WAZIRI WA FEDHA AIAGIZA TUME YA PAMOJA YA FEDHA KUTOA USHIRIKIANO. - SINGIDANI BLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Friday, 20 March 2026

WAZIRI WA FEDHA AIAGIZA TUME YA PAMOJA YA FEDHA KUTOA USHIRIKIANO.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akizungumza wakati wa kikao na Uongozi wa Tume ya Pamoja ya Fedha, ukiongozwa na Katibu wa Tume hiyo, Bw. Ernest Mchanga, aliyeambatana na Katibu Msaidizi, Idara ya Huduma za Kiufundi wa Tume hiyo, Bw. Jonas Nduttu, walipomtembelea Mhe, Balozi Omar (Mb), ofisini kwake, Wizara ya Fedha, Treasury Square, Dodoma.
--------------------------------------------

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), ameiagiza Tume ya Pamoja ya Fedha (JFC), kushirikiana na Serikali kuchambua na kutoa mapendekezo ya namna bora ya kuboresha huduma kwa Watanzania kupitia mapato ya Serikali za Mitaa pamoja na uwezeshaji unaofanywa na Serikali Kuu kwenda Serikali za Mitaa.


Mhe. Balozi ametoa agizo hilo jijini Dodoma, alipokutana na kufanya mazungumzo na Uongozi wa Tume ya Pamoja ya Fedha, ukiongozwa na Katibu wa Tume hiyo, Bw. Ernest Mchanga, walipomtembelea ofisini kwake Wizara ya Fedha, Treasury Square jijini Dodoma, kwa ajili ya kujitambulisha.


Mhe. Balozi Omar alibainisha kuwa, pamoja na majukumu mengine ya kimuungano, Tume hiyo inapaswa kufanyia kazi masuala mengine ya kifedha hususani yale yasiyokuwa ya muungano ili kuboresha zaidi huduma za kijamii na kiuchumi.


“Kwa kutumia uzoefu wa Kimataifa tumewaagiza kufanya uchambuzi, tutakuja kukaa nao tutoe mapendekezo ya namna bora ambayo Serikali itaweza kuboresha huduma kwa Watanzania wote”. alibainisha Mhe. Balozi Omar (Mb).


Kwa upande wake Katibu wa Tume ya Pamoja ya Fedha, Bw. Ernest Mchanga, alisema Taasisi hiyo itaendelea kushauri Serikali mbili za Jamhuri ya Muungano ya Tanzania kuhusu Mfumo wa Fedha hususani katika mapato, matumizi pamoja na fedha nyingine zitakazowekwa na pande mbili za Muungano katika Akaunti ya Fedha ya Pamoja.


Kikao hicho pia kilihudhuriwa na baadhi ya Viongozi wa Wizara ya Fedha, akiwemo, Kamishina Msaidizi, Idara ya Sera, Bw. Wiliam Mhoja, pamoja na Kamishna Msaidizi, Idara ya Madeni, Bw. Omary Khama.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad