Na. Mwandishi Wetu Dodoma.
Serikali imesema kuwa kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inaendelea
kufanya tathmini ya mahitaji ya ujenzi wa Kituo cha Forodha katika Jimbo la
Momba, ikiwemo upembuzi yakinifu, upatikanaji na utambuzi wa eneo, gharama za
mradi na utayari wa nchi jirani.
Hayo yalisemwa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe.
Laurent Deogratius Luswetula (Mb), alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Momba,
Mhe. Condester Michael Sichalwe, aliyetaka kujua wakati ambao Serikali itajenga
kituo cha forodha katika Jimbo la Momba mkoa wa Songwe.
Alisema eneo hilo linaangaliwa kwa kuzingatia ongezeko la shughuli za
biashara na umuhimu wake katika kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato na
udhibiti wa biashara mipakani.
’’Ujenzi wa vituo vya forodha, ikiwemo katika Jimbo la Momba, hufanyika
kwa kuzingatia vipaumbele vya Serikali, ukamilifu wa taratibu na kanuni za
kiforodha, utayari wa nchi jirani tunazopakana nazo, masuala ya kiusalama,
upatikanaji wa rasilimali fedha, pamoja na tathmini ya umuhimu wa eneo husika
katika shughuli za biashara za mipakani,’’ alifafanua Mhe. Luswetula.
Aliongeza kuwa ujenzi wa kituo hicho utaanza mara baada ya kukamilika kwa
maandalizi yote muhimu, ikiwa ni pamoja na kupatikana kwa fedha za utekelezaji
wa mradi katika bajeti ya Serikali na kutangazwa kwenye Gazeti la Jumuiya ya
Afrika Mashariki.
Aidha, Mhe. Luswetula alieleza kuwa TRA inaendelea na maandalizi na itatoa taarifa rasmi pindi ratiba ya utekelezaji wa ujenzi itakapokamilika na kuielekeza TRA kuharakisha tathmini hiyo ambayo iko katika hatua za mwisho.








No comments:
Post a Comment