𝐖𝐀𝐙𝐈𝐑𝐈 𝐌𝐊𝐄𝐍𝐃𝐀: 𝐒𝐄𝐊𝐓𝐀 𝐘𝐀 𝐄𝐋𝐈𝐌𝐔 𝐍𝐈 𝐌𝐇𝐈𝐌𝐈𝐋𝐈 𝐖𝐀 𝐌𝐀𝐄𝐍𝐃𝐄𝐋𝐄𝐎 𝐘𝐀 𝐍𝐂𝐇𝐈 - SINGIDANIBLOG

Habari za Hivi Punde

Post Top Ad

Thursday, April 30, 2026

𝐖𝐀𝐙𝐈𝐑𝐈 𝐌𝐊𝐄𝐍𝐃𝐀: 𝐒𝐄𝐊𝐓𝐀 𝐘𝐀 𝐄𝐋𝐈𝐌𝐔 𝐍𝐈 𝐌𝐇𝐈𝐌𝐈𝐋𝐈 𝐖𝐀 𝐌𝐀𝐄𝐍𝐃𝐄𝐋𝐄𝐎 𝐘𝐀 𝐍𝐂𝐇𝐈

Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda,akizungumza wakati akifungua  Mkutano wa 37 wa Baraza la Wafanyakazi wa wizara hiyo uliofanyika Aprili 29,2029 jijini Dodoma.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema utekelezaji wa mageuzi ya elimu unaoendelea nchini ni sehemu ya dhamira thabiti ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuhakikisha vijana wanapatiwa ujuzi, maarifa na uwezo unaowawezesha kushiriki kikamilifu katika uchumi wa taifa.

Ameyasema hayo   Aprili 29, 2026 katika Mkutano wa 37 wa Baraza la Wafanyakazi wa wizara hiyo, Prof. Mkenda amesisitiza kuwa sekta ya elimu inabeba wajibu mkubwa katika maendeleo ya nchi na kwamba, wajibu wa Wizara ni kuhakikisha mipango yote inatekelezwa kwa ufanisi na kwa kasi.

Waziri Mkenda ameongeza kuwa kuanzishwa kwa Wizara maalum ya maendeleo ya vijana ni uthibitisho wa umuhimu wa kundi hilo katika maendeleo ya taifa na kuwa elimu ya ufundi kupitia VETA, ni msingi wa kuwaandaa vijana kuzalisha na kushiriki katika uchumi wa kisasa. 

 "Utekelezaji wa elimu ya miaka 10 ya lazima na uimarishaji wa shule za Sekondari na shule za amali unatekelezwa kwa ushirikiano wa karibu na Ofisi ya Rais – TAMISEMI, na hata sekta binafsi hasa katika kuhakikisha upatikanaji wa shule karibu na makazi ya wananchi na ununuzi wa vifaa vya kisasa kwa ajili ya mafunzo ya ufundi."amesema Prof. Mkenda

 Katika kuhimiza ubunifu na uwajibikaji, Prof. Mkenda amewataka watumishi wa Wizara kuendeleza kasi ya utendaji na kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata taarifa kuhusu utekelezaji na mafanikio ya serikali katika maeneo ya sekta ya elimu, sayansi, teknolojia na ubunifu.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo,amesema Serikali inaendelea kuimarisha usimamizi wa ajira na rasilimaliwatu kwa kuzingatia malengo na maono ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan hususan katika utekelezaji wa Kifungu cha 73 cha Sheria ya Ajira kinachohusu uhusiano kazini.

Prof. Nombo amesema kuwa kupitia mkutano huo, wajumbe watapitia mpango na bajeti ya wizara pamoja na masuala ya utawala na usimamizi wa rasilimali watu pamoja na kujadili masuala mbalimbali yanayolenga kuboresha afya na usalama mahali pa kazi. Prof. Nombo amesisitiza kuwa mshikamano na ushirikiano miongoni mwa wafanyakazi ni nguzo muhimu ya kufanikisha ubora na uaminifu katika utendaji kazi, 

 "Dhamira ya Wizara ni kuona watumishi wanafanya kazi kwa bidii, kwa uadilifu na kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma ili kuendeleza mageuzi yanayoendelea katika elimu."amesema Prof. Nombo

 Aidha, amewashukuru wajumbe wa Baraza hilo kwa ushirikiano wao na amewataka kuendekeza juhudi za kuimarisha mifumo ya usimamizi ndani ya Wizara. 

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad