Na Mwandishi Maalumu – Njombe
30/04/2026 Serikali kupitia Wizara ya Kazi kwa kushirikiana na Wizara ya Afya imeahidi kuweka mikakati madhubuti ya kuiwezesha Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kufikisha huduma bingwa na bobezi za uchunguzi na matibabu ya moyo katika mikoa yote nchini hatua inayolenga kusogeza huduma hizo karibu zaidi na wananchi.
Hayo yamesema jana na Waziri wa Kazi Mhe. Deus Clement Sanga alipotembelea banda la JKCI katika maonesho ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi yanayoendelea katika viwanja vya Shule ya Msingi Mji Mwema mjini Njombe.
Akiwa katika banda hilo Waziri Sanga alipata fursa ya kujionea huduma mbalimbali zinazotolewa na wataalamu wa JKCI pamoja na mwitikio mkubwa wa wananchi waliojitokeza kupima afya zao.
Mhe. Sanga alisema mahitaji ya huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo yanaendelea kuongezeka kutokana na kasi ya magonjwa yasiyoambukiza hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kuhakikisha huduma hizo zinawafikia wananchi kwa urahisi zaidi.
“Mwitikio mkubwa wa wananchi wa Njombe ni ishara tosha ya uhitaji wa huduma hizi za uchunguzi na matibabu ya moyo na kuhimiza JKCI kutumia fursa hiyo kufanya tathmini ya kina itakayosaidia kupanga mikakati ya kufikisha huduma hizo kwa upana zaidi”.
“Kaulimbiu ya mwaka huu inayozungumzia umuhimu wa mazingira bora ya kisaikolojia mahali pa kazi ina uhusiano wa moja kwa moja na afya ya moyo, kwani msongo wa mawazo unaweza kuchangia ongezeko la magonjwa ya shinikizo la damu na matatizo ya moyo”, alisema Mhe. Sanga.
Waziri huyo wa Kazi aliwapongezata wataalamu wa JKCI kwa kutoa elimu ya jinsi ya kujikinga na magonjwa ya moyo katika maonesho hayo huku akisema imewasaidia wafanyakazi na wananchi kuelewa namna ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza kupitia mabadiliko ya mtindo wa maisha.
Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kutoka JKCI, Moses Manumbu alisema mwitikio wa wananchi wa Njombe umekuwa mkubwa na wenye hamasa ya kujua hali zao za afya.
Dkt. Manumbu alieleza kuwa watu wengi wamejitokeza kupima moyo na kupata ushauri wa kitaalamu huku wengi wao wakiomba huduma hizo ziendelee kutolewa hata baada ya maonesho hayo kukamilika.
“Tumebaini kuwa kuna watu wengi wanaishi na magonjwa yasiyoambukiza bila ya wao kufahamu hali inayoonyesha umuhimu wa uchunguzi wa mara kwa mara. Wananchi wameonesha uhitaji mkubwa wa huduma hizi kuendelea kufikishwa hapa Njombe angalau mara moja au mbili kwa mwaka”, alisema Dkt. Manumbu.
Naye Paulo Mbando mkazi wa Njombe alisema amenufaika na huduma hizo kwa kupima afya ya moyo bure pamoja na kupata elimu ya mtindo bora wa maisha kutoka kwa wataalamu wa JKCI, huduma hizo ni matokeo ya juhudi za Serikali ya awamu ya sita katika kuboresha huduma za afya na kuwajali wananchi wake.
“Leo nimepata fursa ya kupima moyo bila gharama na kupewa elimu muhimu itakayosaidia kulinda afya yangu. Hii ni hatua kubwa kwetu wananchi, naamini kupitia elimu hii nitaweza kujilinda nisipate magonjwa ya moyo”, alisema Paulo.









No comments:
Post a Comment