Na: OWM (KAM) –
Mwanza
Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, amesema kuwa
taasisi za dini zina mchango mkubwa katika kuimarisha ustawi wa jamii kwa kutoa
huduma za kiroho, maadili na malezi bora, hatua inayochangia kwa kiasi kikubwa
kuwa na maendeleo endelevu ya Taifa.
Aidha, amesema
dhamira hiyo imedhihirishwa kwa vitendo na Serikali ya Awamu ya Sita
inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kwa kushirikisha Taasisi za Dini katika masuala mbalimbali
nchini.
Waziri Sangu amesema
hayo Aprili 19, 2026 alipomwakilisha Waziri Mkuu, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba
katika Harambee ya Ujenzi wa Kanisa Kuu la Jimbo Katoliki Rulenge, Ngara.
Harambee hiyo imefanyika katika ukumbi wa Kwatunza Beach Arena, Jijini Mwanza.
Akisoma hotuba hiyo,
Waziri Sangu amesema Mheshimiwa Waziri Mkuu amewaomba Viongozi wa dini
kuendelea kuwalea kiroho vijana ili waendelee kuwa na maadili, tabia njema,
wazalendo na wenye kupenda Taifa lao, malezi bora kwa lengo la kuwa na jamii
tulivu na yenye amani.
Vilevile,
amehamasisha ushirikiano baina ya Serikali na makundi mbalimbali ya kijamii
ikiwemo Taasisi za Dini. Ameongeza kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu
Hassan ameanzisha jukumu hili matamanio yake ni kuona Mahusiano baina ya
Serikali na Makundi hayo ya Kijamii yanaendelea kuimarika kwa kudumisha tunu za
Taifa ambazo ni amani, upendo, mshikamano na umoja wa Kitaifa.
Katika harambee
hiyo, Mhe. Sangu amefanikiwa kuchangisha zaidi ya shilingi Milioni 114,982,000
ambapo katika pesa hiyo Waziri Mkuu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba amechangia
Tsh. Milioni 30 taslimu.
Naye, Muhashamu Baba
Askofu wa Jimbo la Rulenge Ngara, Severine Niwemugizi amesema ujenzi wa kanisa
hilo hadi kukamilika utagharimu shilingi bilioni 7.7 ambazo zitahusisha gharama
za ujenzi na ununuzi wa thamani za kanisa.
Kwa upande mwengine,
ameipongeza na kuishukuru Serikali kwa kuendelea kushirikiana kwa karibu na
taasisi za dini nchini, akieleza kuwa ushirikiano huo umechangia kwa kiasi
kikubwa kuimarisha ustawi wa jamii. 
Viongozi na wageni mbalimbali wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu (hayupo pichani) alipomwakilisha Waziri Mkuu, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba katika Harambee ya Ujenzi wa Kanisa Kuu la Jimbo Katoliki Rulenge, Ngara, hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Kwatunza Beach Arena, tarehe 19 Aprili, 2026 Jijini Mwanza.
Muhashamu
Baba Askofu wa Jimbo la Rulenge Ngara, Severine Niwemugizi akieleza jambo
wakati wa Harambee ya Ujenzi wa Kanisa Kuu la Jimbo Katoliki Rulenge, Ngara,
hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Kwatunza Beach Arena, tarehe 19 Aprili,
2026 Jijini Mwanza.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Sangu, akiongoza zoezi la harambee ya kuchangia Ujenzi wa Kanisa Kuu la Jimbo Katoliki Rulenge, Ngara katika ukumbi wa Kwatunza Beach Arena, Aprili 19, 2026, Jijini Mwanza.










No comments:
Post a Comment