𝐌𝐅𝐔𝐌𝐎 𝐖𝐀 𝐊𝐎𝐃𝐈 𝐘𝐀 𝐌𝐀𝐊𝐀𝐃𝐈𝐑𝐈𝐎 𝐊𝐔𝐂𝐇𝐎𝐂𝐇𝐄𝐀 𝐔𝐋𝐈𝐏𝐀𝐉𝐈 𝐊𝐎𝐃𝐈 𝐖𝐀 𝐇𝐈𝐀𝐑𝐈 - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Wednesday, 22 April 2026

𝐌𝐅𝐔𝐌𝐎 𝐖𝐀 𝐊𝐎𝐃𝐈 𝐘𝐀 𝐌𝐀𝐊𝐀𝐃𝐈𝐑𝐈𝐎 𝐊𝐔𝐂𝐇𝐎𝐂𝐇𝐄𝐀 𝐔𝐋𝐈𝐏𝐀𝐉𝐈 𝐊𝐎𝐃𝐈 𝐖𝐀 𝐇𝐈𝐀𝐑𝐈

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), akijibu swali la Mbunge wa Busokelo Mhe. Lutengano George Mwalwiba, aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kuweka vivutio maalum vya kikodi kwa Vijana wanaoanza biashara ili kuchochea ajira na kukuza uchum.
--------------------------------------------

Josephine Majura, WF, Dodoma

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), amesema kuwa Serikali inatekeleza mkakati wa Mfumo wa Kodi ya Makadirio (Presumptive Tax Scheme) ili kuwahamasisha walipakodi wadogo wasiokuwa na kumbukumbu sahihi za mapato kusajili biashara zao na kuanza kulipa kodi kwa hiari.

Ameyasema hayo bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu swali la Mbunge wa Busokelo Mhe. Lutengano Mwalwiba, aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kuweka vivutio maalum vya kikodi kwa Vijana wanaoanza biashara ili kuchochea ajira na kukuza uchumi.

Mhandisi Munde, alisema kuwa, mkakati huo unaolenga kuwasaidia walipakodi wadogo wasiokuwa na kumbukumbu sahihi za mapato au vitabu vya hesabu, kwa kuwa masharti yake ni mepesi na yanatabirika.

“Serikali pia imeanzisha utaratibu wa kipindi cha neema (grace period) kinachowaruhusu wafanyabiashara wapya kufanya biashara bila kulipa kodi kwa muda wa miezi sita tangu kuanza shughuli zao ili kutoa nafasi kwa wajasiriamali kukuza biashara zao na kujiimarisha kabla ya kuanza kulipa kodi”, alisema Mhandisi Munde.

Alisema kuwa Serikali inatambua umuhimu wa kutoa vivutio maalum vya kikodi kwa vijana ili kuchochea uanzishaji wa biashara na ajira, ikiwemo msamaha wa kodi na viwango pungufu, huku ikiendelea kufanya tathmini ya athari zake ili kuhakikisha usawa, ufanisi wa sera, na uendelevu wa mapato ya Serikali.

Kupitia Sheria ya Fedha ya Mwaka 2023 na Maboresho ya Mwaka 2024, Serikali pia imetoa ahirisho la kodi ya mapato (Corporate Income Tax) kwa kipindi cha miezi sita ya mwanzo kwa biashara mpya (start-ups), hatua inayolenga kusaidia biashara changa kukua na hatimaye kuwa na walipakodi wakubwa na endelevu.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad