Na Saidi Saidi, WMJJWM – Dodoma
Serikali imeanza kuchukua hatua madhubuti kukabiliana na mmomonyoko wa maadili nchini unaochochewa na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii, maudhui yasiyofaa pamoja na kulegalega kwa malezi ndani ya familia. Hayo yamebainishwa leo Mei 8, 2026 jijini Dodoma, ambapo Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mheshimiwa Dkt. Dorothy Gwajima, ameongoza kikao kilichowakutanisha mawaziri wa kisekta na manaibu mawaziri kujadili hatua za pamoja za kudhibiti mmomonyoko wa maadili nchini.
Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Gwajima amesema wizara yake imepokea malalamiko mengi kuhusu ukiukwaji wa maadili, ikiwemo usambazaji wa maudhui yasiyofaa mtandaoni, burudani zinazokiuka maadili ya Kitanzania pamoja na huduma zinazotolewa kinyume na utu na staha ya jamii.
Aidha, Dkt. Gwajima ameeleza mapendekezo ya Kamati ya Wataalamu kuhusu hatua za haraka yamejumuisha umuhimu wa kuundwa kwa kikosi kazi maalum cha ufuatiliaji wa maudhui mtandaoni na kuwachukulia hatua za kisheria wanaosambaza maudhui yanayoharibu maadili ya jamii.
Amesema, mafanikio ya mapambano dhidi ya mmomonyoko wa maadili yatategemea ushirikiano wa wizara, taasisi, familia na jamii kwa ujumla, huku akihimiza matumizi salama ya teknolojia kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho. Aidha, alisisitiza kaulimbiu ya “Maadili Yetu, Taifa Letu” kuwa msingi muhimu wa kulinda utamaduni, umoja na ustawi wa Tanzania.
Kwa upande wake, Waziri wa Katiba na Sheria, Mheshimiwa Juma Homera, amesema wizara yake ipo tayari kupokea mapendekezo ya maboresho ya sheria ili kuimarisha udhibiti wa vitendo vinavyokiuka maadili ya jamii. Amesema Serikali itaendelea kuhakikisha sheria zinaendana na mabadiliko ya teknolojia na mazingira ya sasa kwa lengo la kulinda mila, desturi na maadili ya Kitanzania.
Katika kikao hicho, mawaziri na manaibu mawaziri walitoa mawazo mbalimbali na kusisitiza kuwa, watuhumiwa wa ukiukwaji wa maadili wakabidhiwe kwa Wizara ya Mambo ya Ndani kwa hatua za kisheria, huku orodha yao ikiendelea kuhuishwa.










No comments:
Post a Comment