi 18, 2026 lakini kutokana na deni hilo kitengo cha huduma za ustawi
wa jamii katika hospitali hiyo kimemzuia asiondoke mpaka atakapolipa deni hilo.
Mgonjwa huyo
mwenye namba ya matibabu DM-00280606 yupo wodi namba mbili chumba namba 8 akiwa
na mdogo wake Celina John Furaha anayemuuguza huku wakiishi kwa kutegemea
kupewa msaada wa chakula na mahitaji mengine na ndugu za wagonjwa wengine wanapofika kuwaona jamaa zao waliolazwa
hospitalini hapo.
Akizungumzia
hali waliyo nayo Celina amesema hajui cha kufanya, dada yake hali yake ni mbaya
na hawajui deni hilo watalilipaje kwani hawana fedha na hata jinsi ya kwenda
Dar es Salaam kupata matibabu.
“Tumekuwepo
hapa hospitali kwa zaidi ya miezi mitatu tukitokea Hosptali ya Makiungu wilayani
Ikungi mkoani Singida ambapo walibaini kuwa anasumbuliwa ugonjwa wa kansa na
tumelipia matibabu yake zaidi ya Sh. Milioni 3.2 tumeishiwa na hatuna msaada
wowote,” alisema Celina huku akiwa na huzuni.
Celina alisema
Machi 18, 2026 majira ya saa 10 jioni alikwenda ofisi ya huduma ya ustawi wa jamii hospitalini hapo ambapo aliambiwa mgonjwa hataruhusiwa kuondoka mpaka alipe
deni hilo na kuwa wapo wodini na dada yake hapati matibabu yoyote na hali yake
ni mbaya kwani anatapika na hawezi hata
kuinuka zaidi ya kulala wakati wote.
Akifafanua
kuhusu deni hilo alisema Afisa mmoja wa kitengo hicho cha huduma ya ustawi wa
jamii alimuandikia kuwa matibabu yake gharama ilikuwa ni Sh.685,000, gharama za kitanda
Sh.490,000 na Sh.70,000 jumla kuu ikiwa ni Sh.1,175,000.
Jitihada za
kumpata Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), Prof. Abel
Makubi ili kuzungumzia suala hilo hazikuweza kuzaa matunda.
Hata hivyo Afisa
Habari wa Hospitali hiyo, Ludovick Kazoka akizungumzia suala hilo alisema
kuhusu deni hilo mgonjwa huyo anapaswa kwenda ofisi ya huduma ya ustawi
wa Jamii ambao watafanya tathimini na kama itaonesha kweli hawezi kulipa wataona namna ya kufanya na kuwa huo ndiyo utaratibu uliopo.
Mwaka jana katika Uzinduzi wa kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM), kitaifa uliofanyika Agosti 28, 2025, katika Viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe jijini Dar es Salaam.
, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye alikuwa mgombea nafasi ya urais wakati akihutubia moja ya ahadi yake ilikuwa ni kupiga marufuku kuzuia miili ya marehemu ambayo ilikuwa ikizuiliwa kwa kushindwa kuilipia katika hospitali mbalimbali lakini kwa wagonjwa kama Ester Furaha inapaswa pia kuwekwa muongozo wa wazi ili kuondoa hali hiyo ya kuzuiliwa wakati alipaswa kukimbizwa hospitalini alikopewa rufaa jambo litakalosaidia kuokoa maisha yake badala ya kumzuia wodini bila ya kumpatia matibabu na pengine kusababisha kifo kwa mgonjwa husika.
Taarifa hii imeandaliwa na Dotto Mwaibale simu namba 0754362990.








No comments:
Post a Comment