SERIKALI YAIMARISHA UPATIKANAJI WA MAFUTA YA PETROLI NCHINI MALAWI - SINGIDANI BLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Wednesday, 25 March 2026

SERIKALI YAIMARISHA UPATIKANAJI WA MAFUTA YA PETROLI NCHINI MALAWI

Waziri wa Nishati na Madini wa Malawi, Mhe. Dkt. Jean Mathanga (katikati) akimsikiliza Meneja wa Mafuta wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Mhandisi Yona Malago (kushoto) akifafanua kuhusu namna flowmeters zinavyosaidia kujua kiasi cha mafuta ya petroli kilichoingia,wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua miundombinu ya mafuta kwenye  Kituo cha Kurasini Oil Jet (KOJ-1), kilichopo katika Bandari ya Dar es Salaam leo Machi 24,2026 jijini Dar es Salaam.. Wengine pichani ni ujumbe ulioambatana na Waziri  kutoka nchini Malawi pamoja na na baadhi ya watumishi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA).
Waziri wa Nishati na Madini wa Malawi, Mhe. Dkt. Jean Mathanga (katikati) akiwa ameongozana na Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA), Mhandisi Bruno Tarimo (kushoto) kukagua miundombinu ya mafuta kwenye  Kituo cha Kurasini Oil Jet (KOJ-1), kilichopo katika Bandari ya Dar es Salaam leo Machi 24,2026 jijini Dar es Salaam. Wengine pichani ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini wa Malawi, Mhandisi Emmanuel Matapa na ujumbe ulioambatana na Waziri kutoka nchini Malawi na baadhi ya watumishi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA).
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA), Mhandisi Bruno Tarimo akifafanua kuhusu  Mfumo wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja unavyofanya kazi wakati wa ziara ya kikazi ya aziri wa Nishati na Madini wa Malawi, Mhe. Dkt. Jean Mathanga (kushoto kwake) iliyofanyika katika Kituo cha Kurasini Oil Jet (KOJ-1), kilichopo katika Bandari ya Dar es Salaam leo Machi 24,2026 jijini Dar es Salaam. Wengine pichani ni ujumbe ulioambatana na Waziri kutoka nchini Malawi pamoja na na baadhi ya watumishi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA).
Muonekano wa flowmeters zinazotumika kupima kiasi cha bidhaa za mafuta ya petroli katika Kituo cha Kurasini Oil Jet (KOJ-1), kilichopo katika Bandari ya Dar es Salaam leo Machi 24,2026 jijini Dar es Salaam.
Muonekano wa meli ya mafuta ya petroli ikipakua mafuta katika Kituo cha Kurasini Oil Jet (KOJ-1), kilichopo kwenye Bandari ya Dar es Salaam leo Machi 24,2026 jijini Dar es Salaam.
--------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Serikali kupitia Bandari ya Dar es Salaam imeendelea kuwa nguzo muhimu ya upatikanaji wa mafuta kwa nchi jirani ya Malawi, hatua inayochochea shughuli za kiuchumi na kuboresha maisha ya wananchi wa nchi hizo mbili.


Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua miundombinu ya mafuta katika Kituo cha Kurasini Oil Jet (KOJ-1), kilichopo katika Bandari ya Dar es Salaam, Waziri wa Nishati na Madini wa Malawi, Mhe. Dkt. Jean Mathanga, aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa mchango wake mkubwa katika kuwezesha mtiririko wa mafuta kwenda nchini Malawi.


Alisema kuwa kutokana na Malawi kutokuwa na bandari, nchi hiyo inategemea kwa kiasi kikubwa miundombinu ya nchi jirani, hususan Tanzania, katika kuhakikisha upatikanaji wa mafuta unaendelea kuwa wa uhakika.


Alibainisha kuwa ziara hiyo imelenga kujionea kwa vitendo namna mafuta yanavyopokelewa na kusimamiwa bandarini ili kuboresha mipango ya ununuzi na usambazaji wa mafuta nchini Malawi. 


Aidha, alieleza kuridhishwa na mifumo na taratibu alizoziona, akisisitiza kuwa uzoefu huo utasaidia nchi yake kupanga kwa ufanisi zaidi mahitaji ya mafuta.


Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA), ambaye ni Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Petroli PBPA, Mhandisi Bruno Tarimo, alifafanua kuwa sehemu kubwa ya mafuta yanayoingia Malawi hupitia Tanzania kupitia Mfumo wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (BPS), huku wakati mwingine nchi hiyo ikiagiza moja kwa moja kutoka kwa wazabuni wake.


“Ugeni huu umepata nafasi ya kujionea hatua zote za upokeaji wa mafuta, kuanzia meli zinapowasili, upimaji wa ubora na ujazo kupitia mifumo ya kisasa, hadi usimamizi wa wataalamu wetu,” alisema Tarimo.


Akihitimisha, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Bw. Mussa Biboze, alisema kuwa uelewa walioupata wageni hao utaongeza imani kwa Malawi na nchi nyingine kutumia bandari hiyo kama lango kuu la kuingiza mafuta, jambo litakaloongeza ufanisi wa biashara na kukuza uchumi wa ukanda.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad