WAKUU WA NCHI EAC WACHUKUA HATUA MADHUBUTI KUIMARISHA MTANGAMANO - SINGIDANI BLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Sunday, 8 March 2026

WAKUU WA NCHI EAC WACHUKUA HATUA MADHUBUTI KUIMARISHA MTANGAMANO

• Waweka mikakati kabambe kutatua changamoto na kuongeza kasi ya maendeleo ya Jumuiya.

Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wameazimia kuendelea kuimarisha mtangamano wa Jumuiya hiyo kwa kuweka mikakati mipya inayolenga kutoa suluhisho dhidi ya changamoto mbalimbali zinazoikabili Jumuiya kwa sasa, ikiwa ni pamoja na kuimarisha uwezo wa kifedha wa Sekretariati na taasisi zake, kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu shughuli na faida za Jumuiya, kuondoa vikwazo vya biashara visivyo vya kikodi (NTB’s) pamoja na kuongeza zaidi ushiriki wa wanawake na vijana katika shughuli za kiuchumi ili kuongeza kasi ya maendeleo katika Jumuiya.

Maazimio hayo yamefikiwa leo, tarehe 7 Machi 2026, katika Mkutano wa Kawaida wa 25 wa Wakuu wa Nchi wa EAC, uliofanyika katika Makao Makuu ya Jumuiya hiyo jijini Arusha, uliolenga kujadili kuhusu mustakabali mpya wa mtangamano na hatua za kuimarisha utekelezaji wa ajenda za maendeleo ya Jumuiya.

Awali akizungumza, Mwenyekiti wa mkutano huo aliyemaliza muda wake Mheshimiwa Dkt. Willian Samoei Ruto na Rais wa Jamhuri ya Kenya ameeleza kuhusu mafanikio yaliyofikiwa na Jumuiya katika kipindi chake mwaka mmoja wa uenyekiti, akitaja kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa miundombinu ya barabara inayounganisha nchi wanachama, kuongezeka kwa mauzo ya bidhaa nje ya Jumuiya, kupungua kwa NTB’s, pamoja kuendelea kuimarika kwa amani na usalama katika Jumuiya.

Aidha, Rais Ruto ameyataja maamuzi yaliyochukuliwa na mkutano huo kuwa ni pamoja na kukubaliana na mapendekezo ya kanuni mpya itakayotumiwa na Nchi wanachama kuchangia michango ya Jumuiya itakayoanza kutumika kuanzia Julai 2026, Wabunge wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) kulipwa mishahara yao na Bunge la Nchi Mwanachama husika, Wafanyakazi wa Sekretariati ya EAC kulipwa malimbikizo ya mishahara yao, maamuzi ya Jumuiya kufikiwa kwa kutegemea akidi ya asilimia 65 ya uwakilishi, uteuzi wa majaji, pamoja na Nchi wanachama kukosa nafasi ya kunufaika na baadhi ya fursa endapo haijakamilisha matakwa muhimu ya Mkataba wa Uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (Protocol for the Establishment of East African Community) ikiwemo nafasi za ajira.

Viongozi hao pia wameelekeza kufutwa kwa malimbikizo ya madeni ya muda mrefu ya michango wanayodaiwa baadhi ya nchi wanachama kwa asilimia 50 na kukubalia kuwa kiasi kinachosalia cha asilimia 50 kilipwe ndani ya miaka 2 kuanzia sasa ikiwa ni juhudi za kuhakikisha Sekretatriati na Taasisi zake zinapata uwezo wa kifedha wa kutosha kutekeleza majukumu yao. 

Katika hatua nyingine mkutano huo umemteua Balozi Stephen Patrick Mbundi kuwa Katibu Mkuu Mpya wa Sekretaraiati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, akichukua nafasi ya Bi. Veronica Nduva aliyemaliza muda wake wa kuhudumu katika nafasi hiyo.

Vilevile Wakuu hao wamemteua Mhe. Yoweri Kaguta Museveni wa Jamhuri ya Uganda kuwa Mwenyekiti mpya wa Jumuiya hiyo akipokea kijiti hicho kutoka kwa Rais Ruto wa Kenya aliyeshika nafasi hiyo tokea mwezi Novemba 2024.

Wakuu wa Nchi walioshiriki mkutano huo ni mwenyeji wake Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni Rais wa Uganda, Mhe. Dkt. Willian Samoei Ruto Rais wa Kenya, Mhe. Évariste Ndayishimiye Rais wa Burundi na Mhe. Hassan Sheikh Mahamud Rais wa Somalia. Wengine ni Waziri Mkuu wa Rwanda Mhe. Justin Nsengiyumva kwa niaba ya Rais Mhe. Paul Kagame, Mhe. Balozi Monday Semaya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Sudani Kusini akimwakilisha Rais Mhe. Salva Küir Mayardit na Mhe. Didier Mazenga Mukanzu Waziri wa Ushirikiano wa Kikanda wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa niaba ya Rais Mhe. Félix Antoine Tshisekedi Tshilombo.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad