𝐒𝐄𝐑𝐈𝐊𝐀𝐋𝐈 𝐘𝐀𝐒𝐀𝐈𝐍𝐈 𝐌𝐊𝐀𝐓𝐀𝐁𝐀 𝐖𝐀 𝐃𝐎𝐋𝐀 𝐙𝐀 𝐌𝐀𝐑𝐄𝐊𝐀𝐍𝐈 𝐁𝐈.𝟏.𝟐𝟖 𝐙𝐀 𝐔𝐉𝐄𝐍𝐙𝐈 𝐖𝐀 𝐒𝐆𝐑 𝐌𝐀𝐊𝐔𝐓𝐔𝐏𝐎𝐑𝐀 𝐇𝐀𝐃𝐈 𝐈𝐒𝐀𝐊𝐀. - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Tuesday, April 28, 2026

𝐒𝐄𝐑𝐈𝐊𝐀𝐋𝐈 𝐘𝐀𝐒𝐀𝐈𝐍𝐈 𝐌𝐊𝐀𝐓𝐀𝐁𝐀 𝐖𝐀 𝐃𝐎𝐋𝐀 𝐙𝐀 𝐌𝐀𝐑𝐄𝐊𝐀𝐍𝐈 𝐁𝐈.𝟏.𝟐𝟖 𝐙𝐀 𝐔𝐉𝐄𝐍𝐙𝐈 𝐖𝐀 𝐒𝐆𝐑 𝐌𝐀𝐊𝐔𝐓𝐔𝐏𝐎𝐑𝐀 𝐇𝐀𝐃𝐈 𝐈𝐒𝐀𝐊𝐀.

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Natu El-maamry Mwamba na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Standard Chartered, Bw. Herman Kasekende, wakisaini Mkataba wa kugharamia ukamilishaji wa Reli ya Kisasa (Standard Gauge -SGR), kipande cha tatu (loti 3) na cha nne (loti 4) kutoka Makutupora ya mkoani Singida hadi Isaka, yenye thamani ya takriban dola za Marekani bilioni 1.277, katika hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kambarage, Treasury Square, jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Natu El-maamry Mwamba na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Standard Chartered, Bw. Herman Kasekende, wakibadilishana Mkataba wa kugharamia ukamilishaji wa Reli ya Kisasa (Standard Gauge -SGR), kipande cha tatu (loti 3) na cha nne (loti 4) kutoka Makutupora ya mkoani Singida hadi Isaka, yenye thamani ya takriban dola za Marekani bilioni 1.277, katika hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kambarage, Treasury Square, jijini Dodoma.
Meza Kuu ikiongozwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb), Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mhe. Sulemani Kakoso (Mb), Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba na Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Prof. Godius Walter Kahyarara, wakiwa katika picha ya pamoja na mabalozi wa Sweden, Italy na Poland baada ya hafla ya utiaji saini wa Mkataba wa kugharamia ukamilishaji wa Reli ya Kisasa (Standard Gauge -SGR), kipande cha tatu (loti 3) na cha nne (loti 4) kutoka Makutupora ya mkoani Singida hadi Isaka, yenye thamani ya takriban dola za Marekani bilioni 1.277, katika hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kambarage, Treasury Square, jijini Dodoma.
-----------------------

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesaini mkataba wa kukamilisha mpango wa ufadhili wa pamoja wenye thamani ya takribani dola za Marekani bilioni 1.277 kwa ajili ya kuendeleza mtandao wa Reli ya Kisasa (Standard Gauge -SGR), kipande cha tatu (loti 3) na cha nne (loti 4) kutoka Makutupora ya mkoani Singida hadi Isaka.

 

Hafla ya utiaji saini wa mkataba huo umefanyika jijini Dodoma na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba kwa upande wa Serikali na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Standard Chartered, Bw. Herman Kasekende.

 

‎Akizungumza wakati wa utiaji saini wa mkataba huo, Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi, Khamis Musa Omar (Mb) amesema fedha hizo ambazo ni sehemu ya jumla ya dola za Marekani bilioni 2.33 za utekelezaji wa mradi huo, ni mpango wa ufadhili wa pamoja kutoka Italia (SACE), Sweden (EKN) na Poland (KUKE), kupitia taasisi zao za dhamana za mikopo ya mauzo ya nje (Export Credit Agencies) za SACE, EKN na KUKE, kwa kuratibiwa na Benki ya Standard Chartered.

 

‎"Uwekezaji huu unaendeleza moja ya miradi ya kimkakati katika historia ya taifa letu, uliolenga kuunganisha Bandari ya Dar es Salaam na Kanda ya Ziwa pamoja na nchi jirani, huku ukiimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha biashara na usafirishaji katika ukanda huu", alisema Balozi Omar.

 

‎Alieleza kuwa mradi huo siyo tu uwekezaji mkubwa wa miundombinu, bali ni mradi wa kitaifa wa mfano unaoakisi dira ya muda mrefu ya maendeleo ya Tanzania na ni uwekezaji wa kimkakati wa Taifa, bali pia kama kichocheo kikuu cha kufanikisha malengo ya muda mrefu ya maendeleo.

 

Aidha, Mhe. Balozi Omar alisema kuwa mradi huo ukiendeshwa kikamilifu kwa nishati ya umeme, ni miongoni mwa njia za usafiri zenye ufanisi mkubwa wa matumizi ya nishati na uzalishaji mdogo wa hewa ukaa, hivyo kuiweka Tanzania mstari wa mbele katika kuelekea uchumi wa kaboni ndogo na unaostahimili mabadiliko ya tabianchi.

 

Naye Waziri wa Uchukizi, Mhe. Prof. Makame Mbarawa alisema kuwa Mradi wa SGR utakapokamilika utawawezesha kusafirisha hadi tani milioni 5 za mzigo kwa mwaka na kupunguza kwa kasi kubwa muda wa usafirishaji wa mizigo hali ambayo itaboresha usalama, ufanisi na uendelevu.

 

‘‘Mradi huu wa kimkakati tayari umeanza kuleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi na kijamii, ambapo huduma kati ya Dar es Salaam na Dodoma zimeshasafirisha takriban abiria milioni sita na tani 120,000 za mizigo pamoja na kupunguza muda wa kusafiri kutoka saa 12 hadi saa 3 pekee, huku ukichochea utunzaji wa mazingira kwa kupunguza matumizi ya mafuta kwa lita milioni 17 na kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa kwa zaidi ya asilimia 50’’, alifafanua Mhe. Mbarawa.

 

Alisema mkataba uliosainiwa utawawezesha kupanua reli hadi maeneo muhimu na kuiunganisha nchi za jirani kuimarisha biashara, kupunguza gharama za usafirishaji na kufungua fursa za kikanda.

 

Kwa upande wao Mabalozi wa nchi za Sweden, Mhe. Charlotta Marcias, Balozi wa Italia, Mhe. Giuseppe Sean Coppola na Mwakilishi wa Balozi wa Poland nchini, Bw. Sergiusz Wolski, wamesema kuwa wameridhishwa na uendelezaji wa mradi wa reli ya kisasa (SGR), na kueleza kuwa ni kielelezo cha uhusiano imara wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya Tanzania na nchi hizo ambapo mafanikio yaliyopatikana katika Loti ya 1 na 2 yamefungua milango ya ushirikiano mpana zaidi katika loti zinazofuata.

 

Walisisitiza kuwa kupitia taasisi zao za kifedha na mashirika ya mikopo, wataendelea kusaidia miradi mikubwa ya miundombinu inayozingatia uendelevu na viwango vya kimataifa huku wakibainisha kuwa ushirikiano huo utafungua milango kwa kampuni zaidi za Ulaya kuwekeza nchini na kuchangia ukuaji wa sekta binafsi pamoja na ajira.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad