Na Mwandishi Maalumu - Dar es Salaam
Wananchi hususan wanamichezo wametakiwa kutambua mapema dalili hatarishi za magonjwa ya moyo ikiwemo maumivu ya kifua, kizunguzungu na kupoteza fahamu ili kuepuka madhara makubwa yakiwemo ya vifo vya ghafla wakati wa mazoezi au mashindano.
Wito huo umetolewa na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group ambaye pia ni Mratibu wa Magonjwa ya Moyo kwa Wanamichezo Eva Wakuganda wakati wa kambi maalumu ya siku tano ya upimaji iliyofanyika wakati wa mashindano ya Dkt. Mambosasa Cup yaliyomalizika hivi karibuni katika Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es Salaam (DPA).
Dkt. Wakuganda alisema zoezi hilo la upimaji wa afya limefanikiwa kuwafikia watu wengi kwa muda mfupi wakiwemo wanamichezo na Askari Polisi walioshiriki mashindano hayo.
“Leo ni siku ya tano hapa DPA ambapo tumekuwa tukihudumia wanamichezo na askari Polisi katika mashindano ya Dkt. Mambosasa Cup na tumepima jumla ya watu 482 walioshiriki michezo mbalimbali”, alisema Dkt. Eva.
Alieleza kuwa katika mashindano hayo wataalamu wa JKCI wametoa huduma za vipimo vya magonjwa ya moyo pamoja na elimu kuhusu magonjwa hayo kwa wanamichezo na askari Polisi ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza uelewa na namna ya kujikinga.
“Tumetoa elimu kuhusu dalili hatarishi kama maumivu ya kifua, kizunguzungu, kupoteza fahamu au uchovu uliopitiliza ambazo zinaweza kuashiria matatizo ya moyo wakati wa michezo”, alieleza Dkt. Eva.
Aliongeza kuwa ni muhimu kutambua dalili za magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo mapema ili kuzuia hatari ya matatizo ya moyo kwa wanamichezo.
“Tunashukuru uongozi wa chou hususan Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Dkt. Lazaro Mambosasa kwa kutukaribisha na kutuwezesha kutoa huduma hizi muhimu kwa askari na wanamichezo ili watambue afya zao mapema”, aliongeza.
Kwa upande wao wanafunzi wa chuo hicho walieleza kufurahishwa na huduma walizopata na kusema zimekuwa msaada mkubwa kwao katika mazingira ya mafunzo.
“Kwa kweli tumepata huduma nzuri sana ambazo mara nyingi ilikuwa ngumu kuzipata tukiwa nje ya chuo. Tunaiomba JKCI iendelee kuja tena kutoa huduma hizi kwa sababu watu wengi tumenufaika nazo”, alisema mwanafunzi wa Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es Salaam (DPA) Simula Maregesi.
“Tumepimwa vipimo mbalimbali ikiwemo moyo, presha na sukari, tumefurahi sana kupata huduma hii. Kujua afya zetu kutatusaidia kuendelea vizuri na mafunzo yetu hapa chuoni”, alisema Blandina Kasongwa.
Utoaji wa huduma hizo unaonesha umuhimu wa kuendelea kutoa elimu ya afya ya moyo kwa makundi maalumu hasa wanamichezo ili kupunguza hatari ya matukio ya dharura yanayoweza kuzuilika.











No comments:
Post a Comment