Na Maelezo Zanzibar 24.04.2026
Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe, Balozi, Dkt. Emmanuel John Nchimbi amesema ujenzi wa maabara ya sayansi na Skuli ya kilimo utawezesha kuleta mageuzi makubwa katika kujenga misingi imara ya maendeleo ya teknolojia, ujuzi na uchumi katika jamii.
Ameyasema hayo katika hafla ya uwekaji wa Jiwe la msingi majengo ya Maabara za Sayansi na Skuli ya Kilimo ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar SUZA ikiwa ni miongoni mwa Shamrashamra za kuadhimisha sherehe za miaka 62 ya Muungano wa Tanyika na Zanzibar amesema ujenzi huo unaonesha dhamira ya Serikali zote mbili za kuleta mageuzi ya kiuchumi katika sekta ya elimu ya juu.
Aidha Dkt. Nchimbi amesema kukamilika kwa majengo hayo yatasaidia kuleta maendeleo mbali mbali ikiwemo kutengeneza fursa za ajira, kuongeza uelewa wa sayansi na teknolojia pamoja na kukuza uchumi wa buluu kwa kuongeza tija katika kilimo.
“Kupitia mradi huu unachangia moja kwa moja sekta ya kilimo katika kuchochea jamii na kukuza uzalishaji” ameeleza.
Amesema majengo hayo ni msingi wa elimu ya juu katika kukuza utafiti, ubunifu na kuweka msingi imara ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia katika kuchochea maendeleo kiuchumi na kijamii.
“Tunapoweka jiwe la msingi leo tunaangazia sekta ya maendeleo ya Muungano wetu kwa kuendeleza amani umoja na mshikamano kwa pande zote mbili kwani ndio nguzo imara ya maendeleo ya nchi yetu” amasema Dkt. Nchimbi.
Vile vile ameeleza mradi huo ukikamilika utapelekea kujenga jamii iliyokamilika na kupeleka mbele sekta ya elimu hivyo ni vyema vijana kuulinda Muungano kwa kudumisha amani pamoja na kuimarisha sekta ya elimu kupitia Serikali zote mbili.
Hata hivyo amewataka wakandarasi na washauri elekezi wa mradi huo kuhakikisha jitihada inaongezeka na kukamilisha mradi ndani ya muda ili kufanikisha maendeleo yaliyo kusudiwa pamoja na kuwawezesha vijana kuendelea kujipatia elimu iliyobora.
Nae Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) Prof. Abdi Talib Abdalla akitoa maelezo ya ujenzi wa mradi huo amesema mradi huo umeleta mabadiliko katika chuo hicho ya kuhakikisha mpango wa kidijitali unaendelezwa ili kuenda sambamba na mabadiliko ya Dunia.
Aidha amesema majengo hayo yakikamilika yatachukua wanafunzi zaidi ya Elfu moja miasita kwa mkondo moja hiyo yote ni kuonyesha wazi dhamira ya Serikali ya kuhakikisha elimu ya juu inazidi kukua hapa Zanzibar.
Prof. Abdi amefahamisha kua mradi huo umeimarisha matumizi ya kidijitali katika kuendeleza Sayansi na teknolojia pamoja na kuendeleza mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia sambamba na kuahidi kuitunza miundombinu hiyo kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Ujenzi wa Mradi huo umeanza mwaka 2024 na unatarajiwa kukamilika Disemba 2026 ambapo ujenzi huo unatarajiwa kugharimu zaidi ya Bilioni 32.115.











No comments:
Post a Comment