Sheikh wa Mkoa wa Singida, Issa Nassoro, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mabadiliko ya viongozi baada ya Baraza la Ulamaa Taifa kutengua uteuzi wao. Kushoto ni Kadhi Mpya wa Mkoa wa Singida, Sheikh Mbaraka Esya na Katibu wa Baraza Kuu la Kiislamu (BAKWATA), Mkoa wa Singida, Omari Ally Muna.
................................
Na Dotto Mwaibale, Singida
BARAZA la Ulamaa Taifa chini ya Mwenyekiti wake, Mufti wa
Tanzania, Sheikh Dk. Abubakar bin Zubeir, limetengua uteuzi wa baadhi ya
masheikh katika Mkoa wa Singida akiwamo Kadhi wa Mkoa, kufuatia viongozi hao
kufanya kikao na kutangaza kumvua madaraka Katibu wa Baraza la Waislamu
Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Singida kinyume cha katiba na kanuni za taasisi
hiyo.
Hatua hiyo imechukuliwa baada ya Baraza la Ulamaa Taifa
kufanya kikao chake kilichofanyika Machi 4, 2026, ambapo pamoja na mambo
mengine kilijadili mgogoro uliojitokeza ndani ya Baraza la Masheikh Mkoa wa
Singida uliosababisha baadhi ya viongozi kuchukua maamuzi yaliyodaiwa kwenda
kinyume na taratibu za kikatiba za BAKWATA.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi Sheikh wa Mkoa wa
Singida, Issa Nassoro, amesema Baraza la Ulamaa Taifa limeamua kutengua uteuzi
wa viongozi hao ili kurejesha utulivu, umoja na ufuataji wa katiba ndani ya
taasisi hiyo ya Kiislamu.
Amesema miongoni mwa waliotenguliwa ni Kadhi wa Mkoa wa
Singida, Sheikh Ramadhani Kaoja, ambaye nafasi yake sasa imechukuliwa na Sheikh Mbaraka Ally Esya aliyeteuliwa kushika wadhifa huo.
Aidha, Nassoro amesema Mufti wa Tanzania amemteua Sheikh
Isihaka Isangu kuwa Katibu wa Kadhi wa Mkoa wa Singida akichukua nafasi ya
Sheikh Issa Takaza, ambaye uteuzi wake pia umetenguliwa na Baraza la Ulamaa
Taifa kutokana na mgogoro huo.
Katika hatua nyingine, Mufti Dk. Abubakar bin Zubeir
ametengua pia uteuzi wa Sheikh Said Mang’ola na nafasi yake imechukuliwa na
Sheikh Salum Ngaa ambaye ameteuliwa kuwa Kaimu Katibu wa Baraza la Masheikh
Mkoa wa Singida.
Pamoja na mabadiliko hayo, viongozi wengine waliotenguliwa
ni pamoja na Omary Mughenyi aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya BAKWATA Mkoa
wa Singida na Sheikh Abdu Shekitila aliyekuwa Mjumbe wa Baraza la Masheikh Mkoa
wa Singida.
Sheikh Nassoro alieleza kuwa pamoja na kutengua uteuzi wa
viongozi hao, Baraza la Ulamaa Taifa pia limetengua maamuzi yote yaliyofanywa
katika mkutano mkuu wa Baraza la Masheikh Mkoa wa Singida ambao ulifanyika bila
kufuata utaratibu uliowekwa na katiba ya BAKWATA.
Alisema uamuzi huo umechukuliwa ili kulinda misingi ya katiba, nidhamu ya uongozi na kuhakikisha taasisi hiyo inaendelea kufanya kazi kwa umoja na mshikamano kwa maslahi ya waumini wa dini ya Kiislamu.
Katika maelezo yake, Sheikh Nassoro aliwataka viongozi wote
walioteuliwa kushika nafasi mbalimbali ndani ya BAKWATA Mkoa wa Singida kufanya
kazi kwa kuzingatia katiba, kanuni na taratibu za taasisi hiyo ili kuepusha
migogoro isiyo ya lazima.
Pia aliwahimiza waumini wa dini ya Kiislamu mkoani humo kuendelea kudumisha amani, umoja na mshikamano huku wakiiunga mkono uongozi uliopo ili kuendeleza shughuli za dini na maendeleo ya jamii kwa ujumla.
Kadhi mpya wa Mkoa wa Singida, Sheikh Mbaraka Ally Esya







No comments:
Post a Comment