MISANGA: SWADAKA NI NGAO NA KINGA YA MADHAMBI KWA MWENYE KUITOA KWA AJILI YA ALLAH - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Saturday, March 14, 2026

MISANGA: SWADAKA NI NGAO NA KINGA YA MADHAMBI KWA MWENYE KUITOA KWA AJILI YA ALLAH

Mwenyekiti wa Ramadhan Charity Programme 2026, Ahmed Misanga, akiongoza dua wakati akikabidhi sadaka ya iftar katika kituo cha Jaamiul-Furouq, kilichopo wilayani Manyoni Mkoa wa Singida Machi 14, 2026.

Na Mwandishi Wetu, Singida

MWENYEKITI wa Taasisi ya Ramadhan Charity Programme 2026  Ahmed Misanga amewataka Watanzania kutumia mwezi mtukufu wa Ramadhani kuwa wamoja, kusaidiana na kufanya kazi kwa pamoja katika kuwasaidia watu wenye uhitaji katika jamii.

Misanga aliyasema hayo wakati akikabidhi sadaka ya iftar katika kituo cha Jaamiul-Furouq, kilichopo wilayani Manyoni Mkoa wa Singida.

Alisema kuwa kutoa sadaka kunahitaji moyo wa kusaidia na siyo lazima mtu awe tajiri na kuongeza kuwa watu wenye uwezo wajitokeze kushirikiana katika kuwasaidia wenye uhitaji, kwani wapo wengi katika vituo vya kulea watoto yatima na watu wasiojiweza.

" Sadaka na kutumia mali katika njia ya Allah ni miongoni mwa matendo mema na bora, kwani hufuta madhambi na makosa kama vile maji yanavyozima moto," alisema Misanga.

Katika hatua nyingine, amewahimiza vijana kusoma kwa bidii ili wawe watu wema katika jamii na baadaye waweze kusaidia wengine wenye uhitaji.

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa kituo hicho Nawawi Salimu, ameishukuru Taasisi ya Ramadhan Charity Programme 2026 kwa kuendelea kutoa sadaka ya iftar katika kituo hicho kwa mwaka wa tatu mfululizo.

Amesema msaada huo umekuwa na mchango mkubwa kwa wanafunzi wa kituo hicho, na amewahimiza wadau hao kuendelea na moyo huo wa kusaidia jamii, bila kuishia katika kituo hicho pekee bali kufikia pia vituo vingine vyenye uhitaji.

“Mimi pamoja na wanafunzi wangu hatuna cha kuwalipa, lakini tunaamini Mwenyezi Mungu ndiye atakayewalipa kwa wema huu mlioufanya,” amesema Nawawi.

Aidha, amewaomba wadau wengine kuiga mfano wa Ramadhan Charity Programme 2026 kwa kuwafikia walengwa na kutoa sadaka katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhani, kwani bado kuna uhitaji mkubwa.

Ameongeza kuwa katika kituo hicho kuna zaidi ya watoto 100 wanaopata elimu ya dini na malezi ya mazingira, huku akisema milango ya msaada bado ipo wazi kwa yeyote mwenye nia ya kusaidia.

Vitu mbalimbali vilivyotolewa katika kituo hicho.
Msaada huo ukitolewa.

 Msaada huo ukipokelewa.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad