VIONGOZI NA WANANCHI BWAWANI KIJITONYAMA WAKUTANA KATIKA FUTARI - SINGIDANI BLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Monday, 16 March 2026

VIONGOZI NA WANANCHI BWAWANI KIJITONYAMA WAKUTANA KATIKA FUTARI

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tawi la Bwawani, Kijitonyama jijini Dar es Salaam, umejumuika pamoja na viongozi mbalimbali pamoja na wananchi katika futari maalum iliyoandaliwa na uongozi wa tawi hilo ikiwa ni sehemu ya kudumisha mshikamano na kuimarisha mahusiano katika jamii.

Akizungumza wakati wa futari hiyo iliyofanyika Machi 14, Mwenyekiti wa CCM Tawi la Bwawani, Twaha John, alisisitiza umuhimu wa kudumisha amani na upendo miongoni mwa wananchi, akieleza kuwa mazingira ya amani huchangia maendeleo na utekelezaji mzuri wa shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi.

“Tuendelee kudumisha amani na upendo baina yetu, kwani katika mazingira ya amani shughuli zetu zitafanyika vizuri. Pia nawaomba vijana wenzangu tuchangamkie fursa zilizopo na kutumia mikopo inayotolewa na halmashauri zetu ili kujikwamua kiuchumi,” alisema Twaha.

Kwa upande wake, mgeni waalikwa katika futari hiyo, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Kinondoni, Mussa Omary, alimpongeza Mwenyekiti wa CCM Bwawani, Twaha John, kwa uongozi wake mzuri na uwezo wa kuratibu shughuli za chama kwa ushirikiano na viongozi wengine wa tawi hilo.

Alisema ushirikiano na mshikamano wa viongozi wa CCM katika tawi hilo umewezesha kufanikisha shughuli mbalimbali za kijamii, ikiwemo kuandaa futari hiyo inayowakutanisha viongozi na wananchi.

Futari hiyo pia ilihudhuriwa na Diwani wa Kata ya Kijitonyama ambaye pia ni Naibu Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Amani Balande, pamoja na Mwenyekiti wa CCM Kata ya Kijitonyama, Ismail Mwenda, wajumbe wa Kamati ya Siasa na wajumbe wa Halmashauri ya Tawi la Bwawani.

Aidha, wadau mbalimbali pamoja na wananchi wa eneo la Kijitonyama walijitokeza kwa wingi kushiriki futari hiyo, ambayo imeelezwa kuwa ni utaratibu wa kila mwaka unaoandaliwa na Mwenyekiti Twaha John kwa kushirikiana na Kamati ya Siasa ya tawi hilo kwa lengo la kuimarisha mshikamano na upendo katika jamii.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad